Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Monday, April 21, 2014

SINTASHANGAA KUONA KATIBA MPYA IKIKATA NA NYEMBE VIZAZI VYETU


NA GORDON KALULUNGA

KATIKA historia ya kutoka Nyikani kuelekea Jijini Dare es Salaam, siwezi kuisahau historia chungu inayohitaji majibu ya vitendo.

Historia hiyo ilitokea April 14, mwaka huu, yalipo katika mawasiliano ya Barabara eneo la Ruvu mkoani Pwani ambako nami nilionja joto la jiwe la kulala porini na abiria wenzangu kisha kufika saa kumi na moja alfajiri siku iliyofuata.

Walikuwepo wajawazito. Watoto wachanga na chini ya miaka mitano. Wazee na vikongwe nao walikuwemo kwenye msululu mrefu wa magari kila aina yaliyozuiwa kupita katika eneo la Ruvu kutokana na maji kujaa.

Madaraja nayo kila kona ya kuingia na kutoka Dar es Salaam, yakiwa yameharibika kwa kusombwa na maji!

Nikiwa nakaribia kupata usingizi majira ya saa tisa usiku ndani ya basi kutoka Jijini Mbeya kuelekea Dar es Salaam, kuwa kiranja wa baadhi ya wanahabari wa masuala kupambana kuzuia vifo vya Mama na mtoto, nikajiuliza maswali mawili makubwa kwa akili za watu wa Nyikani, lakini mepesi kwa wanaojadili katiba mpya.

Mambo hayo ni kwamba je? Mji mashuhuri wa Tanzania Jiji la maraha, Dar es Salaam ni kisiwa? Je mji huu ambao unaelezwa kuwa ndiyo kila kitu katika nchi hii, kumbe unaweza kutekwa kirahisi hivi na watu wake wakakosa kwa kukimbilia huku chakula kutoka kwenye mikoa inayozalisha kikishindwa kuingia?

Hapa sitaki kuendelea, maana ninaweza kujikuta naitwa mchochezi na Gazeti hili likafungiwa kwa kusema ukweli mchungu, ingawa siku zijazo nitaeleza jinsi Malori ya Magufuli, ambavyo hayawezi kuharibu Barabara na madaraja bali uchakachuaji wa ujenzi unavyofanywa.

Lakini ikumbukwe kuwa, mambo ya Kienyeji yanahitaji ufumbuzi wa wenyeji.

Tarehe 25 mwezi huu wa Nne, Bunge la katiba litahailisha shughuli zake kupisha sikukuu za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na bunge la bajeti kuendelea hadi litakapoitwa tena.


Kwa tafsri nyingine  Bunge la malumbano kwa sisi tunaopenda malumbano na kulishwa chuki tutalimisi sana.

Tutalimisi kwa kukumbuka yale tuliyokuwa tukiyapenda hususani vijembe.

Zitakumbukwa siku sabini za kutupiana vijembe vyenye tafsri ya kutumwa na wananchi wakati ki-msingi hayo si mawazo ya wananchi wa kawaida, bali wanasiasa.

Malumbano hayo ya wanasiasa yamefanya bunge kubeba mzigo wa uhasama wa vyama, ukanda na makundi ndani ya Tanzania.

Majawabu mazito ambayo yalitazamiwa kujibiwa na katiba mpya yanaonekana kujibiwa na majibu mepesi yasiyo na tija kwa kipindi cha miaka mingi ijayo.

kuna kila dalili za kupata katiba dhaifu au njiti kama nilivyoeleza juma lililopita, itakayotokana na pesa nyingi za walipa kodi ambao bado maisha yao ni duni sana.


Pesa wanazopata wajumbe hao, zingetosha kumaliza malalamiko ya walimu na chenji zingelekwa katika suala la kampeni za kuzuia vifo vya mama na vichanga vyetu.

Suala la muungano limetuonesha uchu wa madaraka wa baadhi ya viongozi wetu wanaojifanya watetezi wa haki za wanyoge na misimamo ya kizamani kwamba tuweza kumuunga mkono mtu, alimradi tu ni mwenzetu  tena kwa nguvu sana bila kujali madhara ya misisimamo hiyo.

Mishipa ya vichwa imesimama kutetea miundo ya muungano na kutaka nafasi za kutawala, lakini mishipa hiyo imelala katika kusema changamoto zilizomo ndani ya muungano zitatatuliwa vipi na miundo hiyo inayo piganiwa.

Rais wa Umoja wa vyama vya waandishi wa habari Tanzania(UTPC), Kenny Simbaya, mara kadhaa ananukuliwa akisema ‘’Kuna watu wanailaumu serikali kwa kila jambo lakini wanasahau kuwa kabla ya kulaumu vitu vingi hapa duniani kila mmoja anatakiwa awajibike kwanza mahali alipo na kuwa mfano’’

Nukuu hii inanikumbusha kuwa, matatizo ya kimaisha kwa wananchi matharani Afya, elimu, kilimo, ufugaji, miundo mbinu, usalama, haki za kisheria, uraia na mengine mengi, wachache wanaojali.

Wanasiasa wameteka mjadala wa katiba na ki-msingi wamejitahidi kutetea maslahi yao zaidi ingawa wao wanayaita mawazo ya wananchi.

Ukiwauliza wananchi ambao siyo viongozi wa siasa hawajui lolote kuhusu wanachodai kuwa walikitoa kwenye tume, hata shangazi yangu naye hajui.

Wanasema kuwa eti mawazo wanayoyataka baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo ni maoni ya wananchi na wala siyo ya wana CCM.

Najenga mashaka. Swali dogo la kujiuliza ni kwamba je? Wana CCM siyo wananchi wa Tanzania? Wanajuaje kuwa maoni yaliyotolewa kwenye Tume ya Jaji Joseph Warioba, hususani suala la Muungano hawakuwemo wana CCM?

CCM inakadiliwa kuwa na takribani ya wanachama zaidi ya Milioni sita na laki tano. Tume ya Jaji Warioba ilikusanya maoni ya mabadiliko ya Katiba kwa watu wasiozidi Laki tano!  Je hawakuwemo wana CCM?

Kwasababu wamaemua kutulisha uchafu wa mawazo hasi ya chuki, lakini ni vema tukaambiwa kuwa hao ni raia wa wapi na je! wanachama wa vyama vya upinzani ndiyo raia kamili wa nchi hii?.

Nasikitika kuibuka kwa kikundi kilichozima mbwembwe za Chadema!

Hapa sitaki kusema kuwa kuna kufirisika kwa mawazo ya viongozi wanaowabagua na kuwalisha chuki watanzania, bali najenga maswaka na suala zima la siasa safi na uongozi bora.

Maswali  machache yafuatayo ni vema watu wa nyikani nao wakapata majibu ili kwa pamoja tutafakari kama kuna ukweli wa wanachokidai hawa wateule waliojimilikisha akili za kurudi nyuma kwa kasi na kupandikiza chuki kila kukicha kwa walioamua kwa makusudi kuacha kufikiri bali kufikiliwa na wengine.

Hivi kati ya watanzania waliotoa maoni tume ya Jaji Warioba wanachama wa Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF, CCM au chama kingine walikuwa wangapi na walisema nini?

Lijibiwe swali hilo kwa nia njema ya kuuaminisha umma kuwa mawazo wanayoyasema kuwa ni ya wananchi na wala siyo ya CCM ni sahihi, vinginevyo tutarajie kuvuna Katiba ya nyembe kali, zitakazokatakata vizazi na vitovu vya vizazi vya viuno vyetu.

Mawasiliano ya Mwandishi wa makala hii ni 0754 440749
Email; kalulunga2006@gmail.com

No comments: