Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Saturday, March 29, 2014

SAUTI KUTOKA NYIKANI.....RAIS KIKWETE SASA AMEPUMUA


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa Bungeni mjini Dodoma akihutubia Bunge maalum la Katiba.

NA GORDON KALULUNGA

‘’NITAILINDA na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania’’ hiki ndicho kiapo alichokiapa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alipokuwa akiingia madarakani.

Watanzania walikichagua Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuendelea kuongoza dola kutokana na ilani ya chama hicho na mwelekeo wake.

Katika ilani ya chama hicho 2015-1015, hakuna mstari wowote ambao umeeleza kuwa CCM ikiingia madarakani itaanzisha mchakato wa Katiba mpya.

Sina uhakika kama Kamati kuu au Halmashauri kuu ya CCM, kama ilimhoji Rais Kikwete ambaye ametuleta ilani ambayo haipo kwenye maandishi ya chama madhubuti, CCM.

Kuna dalili za ilani ya Kikwete kuhusu Katiba mpya kukataliwa na wananchi, kama vikao havikuipitisha na itakuwa aibu kwake na chama chake.

Anguko la ilani hiyo ambayo baadhi ya wana CCM, wengi hawajui ilikotoka, ingawa baadhi wanajua kuwa ilikuwa ni ilani ya upinzani, inaweza kufuatiwa na maanguko ya  mipango iliyotangulia.

Mipango iliyoanguka bila mafanikio chanya ni pamoja na Oparesheni tokomeza ujangili, Oparesheni kimbunga na tuendako naiona ‘’Oparesheni’’ Big Result Now(BRN).

Mpango ambao unaonesha matunda ni Shule za sekondari za kata.

Ingawa kunaonekana kuna mapungufu, lakini madarasa yapo kidogo, walimu wapo hata kama hawatoshi, vitabu vipo hata kama havitoshi na mapungufu yanayoonekana ni kutokana na mwenye wazo kuwa nje ya ulingo, Waziri mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa.

Wiki iliyopita, niliisikia hotuba ya Rais Kikwete. Hotuba yake ilisambaratisha magenge yaliyokuwepo mtaani yakibishana kuhusu Rasimu ya mabadiliko ya katiba.

Hotuba hiyo, imenikumbusha ujumbe wa wimbo wa Ngozi ya Kitimoto haiwambwi ngoma na ngoma ya watoto huwa haikeshi.

Licha ya mimi kuwa muumini wa serikali moja, Bunge hilo naamini limemaliza kazi yake au litavunjika.

Kazi iliyobaki kwa sasa ni wajumbe kupata posho na kubishana kuhusu uwingi wa wajumbe kutoka kwenye vyama vyao kana kwamba ndicho walichotumwa na waliowateua.

Rais Kikwete alieleza jinsi gani baadhi ya wajumbe walitaka kufanya uhaini wa kisayansi dhidi ya serikali yake.

Ninapozungumzia suala la uahini wa kisayansi nina maana ya suala zima la kuuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, wengine huita Tanzania Bara na Visiwani.

Njia iliyokuwa ikitumika ni ile ya kutaka serikali tatu, ambazo Rais Kikwete aliamua kueleza msimamo wake kama mkuu wa nchi, kuwa hayupo tayari kuona nchi inaharibikia mikononi mwake na historia ikamuhukumu.

Hakuna ubishi kuwa watu wengi wanaogopa mabadiliko.
Muungano huo watu wa nyikani wanasema una historia yake, wanadai kuwa usingekuwepo, Zanzibar isingepona kupinduliwa na mataifa makubwa…

Naamini idara za ulinzi na usalama, zilimwepusha Rais kudhihakiwa na kusimangwa na mtoto wa eneo la Nyamuswa, tarafa ya Ikizu, wilaya ya Bunda mkoa wa Mara.

Watu wa nyikani wanasema kuna mpango uliokuwa umepangwa kwa ajili ya kumdhalilisha na kumkebehi Rais Kikwete, kupitia uwasilishwaji wa rasimu ya Jaji Warioba.

Mimi siamini lakini wao wanasisitiza kuwa, mpango huo wa kisayansi ambao vyombo vya ulinzi na usalama viliung’amua ni suala zima la nani aanze kulihutubia Bunge hilo maalum la katiba.

Inaelezwa kuwa, endapo Rais Kikwete angetangulia kulihutubia na kulifungua bunge hilo, baadae angekuja Jaji Warioba kuwasilisha rasimu ya katiba na kukazia kauli zake za ‘’Serikali tatu haziepukiki’’, Rais angeonekana kuwa alichoongea hakikuwa na mashiko.

Watu wa nyikani, wanasema, eti tangu awali walishangazwa na uteuzi wa Rais Kikwete kumteua Jaji Warioba kuwa Mwenyekiti wa tume hiyo!

Sababu wanayoitoa, eti wanawajua vema akina Kitine, Butiku na Warioba dhidi ya Rais Jakaya Kikwete na serikali yake.

Wanasema kutokana na demokrasia inavyokua hapa nchini, leo hii hakuna sheria ya kumlazimisha mtu kuvaa tai.

Hivyo kila mmoja anavaa awezavyo huku wengine wakivaa hata kiunoni.

Watu wa nyikani wanatamani kuwa na katiba ya kutukutanisha wakati wowote, kwa jambo lolote linalohusu utaifa wetu.

Katiba inayosimamia misingi ya utu, haki za binadamu, afya, mazingira, ulinzi wa mipaka yetu na rasilimali zetu, inayotafuta fursa za ndani na nje ya Tanzania, kupanua upeo wa fikra na utendajikazi.

Yenye mahusiano na asasi za ndani na nje zinazopigania umuhimu wa waandishi wa habari, kujisimamia katika utekelezaji wa kazi zao badala ya kushikiwa kiboko na watawala.

Wanasema lakini hawana uhakika kama hii ndiyo Katiba inayotafutwa chini ya rasimu ya Jaji Warioba.

Wanakumbuka kuwa eti, hivi karibuni, kuna baadhi ya vyombo vya habari vilimnukuu Jaji Warioba akiwasihi wabunge wa bunge la katiba kuwa wasiyaondoe yale aliyoyaandika kwenye rasimu yeye na wenzake.

Kauli yake haikuwasikitisha watu wa nyikani kwasababu eti ilionesha ni jinsi gani alijaa hofu ya kuondolewa yale yanayodhaniwa kuwa ni mawazo yake yaliyomo kwenye rasimu.

Kuna wakati nilitumwa na Bibi na shangazi kumweleza jambo Jaji Warioba.

Walisema kuwa waliwasikia baadhi ya watu wakisema eti, katika Rasimu, maoni mengi yaliyoandikwa yalikuwa ni ya Warioba na wasiomtakia mema Rais Kikwete na Muungano.

Yote hayo yalikuja kutokana na mawazo yaliyokusanywa mwanzo kuungwa mkono na watu wa upande wa pili na ndiyo yalitaka kumkosanisha na ‘’mke’’ wake wa kwanza(CCM).

Shangazi mpaka sasa anazidi kusisitiza na kukumbusha kuwa, Warioba asikate tamaa, ila asisahau kuwa eti baadhi ya watu hawasahau historia.

Baadhi ya watu wanahisi eti Jaji amehama nayo yale aliyowahi kuyasema awali, wakati yeye Jaji anasema ni mawazo ya sasa na siyo yake bali ni ya watu ingawa naye wakati ule aliwahi kuwa na mawazo kama hayo na aliwahi kuyatamka.

Huku kwetu nyikani kuna msemo usemao, Maisha siku zote hatuhesabu kwa karne au miaka, bali ni sekunde za thawabu zinazoweza kuleta mabadiliko.

Ninachokiona ni kwamba tusiendelee kujadili hotuba za wakubwa hawa, bali wajumbe wajadili wanachotaka wananchi na kama hawakijui, basi Bunge liahirishwe waende wakawaulize kisha warudi kutengeneza Katiba.

MAKALA HII PIA INAPATIKANA GAZETI LA MTANZANIA JUMAPILI TAREHE 30/03/2014

Mwandishi wa makala haya, anapatikana kwa simu  
0754 440749
Email; kalulunga2006@gmail.com

No comments: