Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Sunday, April 06, 2014

SAUTI KUTOKA NYIKANI;.....MWAKABWANGA NA MDINDILE, KAWAULIZENI AKINA LOWASSA

Kulia ni Kamanda wa UVCCM wilaya ya Mbaralk mkoani Mbeya, akiwa na Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, ndugu Kizigo.

NA GORDON KALULUNGA

APRIL 4, mwaka huu. Limefanyika tukio la historia katika kata ya Utengule Usangu, wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.

Hapa ni eneo ilipo Ngome ya chifu Merere.

Kwa waliosoma miaka ya nyuma kidogo, nchi yetu ilipokuwa ikithamini kwa vitendo masuala ya kihistoria na ushujaa wa watemi wetu, wanalikumbuka jina la chifu huyu wa kabila la Wasangu.

Siyo nia yangu leo kueleza historia ya Merere, bali kuelezea suala la kihistoria lililofanyika mita mia moja kutoka eneo la Ngome hiyo.

Kaimu katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mmapinduzi(UVCCM), Taifa, Mfaume Kizigo, alifika eneo hilo na kusimikwa pia kuwa mmoja wa watemi wa kabila la wasangu.

Baadaye, Kizigo, alimsimika kamanda wa Vijana wa UVCCM wa wilaya hiyo, Ibrahimu Ismail(Mwakabwanga), ambaye pia alimsimika naibu wake Leonatus Mdindile.

Kizigo anasema kuwa, kwa wanaokumbuka historia, ni kwamba zamani watu walikuwa wakitembea uchi, lakini hakukuwa na kesi za ubakaji.

Lakini hii leo kuna kesi za namna hiyo kutokana na kuporomoka kwa maadili kunakochagizwa na kuwadharau wazee wakiwemo machifu.

Jamii imeendelea kulalamikia suala zima la uharibifu wa mazingia na ukataji miti kwa ujumla wake na kusahau kuwa, zamani jamii ilipokuwa ikiheshimu wazee ndipo ilikuwa salama, kwasababu machifu walikuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa kukuza mila na desturi na utunzaji wa mazingira.

Baada ya kuapishwa, Ibrahimu Ismail, maarufu kwa jina la kibiashara(Mwakabwanga), ambaye pia ni Mkurugenzi wa kampuni ya Usangu Logistics Ltd, anashukuru vikao vya uteuzi vya vijana kwa madai kuwa yeye siyo mzigo.

Ukimwangalia machoni, unatambua kuwa Mwakabwanga, anajua fika, majukumu yake kama kamanda wa Vijana kwa mujibu wa miongozo ya kanuni za UVCCM kuwa ni kuwaunganisha vijana na shughuli zao za kiuchumi.

Siku hiyo hiyo, alianza kuihudumia jamii kwa kukikabidhi Chama Cha Mapinduzi (CCM), Gari la wagonjwa na Jokofu la kuhifadhia maiti na kwamba haombei watu kufa bali anataka hata watakaotangulia, wawe na mwisho mwema na wa heshima.

Gari na Jokofu anasema vina thamani ya Milioni 35 na zaidi, huku akiweka wazi kuwa ataendelea kuzungumza na marafiki zake kuikomboa jamii ya wananyika wa Mbarali kwa kuwapelekea mahitaji wanayoomba bila kujali itikadi za siasa.

Katibu wa CCM wilayani humo, Mr. Luambano, baada ya kukabidhiwa, naye akakabidhi serikalini. Anamshukuru kamanda huyo na kumsihi azidi kuwasaidia wananchi kwa ujumla.

Mkuu wa wilaya hiyo, Gulam Kiffu, anasema msaada wa gari la wagonjwa na Jokofu ni msaada mkubwa kwasababu kabla ya msaada huo walikuwa wakipeleka maiti kuhifadhi Ilembula mkoani Njombe au katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya zaidi ya kilomita 80.

Katibu wa UVCCM wilayani humo, Sure Mwasanguti na Mwenyekiti wake Amin Kimulungu, wanampa moyo kamanda wao na kwamba wanajua fika kuwa utendaji kazi wake wa kuhudumia jamii unaweza kuwa tatizo kwa baadhi ya wasaka madaraka. Hivyo asikate tamaa.

Vijana wanaruhusu magugu na ngano vikue pamoja kisha jamii itaamua wakati wa mavuno wakati CCM Taifa, sidhani kama ina maono kama jamii inavyohitaji.

Binafsi, niliwashangaa waliompigia makofi. Vigelele. Vifijo. Nderemo na shangwe kamanda huyo, kutokana na kujibu maombi yao hasa ya gari la wagonjwa.

Kilichonishangaza ni kwamba sijui kwanini wananchi hawataki kuamini kuwa CCM haiwataki watu wa namna ya Ibrahimu na Mdindile kwenye jamii, mpaka wao wanaamua kumuomba kisha akiwatekelezea mahitaji yao wanapiga vigelegele!

Niliwasikia baadhi ya wananchi wakieleza na shida zao zingine kwa njia ya mdomo, wakisema eti mkandarasi aliyejenga barabara inayounganisha eneo hilo la Utengule Usangu na Igurusi, achukuliwe hatua!

Yaani wananchi wanajifanya eti hawajui kabisa kitu kinachoitwa Ten percent kwa wakuu wa idara na idara za manunuzi!

Ameshindwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa mapesa yote ya Halmashauri nchini, Hawa Ghasia na John Pombe Magufuli, Kamanda wa UVCCM atafanya nini na wakati hayo pia siyo majukumu yake?

Namuonea huruma sana Ibrahimu Ismail (Mwakabwanga) na Mdindile kwa kujitoa kwao kuhudumia jamii ya wana Mbarali.

Masikitiko yangu ni kwamba sijui kwanini walikubali uteuzi wa nafasi hiyo, kwasababu namfahamu Ibrahimu na marafiki zake wanavyojitolea hata kuchimba visima Jijini Dar es Salaam na kuwaona wagonjwa.

Ningekuwa mimi kabla sijakubali, ningeenda kuomba ushauri kwa mzee wa uvumilivu na maamuzi magumu yaani Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa na kumuuliza athari za kuwahudumia wahitaji walioko nyikani, ukiwa kiongozi wa CCM kwa sasa.

Lakini kwasababu amekubali kuwa mlezi wa vijana na kuwainua kiuchumi, atarajie mambo matatu makuu yafuatayo;

Mosi, atarajie kuwa wana CCM wenzake, watapeleka mashitaka kwenye ngazi za maamuzi kuwa anapiga kampeni za Ubunge kwa ajili yake ama kwa ajili ya mtu wa karibu yake, Mbarali au Kawe na Ilala Jijini Dar es Salaam.

Pili, kwasababu kundi kubwa ni vijana ambao wengi wao wameamua na baadhi wanataka kujikita kwenye biashara ya bodaboda, akithubutu kuwainua kiuchumi kupitia njia hiyo ama njia nyingine kwa kiwango kikubwa, atapigwa marufuku haraka, kwasababu sidhani kama CCM inapenda jamii ijitegemee kiuchumi kupitia wadau.

Chama kinalazimisha watu wakakope, na hata wakienda kukopa, hawapati mafunzo ya urejeshaji wa fedha, nyumba zao zinauzwa na wanaokopa ni maafisa ama ndugu zao na mfano mzuri ni fedha zilizoitwa za JK. Ziko wapi?

Tatu, licha ya Mkuu wa wilaya ya Mbarali, kushukuru kwa niaba ya serikali na kumuomba Kamanda huyo aendelee kuzungumza na marafiki zake na familia ili kupeleka misaada ya kijamii wilayani humo, nauona ugeugeu wa wanasiasa ndani na nje ya CCM.

Ninaamini kuwa watu wataibuka na kusema kuwa kupelekewa Jokofu wilayani humo ni sawa na kuchuliwa kifo, bila kujali uhalisia wa mahitaji halisi ya jokofu hilo na kuondokana na adha ya kumzika mtu kila baada ya saa tano au sita baada ya kufariki kutokana na kutokuwa na Jokofu.

Ninachokijua ni kwamba ukweli wa polisi siyo uwongo wa raia na uwongo wa raia siyo ukweli wa polisi, ndiyo maana nasema wanaojitolea kuhudumia jamii, wakawaulize akina Lowassa.

Mwandishi wa makala anapatikana kwa simu 0754 440749
BARUA PEPE; kalulunga2006@gmail.com

No comments: