Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Monday, October 27, 2014

SAUTI KUTOKA NYIKANI....NWAKA MWAKISU(GOVERNMENT), MJASILIAMALI ANAYETAJWA KUMRITHI SUGU MBEYA MJINI


 Mjumbe wa mkutano mkuu wa Taifa CCM na UVCCM, Nwaka Mwakisu.

NA GORDON KALULUNGA

 WIKI iliyopita tuliona wasifu na mtazamo wa Kamanda wa Vijana wa CCM(UVCCM), kata ya Sinde Jijini Mbeya, Eliurd Mwaiteleke, ambaye ni mtumishi wa ofisi ya Waziri Mkuu(TAMISEMI), anayetajwa kuwa ni mmoja wa wanaohitaji kupeperusha bendera ya CCM katika Jimbo la Mbeya Mjini. Jimbo hilo linaloongozwa na Joseph Mbilinyi(Sugu), (Chadema), linatazamwa kwa jicho la uangalifu na Chama Cha Mapinduzi, kilichoshindwa uchaguzi chini ya Benson Mpesya, ambaye kwa sasa ni Mkuu wa wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga.

 Kwa tathimini ya kisiasa, CCM, ilitakiwa iwe imeondoka madarakani 2010, kutokana na majiji kadhaa kushikiliwa na vyama vya upinzani hususani, Chadema. Mfano Jiji la Mbeya, Mwanza katika Manispaa za Nyamagana na Ilemela, Arusha hali kadhalika Dar es Salaam katika majimbo ya Kawe na Ubungo. 

Vijana kadhaa wanaonekana kuwa na nia na wanatajwa kutafuta uongozi wa nafasi za Ubunge katika majimbo mengi, ambapo kwa mkoa wa Mbeya, Jimbo la Mbeya mjini, licha ya Mwaiteleke, anatajwa pia kijana Nwaka Mwakisu,(Government), na Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Mbeya, Amani Kajuna, jina lake limeanza kusadifu.

 Leo hii tumtazame Nwaka Mwakisu, mwanafunzi wa chuo cha kodi jijini Dar es Salaam, (DCTM), Diploma custom Tax Managiment, ambaye alizaliwa April, 1982, eneo la Nzovwe Jijini Mbeya na kusoma shule ya Msingi Lwangwa wilayani Rungwe katika jimbo la Busokelo, chini ya Bibi yake, tangu mwaka 1992-1998.

 Sauti ya Nyikani, ilifanya mahojiano na kijana huyu ambaye ni mjasiliamali na mwajiriwa wa kampuni ya Lake Oil na nafasi yake katika chma ni mjumbe wa Mkutano mkuu wa CCM na UVCCM Taifa.

 Anasema mwaka 1999-2002, alijiunga na sekondari ya Mano Junior Seminary kidato cha kwanza na cha Nne, kisha mwaka 2003 aliendelea na masomo yake katika shule hiyo huku akikulia katika jamii ya maadili ya dini zaidi kisha akahama na kujiunga na sekondari ya wazazi Meta Jijini Mbeya mpaka mwaka 2005. 

 “Nikiwa Mano Seminary, nikakutana na rafiki yangu Christopher Luagile ambaye tulikuwa naye katika mchepuo wa HGE, na tulipokuwa shuleni hapo tukapachikwa jina la Government kutokana na nafasi zetu za uongozi shuleni” anasema Mwakisu.

 Anaeleza kuwa watu wengi wanadhani yeye ameanza siasa miaka ya hivi karibuni, jambo ambalo siyo kweli kwasababu hawafahamu historia yake, bali anadai kuwa, alianza siasa mikononi mwa Prof. Mark Mwandosya katika jimbo la Rungwe Mashariki miaka ya 1998 ambapo yeye na vijana wengine walikuwa na vikundi vya CCM na kufanya kazi za kujitolea. 

Alipohitimu kidato cha sita, alijiingiza katika shughuli za uwakala wa forodha(Clearing and Fowarding), chini ya Aden Mwakyonde na Kivaula Luhanga, mjini Tunduma mkoani Mbeya, ambao walimfundisha ukokotoaji wa hesabu za kodi za kopa na mafuta yanayosafirishwa kimataifa.

 Yeye akaamua kubobea katika ukokotoaji wa kodi za mafuta kisha akaajiliwa na kampuni ya Tanganyika Investment Oil and Transpot (TIOT), akiwa msimamizi mkuu wa kodi zote za forodha za kimataifa huku akiwa na mkataba wa kampuni ya Prime Fuel kwa ajili ya kusimamia kodi za mipaka ya Tundma, Kasumulu na Rusumu.

 Anasema mwaka 2005 alishiriki kusaidia kampeni za Rais Jakaya Kikwete akiwa anaelekea Sumbawanga akitokea mkoani Mbeya na mwaka 2008 akajinga na wenzake wawili na kuanzisha mgodi wilayani Mbarali mkoani Mbeya kabla hawajafukuzwa na aliyekuwa Mkuu wa wilaya kwa wakati, marehemu, Hawa Ngulume akidai kuwa ofisi yake haikuwa na taarifa na uwekezaji wao.

 Mwaka 2009 akahitajika tena na kampuni ya Oil Com, kisha mwaka 2012, badala ya kuwa mwezeshaji wa chama pekee, akagombea nafasi ya ujumbe wa Mkutano mkuu wa CCM na akashinda.

 Mwakisu, anasema naye licha ya kusikia kuwa anatajwa kuwa mmoja wa watakaochukua fomu na kugombea nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Mbeya Mjini kupitia CCM, bado hajasema jambo lolote na kwamba kama wakati utafika atasema.

 Lakini anasema kuwa wapiga kura wa sasa siyo wa kudanganywa, wanapenda kuchagua kiogozi anayetokana na wao na anayefahamu mambo yao.

 Kuhusu uchumi, anasema jimbo la Mbeya mjini linapaswa kuongozwa na mtu ambaye anazijua fursa za kibiashara ndani na nje ya nchi ambazo baadhi yeye anazifahamu vema.

 Anasikitika kuwa vijana wa Jiji na mkoa mzima wa Mbeya hasa wazawa wananyang’anywa fursa nyingi zikiwemo ajira na nafasi za uongozi. 

“Hawana soko la uhakika na soko Jipya la Mwanjelwa pia hawana uhakika wa kuingia katika vyumba vilivyopo na hawajapata mtu wa kuwasemea” anasema Mwakisu. 

Wakati Mkoani Morogoro kuna kiwanda cha Tumbaku licha ya kwamba mkoani hapo hailimwi tumbaku, anasikitishwa serikali kuua viwanda kutokana na baadhi ya wasomi wasio wazawa na uzalendo na Mbeya kuchukua maamuzi anayoyaita ya ajabu na kwamba kuua viwanda Mbeya ni kuwaondolea fursa vijana na kuua uchumi wa mkoa kwa ujumla. 

 “Kiwanda cha nyuzi za pamba pale Songwe (Mbeya tax) kilikufa baada ya wataalam kusema kuwa pamba iliyokuwa inalimwa wilayani Chunya haifai kutokana na kuingiliwa na mdudu, sasa najiuliza, mdudu akiingia kwenye mahindi watawaambia wananchi waache kulima mahindi?” anahoji Mwakisu na kwamba lazima viongozi waliopo na wajao watafakari upya kuhusu Mbeya. 

 Kuhusu maji, anasema licha ya Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Jijini Mbeya kujinasibu kuwa maji yapo ya kutosha, lakini siyo kweli na kwamba yeye mpaka leo anashindwa kuelewa nani ananufaika na mradi mkubwa wa maji uliozinduliwa na Rais Kikwete, uliopo Nzovwe, Jijini hapo. 

Anasema kutokana na kusoma Seminari, anajivunia kuishi na wananchi wenzake vizuri na kushirikiana nao kuimarisha amani Jijini Mbeya na kuwa mlezi wa vikundi vya bodaboda na bajaji.

“Ninayoyafanya hayalengi kugombea ubunge, bali ninasaidiana na jamii ninayoishi nayo, na kama kuna mtu anafikiri nayafanya haya kwa ajili ya mtazamo wa kugombea Ubunge Jimbo la Mbeya Mjini, basi naye afanye ili jamii yetu iwe imara kimaendeleo” anasema 

Nwaka Mwakisu. Huyu ndiye Nwaka Edson Mwakisu, namtakia kila lakheri katika mambo yake ya kijamii na siasa, wiki ijayo tutamfahamu Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Mbeya, Amani Kajuna, na safari yake ya maendeleo ya jamii na siasa. 

Mwandishi anapatikana kwa simu 0754 440749
EMAIL; kalulunga2006@gmail.com

No comments: