Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Thursday, April 24, 2014

KESHO NAMFIKISHA RAIS KIKWETE MAHAKAMANI


NA GORDON KALULUNGA

WIKI iliyopita, msomaji aliyejitambulisha kwa jina la Malya, alinipigia simu, tukajadili makala iliyohusu mchakato wa Katiba Mpya.

Tukajikumbusha kuwa Rais Jakaya Kikwete aliapa kuilinda na kuitunza Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tulijiridhisha kuwa Rais Kikwete, ameivunja katiba aliyoapa kuwa atailinda. Ameivunja kwa kuruhusu kuundwa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010. Inafaa ashitakiwe. Mimi nimejitolea, nitamshitaki kesho.

Pia Wabunge walioapa kuilinda Katiba iliyopo, nao wanapaswa kushitakiwa kwa kuivunja, kwa kutaka kuibadili badala ya kurekebisha.

Jaji Joseph Warioba, anajua fika mazungumzo ya awali ya Muungano kati ya Shekh Karume na Mwalimu Julius Nyerere, ambapo Karume alitaka nchi moja na kwamba yeye angekuwa mkuu wa mkoa lakini Mwalimu akasema wawe na subira!

Inasikitisha kuona kikundi cha mapenzi ya ghafla kilichojipa jina la UKAWA, kinatoka nje ya Bunge kana kwamba Katiba inatungwa nje ya Bunge! Kuna sm ikatafsiri kuwa kirefu cha Ukawa ni (Ujinga ni kawaida yetu wapinzani)!

Huo ulikuwa mchapo kidogo tu, lakini dhamira yangu ya kumshitaki Rais Kikwete kesho ipo pale pale na inaongozwa na matakwa ya watu wa nyikani ambao wanasema dosari zote zitaondoka ndani ya viganja vyake akimaliza uongozi.

Ili kupata maendeleo kuna njia mbili kuu ambazo ni kufikiri kwa kina ama kuiga jinsi mambo yanavyoweza kuendeshwa.

Tanzania tuna udongo, miamba na mawe ya kuweza kutengenezea barabara imara, lakini barabara zetu zinakuwa chini ya kiwango. (Ten Percent) wenye mamlaka ni moja ya tatizo. Je niache hata kwa jambo hili kumshitaki Rais Kikwete?

Tuangazie yatokanayo na Mvua zinazoendelea kunyesha na mustakabali wa Barabara zetu.

Wananyika wanasema hawasahau historia. Nyumba za serikali pale Msasani Jijini Dar es Salam, ziliishia kwenye mikono inayoelezwa kuwa si salama chini ya Rais Benjamin Mkapa na Waziri wake John Pombe Magufuli.

Lakini kwasababu Magufuli kama alivyo mwanamuziki mmoja wa kizazi kipya, kupendwa hata kama hakuna ujumbe wa maana anaouimba, hakuna anayejadili udhaifu unaofanywa chini yake, bali yote yanatupwa kwa Rais Kikwete na CCM.

Aprili 12-14 mwaka huu. Tumeshuhudia kuvunjika madaraja na barabara zilizo chini ya Wizara ya Waziri Magufuli, mbali na zile za Halmashauri na miji.

Angekuwa mwingine katika wizara hiyo hiyo, kelele zingepigwa na kulazimishwa kuwajibika,  lakini kwasababu yamefanyika chini ya Wizara ya Magufuli ni bahati mbaya.

Haishangazi kuona kwenye wizaya ya Ujenzi, masuala ya dharula ni muhimu kuliko kufanya ukarabati kwenye njia na kingo za kupitia maji kabla hayajajitokeza maafa.

Sitaki kuamini kuwa eti suala la dharula mipango ya kuiba pesa ni rahisi kuliko kazi zisizo za dharula!

Kuna uzembe wa makusudi unafanywa kwa ushirikiano mzuri kabisa kati ya wizara na wataalam kutoka Tanroad. Haliangaliwi suala la ubora hasa wakati wa ushindiliaji na ubora wa udongo.

Wakandarasi wanaopewa tenda, baadhi wanatengenezea barabara udongo wenye rutuba na mchanga, ili hali wakati wa kutafuta kazi walionyesha sampo nzuri ya udongo unaofaa(Moram).

Wakandarasi chini ya ukaguzi wa serikali, wanashindilia barabara na mashine zenye uzito mdogo kwasababu wakileta mashine zenye uwezo mzuri wa kushindilia barabara, wanakamatwa kwenye mizani.

Watendaji ambao tenda hizo zinapitia mikoni mwao, wanalazimisha kupewa Ten Percent kutoka kwa wakandarasi. Tunategemea ubora hapo?

Wenye mamlaka wanapeleka lawama za uhalibifu wa barabara kwa wasafirishaji hasa wale wenye magari ya mizigo!

Utafiti unaonesha kuwa, gari kubwa kila Excel moja ina uzito wa tani 8-10, uzito ambao hauwezi kuharibu barabara kama zitajengwa kwa kiwango kinachokusudiwa.

Kama kweli magari yenye uzito mkubwa yanaharibu barabara na madaraja yetu, je daraja la eneo la Ubungo -Mandela, Morogoro Road na Kurasini la Jijini Dar es Salaam na zile foleni lingetengenezwa kiholela kama zinavyotengenezwa barabara zetu, lingekuwepo au kumudu uzito?

Barabara ya mabasi ya kwenda kasi zinajengwa sasa Jijini Dar es Salaam. Mabasi hayo hayatapata nafasi wala umbali wa kwenda kasi kutokana na wembamba wake, likitokea tatizo, mabasi mengine yote yatasimama.

Katika nchi ya Malaysia na China, ambako viongozi wetu wanashindana kwenda, kuna barabara nyingi na wana mipango ya kujenga barabara za juu kwa kiwango cha maono makubwa na siyo ilani za matumbo ya wenye mamlaka.

Ni aibu kushindwa na nchi kama Nethaland, ambayo ni nchi ya kutengenezwa, lakini ina barabara nzuri za kuhimili uzito wowote.

Ushahidi huo pia unathibitishwa na kampuni ya usafirishaji ya Notebum, chini ya Mkurugenzi wake ambaye ni Mtanzania.

Tanroad kama wakala wa Serikali, wanafanya ukarabati wa Barabara kwa kukoka majani moto, kufyeka na kuziba viraka vya Lami kwa kutumia spedi!

Barabara hazina sehemu za dharula. Tanroad wakikuta gari mfano pale Kibaha, wanakamata kwa kosa la Wrong parking! Wanalipisha faini ya Tsh. 600,000/= papo hapo,  wao wakishitakiwa kwa ukiukwaji wa sheria na kushindwa, hawawalipi wadau wa sekta hiyo. Hii ni kamali inayokula upande mmoja.

Maandiko yanasema, ukweli unamweka mtu huru, tatizo kubwa hapa ni Ten percent kwa watendaji wa Serikali katika masuala ya manunuzi, usimamizi na utoaji wa tenda.

Natamani kipande cha barabara ya mfano, mkataba utolewe na Rais Kikwete mwenyewe, hicho kitakuwa imara na bora, kwasababu hatoweza kuomba Ten Percent kwa Mkandarasi.

Baada ya kushindwa kwenye Barabara, leo tunataka kuboresha Reli! Hiki siyo kiroja kipya. Tulishindwa kuendesha Tazara iliyokuwa na kila kitu, wakiwemo wataalam tuliokuwa tumesomeshewa na wachina, leo je tutaweza?

Serikali iwaeleza watanzania kuwa tuta la Reli ya Singida - Manyoni ni lini treni lilipita, na kwanini halipiti? pesa kiasi gani kilitumika? Na je waliochezea fedha hizo wako wapi?

Ni vema watawala wakapunguza kuwafanya Watanzania kama mazuzu wa kulipa madeni mpaka kifo chao na vizazi vyetu.

Tunatakiwa tupate kiongozi anayetoka katika uzao wa Farao usiomtambua Yusufu, ili kupunguza Rushwa, hapo tutapata vitu bora. Kwa haya na mengine, kesho naenda kumshitaki Rais Kikwete.

Natoa hoja.

0754 440749
kalulunga2006@gmail.com

No comments: