IMEGUNDULIKA kwamba Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM) ndiye mfadhili mkuu na mpanga mikakati mkuu wa kundi linalomfuata Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), ambalo limeanzisha chama kipya cha siasa, Alliance for Change and Transparency (ACT-Tanzania).

Kwa wiki kadhaa za hivi karibuni, makundi ya wanachama, washauri na wapanga mikakati wa Lowassa na Zitto wamekuwa wakikutana katika maeneo kadhaa jijini Dar es Salaam na kupeana mbinu, lengo kuu likiwa ni jinsi ya kumega Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika mapande ili kidhoofike kabla ya uchaguzi mkuu 2015.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari, Lowassa amejiaminisha kwamba ndiye atakayekuwa mgombea urais kupitia CCM. Kazi kubwa anayoona mbele yake ni kuanza mapema kusambaratisha CHADEMA ili kupunguza upinzani wakati wa kampeni utakapofika.

Zitto naye, ambaye uanachama wake kwa CHADEMA umebaki kwenye makaratasi tu, anatajwa kuwa ndiye mwasisi mwenza wa ACT, na amekuwa na uhusiano wa “kikazi” na Lowassa, hata kabla hajaingia kwenye matata ya wazi na chama chake, ambacho mwishoni mwa mwaka jana kilimvua vyeo vyake vyote vya uteuzi ndani ya CHADEMA kwa tuhuma mbalimbali.

Katika hatua mojawapo, chanzo kimoja kilicho karibu na Lowassa kimesema kwamba mapema mwaka juzi, Zitto alimwendea Lowassa na kumwambia kuwa mustakabali wake kisiasa ndani ya CHADEMA si mzuri, na kwamba alikuwa tayari kumsaidia Lowassa kufanikisha malengo yake, lakini kwa sharti kwamba iwapo mbunge huyo wa Monduli atafanikiwa kupata urais, basi amteue kuwa Waziri Mkuu.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, kauli hiyo kwanza ilimstua Lowassa kwa sababu ilimuonesha Zitto kama kiongozi asiye mwaminifu, ambaye yupo tayari kufanya hujuma dhidi ya chama chake, jambo ambalo lilimfanya Lowassa atilie shaka lengo la ombi hilo.

Jambo la pili lililomshtua Lowassa ni cheo kilichopendekezwa na Zitto, maana kwa mujibu wa Katiba ya sasa, Waziri Mkuu lazima atokane na wabunge wa majimbo, na awe kwenye chama chenye wabunge wengi.

Kwa kuwa hoja hiyo ilitolewa katika mazingira ya Katiba ya sasa, na kwa kuwa haikujulikana wakati ule kama Zitto alikuwa bado ni mwanachama na kiongozi wa CHADEMA, Lowassa hakuipata nafasi kauli hiyo, lakini amekuwa anaitumia kujadili sura halisi ya Zitto.

Hata hivyo, taarifa zinasema uhusiano wao umeimarika baada ya Zitto kuchukuliwa hatua na CHADEMA, huku wapambe wa Lowassa wakipita huku na kule kusambaza propaganda kuwa CHADEMA bila Zitto inakufa.

Taarifa ambazo hazijathibitishwa zinasema Zitto anatarajiwa kujiunga rasmi na ACT mwanzoni mwa mwezi Septemba mwaka huu, na timu ya Lowassa imedhamiria kumfadhili ili kujenga taswira ya mpasuko ndani ya CHADEMA, na kuipa CHADEMA mpinzani mpya ambaye ataifanya ishindwe kumfuatilia na kumshambulia Lowassa.

Katika kikao cha mwisho kilichofanyika kati ya timu ya Lowassa na “Vijana wa Zitto” kilijumuisha baadhi ya wapambe wakuu wa Lowassa wenye kauli ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM, watu wa karibu kifamilia na Lowassa na washauri wa karibu wa Zitto, akiwamo Mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Ajenda zao nje nje

Moja ya ajenda zao kuu ni kufadhili na kupandikiza watu ndani ya mfumo wa CHADEMA ambacho kinaendelea na uchaguzi wa ndani, ili wapate nafasi za uongozi, wazitumie kupata taarifa na mipango ya chama, na baadaye wajivue nafasi hizo na kukimbilia ACT, na kuleta msisimko wa kitaifa.

Gazeti hili lina taarifa kutoka kwa baadhi ya viongozi wa sasa wa CHADEMA ambao “Vijana wa Zitto” wamekuwa wakiwapigia simu na wakati mwingine kuwatembelea na kuwashawishi ahadi ya fedha na vyeo ili wajiondoe CHADEMA.

Baadhi hao ni viongozi wa majimbo na mikoa ambao katika uchaguzi unaoendelea ndani ya chama hawana uhakika wa kuchaguliwa kutokana na upinzani mkubwa unaojitokeza baada ya chama kukua na kuvutia wasomi na wafanyabaishara wenye mvuto katika maneo yao.

Baadhi ya viongozi walioendewa au kupigwa simu wamechukua tahadhari, na wametoa taarifa panapohusika ndani na nje ya chama.

Mbinu mojawapo ambayo imekuwa inatumiwa na “Vijana wa Zitto” kujaribu kuvunja ngome za CHADEMA ni kuwatangazia viongozi hao kwamba ipo idadi kubwa ya wabunge wa CHADEMA wanaotarajia kujiunga na ACT. Wanawataja majina kama njia ya kujenga ushawishi.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi hao wameliambia gazeti hili kuwa wanajua hizo ni mbinu za kipropaganda. Na baadhi ya wabunge wanaotajwa wamesema hizo ni mbinu za Zitto kutaka kuwagombanisha na chama chao na kujitafutia njia mpya kwa kutumia majina yao.

Mmoja wao alisema, “Zitto mwenyewe ameshalikoroga. Sasa hii ni tabia ya kututaja baadhi yetu, mimi na wenzangu kadhaa tumeshasikia, ni ile ile roho mbaya ya tukose wote. Kwa kuwa yeye amekosana na chama, anatafuta watu wa kufa naye.”

Mbali na kupandikiza wagombea nafasi za uongozi na kuvizia viongozi wanaoogopa joto la uchaguzi ndani ya chama, wamekuwa pia na mbinu ya kushawishi baadhi ya “wagombea watarajiwa” katika baadhi ya majimbo, wanaotajwa kuweka nia ya kugombea nafasi za uongozi kupitia CHADEMA.

Makada kadhaa kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wamezungumza na gazeti hili na kutumia kauli zijazofanana. Kwa mfano, makada sita walioweka nia ya kugombea ubunge katika majimbo kadhaa ya kanda ya Ziwa Mashariki na Magharibi, wamekiri kwamba kila wanapojadili mkakati huu na “Vijana wa Zitto,” kila mmoja wa nafasi yake anapewa ahadi ya kupewa pesa zote za kufanyia kampeni.

Vile vile, baadhi yao wamesema kuwa wanaambiwa kwamba iwapo watakubaliana na mpango huo wa ACT, moja kwa moja watakuwa wamepitishwa, maana chama hicho hakina mpango wa kupata wagombea kwa kutumia kura za maoni.

Taarifa zinasema sehemu ya malengo ya vikao ya Zitto na Lowassa ni kutafuta pesa kwa ajili ya mradi huu.

Zipo taarifa zisizothibitishwa kwamba mwezi uliopita Lowassa aliambatana na Zitto katika ziara ya kimya kimya ya Mkoa mmoja wa kanda ya Ziwa ambako anasemekana anataka kujenga ngome nzito ya ACT.

“Ninachojua ni kwamba iwapo ACT itafanikiwa kupunguza makali ya CHADEMA, Mzee atapita kirahisi, maana kikwazo kikubwa alichonacho hadi sasa hakipo ndani ya CCM, bali CHADEMA,” alisema mtoa taarifa wetu aliye karibu na Lowassa, ambaye hakutaka kuthibitisha kama wawili hao walisafiri pamoja kwenda Kanda ya Ziwa

Chanzo: Tanzania Daima

===================

Lowassa akanusha:

Quote By Ofisi ya Lowassa (mb) View Post
Katika gazeti la Tanzania Daima toleo na.3536 la tarehe 30 Julai, kuna habari inayosema Lowassa aibukia ACT na kumuhusisha na Mbunge wa Kigoma Kaskazini(CHADEMA) Zitto Kabwe katika kile gazeti hilo kilichodai mikakati ya siri dhidi ya Chadema.

Habari hizo ni uzushi, na ni muendelezo wa mikakati ya kumchafua na kumgonganisha Mh Lowassa na wanasiasa wenzake wa kada na maeneo mbalimbali. Mh Lowassa kama walivyo wabunge wengine wa CCM amekuwa na uhusiano na wabunge wenzake bila kujali tofauti ya vyama vyao.

Mh Lowassa ni kiongozi makini ambaye hawezi kupoteza muda wake kujiingiza katika masuala yasiyo na tija kwa nchi, wananchi na ustawi wa demokrasia makini na endelevu nchini.Muda wake anautumia kusimamia utekelezwaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM jimboni kwake Monduli. "Mimi na chama chetu, tuko busy kutekeleza ilani yetu,kuwaletea maendeleo wananchi ili wazidi kutupa ridhaa ya kuwaongoza katika chaguzi zijazo" alisema Mh Lowassa.

Hata hivyo,Mh Lowassa anathamini mchango wa vyama vyote vya siasa nchini pamoja na Chadema katika kujenga demokrasia yenye tija kwa taifa.

Imetolewa na ofisi ya Mh Edward Ngoyai Lowassa (mb)
ACT pia wakanusha:
Quote By Peter Mwambuja View Post
Wana JF,

Naomba kwanza nijitambulishe. Naitwa Peter Mwambuja. Ni Mtunza Hazina na Mhasibu Mkuu wa ACT-Tanzania. Napenda kukanusha taarifa zilizoandikwa kwenye Gazeti la Tanzania Daima la leo kama ifuatavyo. Kwa kuwa chama chetu kinasimamia uwazi kama moja ya misingi mikuu, naambatanisha taarifa ya fedha iliyowasilishwa katika Kikao cha Halmashauri Kuu kilichofanyika tareje 25-26 Julai 2014. Namkaribisha mtu yeyote anayetaka kupata orodha wa wanchama, wapenzi na wananchi waliotuchangia hadi sasa. Kwa sababu za kitaaluma, siwezi kuanika majina ya watu waliotuchangia hapa jukwaani.

1. Katika toleo lake la siku ya Jumatano ya tarehe 30 Julai 2014 Gazeti la Tanzania Daima limechapisha habari zilizodai kuwa mwanasiasa moja maarufu hapa nchini ndiye mfadhili mkuu wa Chama cha ACT-Tanzania.

2. Kwa niaba ya uongozi wa ACT-Tanzania, na kwa nafasi yangu kama Mtunza Hazina na Mhasibu Mkuu wa ACT-Tanzania, napenda kuwataarifa wanachama na wapenzi wa chama na wananchi kwa ujumla kuwa taarifa hizi ni uzushi na uwongo wenye lengo la kuchafua taswira ya chama cha ACT-Tanzania. Napenda kuutaarifu umma kuwa moja ya misingi mikuu ya ACT-Tanzania ni uadilifu na uwazi. Kwa misingi hii, vyanzo vya mapato na matumizi ya ACT-Tanzania yapo wazi kwa mtanzania yeyote anayetaka kujua ukweli.

3. Tangu chama kianzishwe mwezi Januari mwaka huu, kimeshapokea na kutumia jumla ya shilingi 74, 857,000/= (milioni sabini na nne laki nane na elfu hamsini na saba) zilizochangwa na wanachama, wapenzi na wananchi wasiopungua 50 wanaouunga mkono misingi ya chama hiki. Taarifa ya kwanza ya fedha ya chama iliwasilishwa katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya ACT-Tanzania katika mkutano uliofanyika Mjini Singida tarehe 25-26 Julai 2014.

Kwa mtanzania yeyote ambaye angependa kuona orodha ya watu waliokichangia chama anakaribishwa kufika ofisi ya Makao Makuu iliyopo Ubungo National Housing mkabala na Hoteli ya Royal Njombe.

Pamoja na salamu za uzalendo za ACT-Tanzania

Peter Mwambuja, PGDA, CPA (T)
Mtunza Hazina na Mhasibu Mkuu wa ACT-Tanzania.
Imetolewa Jumatano 30 Julai 2014