Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Monday, April 21, 2014

KIKWETE AMECHELEWA KULIITA JESHI-NDIMARA


Rais Jakaya Kikwete (kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Majeshi ya JWTZ, Jenerali Davis Mwamunyange (kulia)
 
YA KIKWETE, KARUME NA LUKUVI
Ni ghiliba, woga au uchovu kisiasa?


Na Ndimara Tegambwage

NAANZA kushindwa kuandika mara kwa mara. Kama ulimi unavyokwama ndivyo mkono unavyotetemeka. Hasa juu ya hili la watawala kusingizia jeshi kuwa litapindua serikali pindi nchi ikiwa na utawala wa mfumo wa serikali tatu.

Jeshi? Kutwaa madaraka? Kwa kuwa wananchi wametaka mfumo wa serikali tatu? Kwani jeshi linalinda nani, kama siyo wananchi? Hapana! Haya ni matusi kwa wananchi na jeshi lao.

Hadi sasa kauli hizo zimetolewa na Rais Kikwete, Balozi Ali Karume na hivi majuzi Waziri William Lukuvi. Eti serikali tatu zitakula fedha nyingi kiasi cha kuishiwa na kushindwa kulipa mishahara ya wanajeshi; na hapo wanajeshi watapata sababu ya kupindua serikali.

Woga wa kupinduliwa unatoka wapi? Tusaidiane: Watawala wamepata wapi woga wa kupinduliwa? Tangu lini wamekumbwa na woga huu? Labda ni hisia tu. Hilo laweza kukubalika; lakini hisia zinatokana na nini? Kutokana na maoni ya wananchi kwamba wanataka utawala wa mfumo wa serikali tatu?

Watawala wana maana kwamba majeshi yana uchungu mkubwa na fedha za wananchi/umma pale tu yatakapokosa mishahara na siyo yanapoona watawala wakishiriki au kunyamazia au kupuuza wizi, uporaji na ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi kutoka Benki Kuu (BoT) na Hazina; na ufisadi wa kila aina?

Haya ni matusi kwa jeshi. Niliishaandika hivihivi. Ni matusi pia kwa wananchi.

Sikubaliani na wanaodai kwamba kauli hizo za watawala zinachochea jeshi. Sikubaliani. Hakuna uchochezi wowote. Kuna kejeli. Kuna kebehi. Kuna dharau – kwa jeshi; na hata wananchi ambao ndio walipakodi na waajiri wa majeshi yote.

Angalia jinsi watoa kauli wanavyohema, wanavyoweweseka, wanavyomiminikwa jasho na mishipa kuwanaga usoni na shingoni. Polepole na taratibu, wanachumbia jeshi na kuliingiza katikati ya mjadala wa wananchi wa kuamua jinsi wanavyotaka kujitawala.

Wanahema kana kwamba wameambiwa au wameona "kikosi kinaingia nchini ili kusimika mfumo wa serikali tatu!" Ajabu! Kama kikosi hicho kipo, andishi hili liwe, mara moja, ombi langu rasmi la kuingia jeshini ili nishiriki kuzuia kikosi hicho kuingia nchini.

Lakini kama mfumo wa serikali tatu ni utashi na uamuzi wa wananchi wenyewe - na bado kuna fursa ya kupima hilo kwa njia ya kura ya maoni - majeshi yanakwenda wapi, badala ya kukaa imara kulinda utashi, matakwa na uamuzi wa wananchi?

Uanasiasa wa aina hii – ya kuita jeshi kutwaa madaraka – kwa kutumia mtindo wowote ule wa kejeli au vitisho kwa wananchi; ni hatari kwa usalama wa wananchi na taifa kwa jumla. Ni kupanda mbegu ya woga miongoni mwa wananchi; ingawa pia ni kuamsha hisia za kisiasa ndani ya majeshi; na kudhalilisha jeshi kuwa ni mali ya watu au kikundi fulani katika jamii.

Aidha, uanasiasa wa ngeli hii – ya vitisho na vitimbi – unaonyesha watawala waweza kuita jeshi la nje kukabiliana na jeshi la ndani; iwapo jeshi la ndani litakataa kukubali matakwa ya wachache wanaotaka kulitumia na wanaotaka kuzima matakwa na sauti ya umma. Hili ndilo tatizo la kutawaliwa na wanaoishi kwa mazoea na wachovu wasio na jipya.

Hadi sasa mjadala wa Katiba Mpya katika Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma, umesaidia wote wanaoufuatilia kujua fikra na upeo wa fikra wa watawala.

Hoja moja tu ya serikali mbili au tatu, imewafanya watawala wajiapize, watambe kuwa wao ni wengi katika Bunge la Katiba; watukane mwenyekiti wa Tume ya Katiba, washambulie na kubeza wajumbe wa Tume; na watishie wananchi kwamba “jeshi litapindua serikali.”

Hoja imewafanya warudi haraka kwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere; yule waliyepuuza, kuua na kuzika alichotamani na kupigania – Azimio la Arusha. Yule ambaye walipuuza miiko yake ya uongozi na maadili – vitu alivyosimamia. Angalia sasa wanaanza kumuimba, kumnukuu na kujiapiza kuwa hawakubali serikali tatu “...alizotuachia Baba wa taifa.”

Mbona watawala hawakumuimba Nyerere wakati wanavunja Azimio la Arusha? Mbona hawakumnukuu Nyerere wakati wanavunja miiko na maadili? Mbona hawakumsifu Nyerere walipokuwa wanauza mali ya umma – viwanda, majumba makubwa na nyumba za serikali? Mbona hawakuogopa jeshi kupindua serikali katikati ya ufujaji wa kiwango hicho?

Hoja ni kuwa na serikali tatu chini ya jina lolote lile – Muungano au Shirikisho; lakini watawala wamechonga ndimi na kupeperusha midomo yao wakidai ndani na nje ya Bunge, kwamba serikali tatu “zitaua Muungano,” na kwamba jeshi litawapindua.

Kinachoonekana machoni mwa watawala na katika kauli zao; ni kwamba hawaamini wanachosema. Wangekuwa wanaamini wasemacho, Zanzibar isingempokonya rais wa Muungano madaraka makubwa anayopewa na Katiba huku yeye na wenzake wakichekelea tu.

Kama kweli watawala wanaogopa serikali yao kupinduliwa na jeshi la wananchi kutokana na kuwa na mfumo wa serikali tatu; wanashindwaje kuelewa kuwa waliishapinduliwa zamani kwa rais kupokonywa mamlaka kadhaa kupitia Katiba ya nchi jirani – Zanzibar?

Walichelewaje kuita jeshi kulinda mamlaka ambayo rais alipewa na wananchi chini ya Katiba? Hakika utawala wa mazonge!


(imechotwa katika mtandao wa: ndimara.tegambwage.facebook.co m ya 17 Aprili 2014)

No comments: