Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Thursday, April 10, 2014

SAUTI KUTOKA NYIKANI;.......BUNGE LA KATIBA LINAONDOKA NA MAITI ILIYO HAI

 Makamu wa Rais Dkt Mohamed Ghalib Bilali, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Mohamed Chande Othman na Rais Mstaafu wa awamu ya pili Alhaj Ali Hassa Mwinyi na wajumbe wakifuatilia hotuba ya Rais Kikwete.Bunge la Katiba limeondoka na maiti iliyo hai

NA GORDON KALULUNGA....0754 440749
kalulunga@gmail.com

BUNGE maalum la Katiba limeahirishwa. Watu wa Nyikani tumefurahi sana. Kwasababu hawajafanya lolote ukilinganisha fedha na muda walioutimia.

Kwakuwa mimi ni mshauri wa Rais katika masuala madogomadogo muhimu kwa wananchi wa nyikani wenye elimu za Upe, ni vema wajumbe walioenda kupumzika, wakatumiwa fedha zao zilizobaki huko huko waliko, kuliko kuwarejesha tena Dodoma kujadili misimamo ya vyama vyao.

Kuna shule za Msingi vijijini, madarasa ya shule hayaeleweki lipi ni dirisha na upi ni mlango.

Upande ambapo inatokea mvua, ndo kabisa, dirisha halieleweki lina pembe ngapi!

Sakafu ndani ya madarasa kunaonekana kuwa kulikuwa na saruji, lakini kwa sasa ni vumbi.

Wanafunzi wamefagia saruji yote. Yamebaki mahandaki.

Wanafunzi kila asubuhi wanaende na ndoo shuleni, siyo kwa ajili ya kuchotea maji. Bali ni kwa ajili ya kukalia.

Madawati hakuna! nguzo za umeme hakuna! Misitu imeisha na inaendelea kuisha!  

Walimu wapo wachache vijijini, ukiwasikiliza, wanasema baadhi ya wenzao walinunua vyeti vya ndoa na kuhamishiwa mjini.

Lakini hakuna hata mmoja ambaye anahamia Kijijini kutoka mjini, ukiona anahamishiwa huko basi ni yule anayeanza kazi, naye ukifika muda fulani anaomba ruhusu ya kwenda kusoma. Hiyo ndiyo tiketi ya kuondoka huko.

Wanasema kwenda kuchukua mishahara na kubandika matangazo wilayani ya kubadilishana vituo ili wao wahamie mjini, wanachanga nauli na kumpa mmoja wao, ili kwenda huko mjini!

Wanahamishia mishahara yao kutoka kwenye akaunti za benki na kuweka kwenye M-PESA.

Wakirudi kwenye vituo vyao vya kazi na matarajio kuwa watatoa pesa kwa wakala, naye anakuwa hawezi kuwasaidia kwasababu simu yake inakuwa imeisha chaji na hakuna umeme.

Haya ni baadhi ya mahangaiko ya wananachi na badhi ya watumishi wanaoishi vijijini.

Watu wengine wa nyikani, wanahangaika na suala la Mashine za EFD, ambazo zinawaumiza walaji na wafanyabiashara wa kati.

Yote hayo yalinyamazishwa na suala la Katiba Mpya, macho yalikuwa ni suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kutupiana maneno makali ili tu waonekane na kusikika na wanaodhani ni wapiga kura wao tarajali huku nyikani.

Asilimia 20 ya wajumbe wateule wana ndoto za kuwania nafasi za Ubunge mwaka 2015 baada ya kuona utamu wa Dodoma.

Watu wa nyikani wanasema hakuna anayeutaka kwa dhati Muungano uliopo kwa sasa, bali wanachohofia watawala ni kuhukumiwa na historia ya Muungano kuvunjikia mikononi mwao.

Muungano huu na Bunge la Katiba, ni kamali inayokula upande mmoja. Upande huo ni kodi za wananchi.

Mimi kama kiongozi wa wananyika, naona kuna haja sasa ya kuuvunja muungano, watu  wanataka misaada kutoka uarabuni.

Kuna fix za kifikra ambazo zina ugonjwa wa kufisha, kuwa Zanzibar ikijitenga na Tanganyika kutatokea Maendeleo ya ghafla na Amani ya kweli.

Ikumbukwe kuwa Ibrahimu haraka zake zinasumbua kule Israel mpaka leo.

Haraka zina hasara zake, sawa na utunzaji wa mtoto njiti na haraka hizi zinaweza kutufikisha mahala pa kupata Katiba njiti.

Naiona sinema ya Bunge la Katiba kama ile ya Richmond mwaka 2008.

Kwa kuwa Watanzania tuna tabia ya kudandia matukio na michezo ya wakubwa, sinema hii kuna siku yatatimia haya ninayoyasema leo kutoka hapa nyikani.

Kuna siku inanikumbusha mbali, nilipotoka huku nyikani na kuelekea mjini.

Nilipofika sehemu nikakuta msiba. Nikasimama. Nikasalimu waombolezaji.

Niliposema nataka kutoa mchango wangu, waliniambia shida kubwa katika msiba ule ni Sanda, Jeneza na gari la kubeba jeneza hilo.

Kabla ya kwenda kununua Jeneza na Sanda, nikawaambia wanipe mtu wa kuambatana nae. Wakanipa mvulana mmoja.

Wakati wa kurudi kwa ajili ya mazishi, yule mvulana akawa amekaa juu ya jeneza nyuma ya gari. Mvua ikaanza kunyesha.

Yule mvulana alipojisikia baridi akaamua kuingia kwenye jeneza ili apate angalau joto.

Mbele kidogo kuna watu wakadandia, ingawa hawakujua gari lilibebeba nini na lilikuwa likielekea wapi.

Baada ya hapo, mvua ikakatika. Yule mvulana kwenye jeneza akaanza kujisikia joto.

Akajitikisa. Wale waliodandia gari wakatazamana na kusemezana kuwa, hakuna kitu kibaya kama kutosindikiza maiti!

Walionesha kuumia na kumhurumia marehemu aliyekuwa ndani ya jeneza! Baadae kidogo yule mtoto akapiga chafya!

Wakasemezana kuwa marehemu aliwekwa kwenye jeneza hilo kabla hajafa vizuri!

Baadae joto lilipozidi, yule mvulana akafunua kidogo mfuniko wa jeneza na kunyosha kiganja, wakasema kwa mshangao kuwa Marehemu sasa anawaaga, huku wakizidi kujawa na woga!

Mfano huo ni kuonya kuwa hakuna jambo baya kudandia gari ambalo hujui linakoenda.

Tumedandia suala la Katiba Mpya, limekuwa gumzo mitaani kila kona na tumesahau kero zinazotusumbhua kuliko Muugano.

Katika ibara ya 26(1) ya Katiba ya nchi yetu, inamlazimisha kila mmoja wetu kuitii Katiba ya nchi na sheria.

Mlinzi mkuu wa Katiba na Sheria wa nchi yeyote duniani yaani pamoja na nchi yetu ni Mahakama. Ambayo kuanzia Tume ya maoni mpaka Bunge la Katiba vimeipuuza!

Inapuuzwa kwasababu, kuna kesi ya kihistoria Mahakama kuu ya Zanzibar, iliyofunguliwa na Wazanzibari wanaotaka muungano wa nchi yao na Tanganyika uvunjwe.

Maadili ya utawala wa kidemokrasia wa Katiba na Sheria yanatulazimisha kungoja uamuzi wa Makahama ndipo masuala mengine yaendelee.

Kupuuza msingi huu hakuwezi kutupatia Katiba halali. Pia sidhani kama Muungano ndiyo unasababisha tukose madawati katika shule zetu na elimu bora,  tupiganie yanayotukera zaidi ya Muungano.

Kuendelea kushambuliana kuhusu Katiba mpya ni kuwapa nafasi watawala kupumua na kuacha kutimiza wajibu wao kwa yanayotukera huku nyikani, hili ni gari lililobeba maiti iliyo hai.

No comments: