Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Saturday, November 29, 2014

ATHALI ZA KUJIFUNGULIA KWA MKUNGA WA JADI, MWANAMKE MMOJA APATA UGUMBA ZANZIBAR!

NA KHADIJA KOMBO, PEMBA

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesogeza vituo vya afya kwa wananchi, tofauti na awali, huduma za afya zilikuwa zikipatikana maeneo  machache.

Maeneo ambayo zamani kulikuwa kuipatikana huduma za afya kulikuwa ni Chake Chake, Mkoani, Wete Micheweni na Vitongoji kwa Pemba, lakini sasa vimefunguliwa  vituo vingi ili kupunguza masafa ya kupata huduma za afya.

Lakini bado kuna tatizo la elimu kwa baadhi ya wananchi, wakiwemo wajawazito, ambao kwa mazoea wanaenda kujifungulia kwa wakunga wa jadi na kuhatarisha maisha yao.

“Bado kidogo nipoteze maisha kutokana na kujifungulia nyumbani, hata hivyo nimepata matatizo makubwa, kwani sijaweza  tena  kubeba ujauzito” anasema Bi Riziki Abdallah(42),mkazi  wa Mkanyageni Mkoani Pemba.

Anaeleza kwamba, alipojifungua mimba yake ya  tano  akiwa na miaka  (30), aliamua kujifungua nyumbani  kutokana na uzoefu kwamba ameshazoea kujifungua, lakini kwa bahati mbaya Mtoto alitoka vibaya na kumsababishia matatizo makubwa.

Akionekana mwenye huzuni baada ya kukumbuka mateso aliyoyapata, anasema alikuwa kwa mkunga wa jadi, mtoto alitangulia kutoka  makalio,akakwama sehemu ya kichwa na mkono, mkunga wa jadi hakuwa na namna ya kuweza kumsaidia ndipo ilipoamuliwa kupelekwa Hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani, akiwa amechanika sana.

“Niliponea chupu chupu, nilipoteza damu nyingi, nikapoteza fahamu na mguu wangu wa kushoto ukafa ganzi kwa miezi miwili sikuweza kusimama”  anaeleza.

“Nawasihi sana wenzangu wasifanye mchezo na kujifungua, hasa nyumbani, wakimbilie Hospitali, kwani kule kuna wengi na kwenye wengi pana mengi lolote litakalo tokea unaweza kusaidiwa kwa  haraka. ”anasisitiza Riziki.


Kwa upande wake, Sauda Salim (49) mkazi wa Chake Chake, anasema, anaeleza jinsi mkwewe alivyopata tabu kwa mkunga wa jadi.


Anasema mtoto alitoka vibaya.Mkunga hakuwa na uwezo tena wa kumsaidia. Eneo la mkunga hakukuwa na usafiri wala mawasiliano ya simu, hatimaye mtoto alipoteza maisha na mama akawa taabani, hajiwezi baada ya kupoteza damu nyingi.


Munira Bakar (40) Mkaazi wa Wete, anatoa ushuhuda kwa aliyoyaona kwa jirani yake, kwamba alihangaika tokea majira ya saa mbili asubuhi, hadi saa nne asubuhi, ambapo bado  zalio halikutoka, huku akipoteza damu nyingi, ndipo walipoamua kumpeleka Hospitali  ya Wete, akiwa na hali mbaya.

“Mtu akisha jiona kashazaa  mimba tatu, nne hujiona mzoefu  hukataa kujifungulia  Hospitali, hubahatisha kwa kujifungua nyumbani jambo ambalo ni hatari”anasema, Munira.


Afisa  wa kitengo Shirikishi,  juu ya afya ya mama na mtoto, ambaye pia ni,Afisa mfuatiliaji wa Chanjo Zanzibar, Abdulhamid Ameir Saleh, anasema tatizo kubwa linalosababisha kuongezeka kwa vifo vya  akina mama wakati wa kujifungua, ni kutokujifungulia Hosptali.


“Tulifikiria kwamba moja kati ya changamoto ni kufuata huduma masafa marefu, lakini pia tumegundua kuwa suala la elimu duni juu ya hilo linachangia”alisema afisa huyo.


Muhudumu wa mama na watoto, ambaye ana uzoefu wa kutoa huduma hizo kwa zaidi ya miaka ishirini sasa katika Hospitali ya Abdalla Mzee, Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba, Bi Zuhura Mussa,  anasema  tatizo kubwa linalo gharimu maisha ya akina mama na watoto wakati wa kujifungua ni kucheleweshwa kufikishwa Hospitali.


“Mama anapokuja Hospita huwa hali imesha kuwa mbaya  pamoja na juhudi utakazochukua basi utakuta unampoteza mama  au mtoto na mara nyingine wote wawili “anasema,  Zuhura .

analeza kwamba, katika kipindi cha mwaka  2013, akina mama 197  walifanyiwa  upasuaji, kama huduma ya dharua ili kuokoa maisha yao na watoto, lakini hata hivyo akina mama 5, walipoteza maisha.

Amina Ali Mbarouk,ambaye pia ni Muhudumu wa Mama na Watoto katika Hospitali hiyo ya Abdalla Mzee, anasema bado elimu juu ya umuhimu wa kujifungulia Hospitali  ni ndogo kwa wananchi hasa vijijini, ambako ndiko kwenye tatizo kubwa la kuwategemea wakunga wa jadi.


“Matatizo kama kukwama kwa zalio,kuchanika Msamba, yote haya husababisha mama kutokwa na Damu nyingi,  Mkunga wa jadi hawezi kumsaidia ”anasema, Amina.

Daktari dhamana Hospital ya Chake Chake  Kisiwani  Pemba,  Dr. Yussuf  Hamad  Iddi,  anasema  katika kipindi cha mwaka 2013, zaidi  ya akina mama 12, walipoteza maisha wakati wa kujifungua.


“Mara nyingi mama hutokwa na damu nyingi kabla au baada  ya kujifungua, kifafa cha mimba au mtoto kulala vibaya, matatizo ambayo Mkunga wa jadi hawezi kuyashughulikia”anasema, Dr Yussuf.

 Kuhusu suala la kauli mbaya kutoka kwa wauguzi dhidi ya wajawazito kama chanzo cha wanawake wengi kuimbia kujifungulia hospitalini, Khadija Said Hemed ,Muhudumu wa mama na Watoto katika Kituo cha afya Kojani, anasema kauli hizo zinakuja pale pasipokuwa na  budi, lakini ni katika  hali  ya  kumuokoa  mama  na  mtoto  wake, kwani lolote litakalo tokea, muuguzi ndiye wa kwanza   kujibu.


Anaendelea kufahamisha kuwa, wauguzi hulazimika kuwa wakali, kwani kuna wajawazito huwa wakaidi, wakati  mtoto anataka kutoka, yeye hujibana hadi anasababisha hatari kwa mtoto.


“Lazima utamkaripia kwani lolote litakalo tokea pale wewe ndie wa kujibu”anasema, Khadija.

Anasema tatizo la wajawazito kujifungulia majumbani ni kubwa hasa Vijijini, kwani akina mama wengi bado wanawaamini wakunga wa jadi.

“Kwa sasa Wakunga wa jadi, ni changamoto, kwani bado wana jiamini bila ya kuwa na hofu kwa matatizo yanayo weza kujitokeza kwa mama wakati wa kujifungua.Idadi ya akina mama  Kituoni hapa ni nusu kwa nusu wanao jifungua Hospitali na wanao jifungua Nyumbani’’ anasema Khadija.

Mratibu wa Afya ya mama na mtoto kanda ya Pemba, Sharifa Humood Rashid, anasema wakunga wa jadi wajitahidi sana wasizalishe nyumbani, kutokana na  matatizo mengi yanayoweza kujitokeza kutoweza kukabiliana nayo.

“Mara nyingi Mkunga wa jadi humleta mama Hospitali akiwa yuko hoi kiasi ya kufia pale Hospital tu “anaeleza Sharifa.

Anasisitiza kwamba akina mama wasiwe na fikira potofu  kwamba watakapo kwenda Hospital watapata  kauli mbaya, bali wanapohisi mabadiliko katika miili yao, basi wakimbilie Hospitali.

Anasema, Serikali imeamua kuwasogezea karibu huduma hiyo, kwa kuongeza vituo mbali mbali, kama vile Pujini, Bogoa, Kojani ,Wesha,na vingi vyenginevyo Kisiwani Pemba, kwa sasa Zanzibar ina Mtandao Mzuri wa Vituo vya Afya, ambao mwananchi hawezi kutembea zaidi ya kilomita 5 bila ya kukuta kituo cha afya.


“Ingawaje hali sasa sio kama zamani  baadhi ya Hospitali tuna bingwa mmoja au wawili ,lakini katika Hospitali nyingine hakuna kabisa hii bado ni changamoto Madaktari  hawatoshi”alisema, Mratibu huyo.

Ukweli huu unathibitika pia kutoka katika Hotuba ya Waziri wa Afya Zanzibar Juma Duni Haji ,aliyowasilisha katika baraza la wawakilishi Zanzibar  mwaka 2013/2014 ,kuwa Wizara imefanikiwa kusomesha wafanyakazi wake, ambapo jumla ya wafanyakazi 142 wamepelekwa masomoni kati yao wamo madaktari 7 wanaosomea fani mbali mbali za udaktari bingwa.

Waziri  huyo  anasema  kuhusu makadirio na matumizi ya wizara ya afya kwa mwaka wa fedha 2014/15,   kuwa miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ,ni kuongezeka kwa kinamama wanaojifungulia katika vituo vya Afya na Hospitali kutoka asilimia 49.4 mwaka 2012 hadi asilimia 56.6 mwaka 2013.


“Kutokana na Takwimu hizo ni dhahiri kuwa asilimia 43.4 bado wanajifungulia nyumbani wakihudumiwa na wakunga wa jadi, jambo ambalo linaweza kuchangia ongezeko la vifo vya akinamama na watoto wakati wa kujifungua” anasema.


Aidha  Waziri anakiri kuwa Idadi ya vifo vya uzazi vilivyotokea   katika  hospitali  za  Zanzibar kwa mwaka 2013 ni 103 (Unguja 68, Pemba 35) ambavyo ni ongezeko la vifo 37 ukilinganisha na mwaka 2012.


“Pamoja na  jitihada  zinazofanywa na Serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar ,kwa muda mrefu kutatua tatizo la vifo vya akina mama, vitokanavyo na uzazi  (maternal mortality), takwimu za karibuni zinaonyesha kuwa hali siyo nzuri ,kwani vifo vya akina mama vinaendelea kuongezeka kila mwaka,  Huku ikisalia  miezi  mitano  tu ,kufikia mwaka 2015,mwaka ambao malengo ya maendeleo ya millennia (MDGs) yamepangwa kufikiwa” inasomeka moja ya haya ya hutuba ya Waziri.

No comments: