Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Saturday, November 29, 2014

MJAMZITO AFIA ''JUU'' YA BODA BODA AKIENDA KUIFUNGUA

File:Three persons on boda-boda.JPGPicha hii haihusiani na tukio husika.

NA ZAKIYA KATAKWEBA, MTWARA

TATIZO la vituo vya afya na hospitali kuwa mbali na jamii, limepelekea wajawazito na vichanga kupoteza maisha mkoani Mtwara.

Ushahidi wa hali hiyo, umeacha historia mbaya kwa wananchi wa kijiji cha Mnima, Kata ya Mnima, wilaya ya Mtwara Vijijini.

Mjamzito Mariam Chibwana pamoja na kichanga chake, hivi karibuni walipoteza maisha akiwa anapelekwa hospitali ya mkoa wa Mtwara, iliyopo umbali wa kilomita 70, kwa ajili ya kujifungua.

Mumewe aitwaye Rashid Mkapa, anasema kabla  mkewe hajafariki, alipewa rufaa ya kutoka Zahanati ya Mnama, kwenda hospitali ya mkoa wa Mtwara, kwasababu alitakiwa ajifungue kwa njia ya upasuaji.

Anasema kutokana na kuchelewa kwa gari la kubebea wagonjwa, ambalo walikua wakilisubiri kutoka katika kituo cha afya Kitere kilichopo umbali wa zaidi ya km 30 mpaka zahanati ya Mnima, aliamua kukodi bodaboda kwa Tsh.35,000/= na kuanza safari kuelekea katika hospitali ya mkoa.

“Iliniuma sana kumuona mke wangu anapoteza maisha huku nikiwa nashuhudia kwa macho yangu, kwa kweli ni tukio ambalo siwezi kulisahau katika maisha yangu”….

“Mpaka sasa ni miezi sita imepita lakini wakati mwingine huwa picha ya lile tukio inanijia na kujikuta nakosa amani hata kama nipo katika shughuli zangu” Alisema Mkapa, nakuongeza kuwa kila akimwangalia mwanaye wa kwanza mwenye miaka miwili, anamkumbuka marehemu mkewe.

Anasema mkewe kabla hajakata roho, alianza kuhangaika juu ya pikipiki, akaomba pikipiki isimame, kisha wakamteremsha, kwa kuwa hawakuwa na utaalamu wowote na hawakuwa na muuguzi, walishindwa kumsaidia na hatimaye alipoteza maisha pamoja na kichanga chake.

“Nakumbuka wakati tunampakia kwenye pikipiki ili tuanze safari aliniambia mume wangu sitoweza kwenda hata msijisumbue mtajipa tabu bure na kupoteza pesa bila sababu, mimi ni wa kufa tu” Anasema kwa hisia, mgane huyu.

Anasema kutokana na hali aliyokuwa nayo marehemu mke wake kama wangepata msaidizi pamoja na usafiri wa gari la wagonjwa wangeweza kuokoa maisha ya mkewe na kichanga chake.

Mkunga katika zahanati hiyo, Saada Mpaji, anasema endapo marehemu, Mariam angewahi kufikishwa katika zahanati hiyo, wangeweza kutambua dalili za uchungu pingamizi aliokuwa nao, lakini alichelewa.

Anasema hakuweza kumsindikiza katika pikipiki hiyo kwasababu katika zahanati yao wapo wahudumu wawili tu, na siku hiyo mwenzake hakuwepo, hivyo yeye hakuwa na jinsi, alibaki kuhudumia wagonjwa wengine.

Aliitaja changamoto nyingine kuwa ni wajawazito wengi katika eneo hilo kutohudhuria kliniki wakati wa ujauzito na kungojea mpaka siku wanayokaribia kujifungua.

Anasema kuwepo kwa huduma za dharura ikiwemo gari la kubebea wagonjwa litakalopatikana kwa wakati pindi linapohitajika katika zahanati na vituo vya afya, kutasaidia kuokoa maisha ya mama na mtoto kwa kuwa katika kijiji hicho wakina mama wengi licha ya wengine kuwa wanahudhuria kliniki, lakini wamepoteza vichanga vyao kwa sababu ya kutopatikana kwa wakati kwa huduma ya gari hilo.
“Hivi unadhani mtu anawezaje kukaa kwenye pikipiki akiwa katika hali ya uchungu wakati hata mtu asiyekuwa na tatizo lolote tu hawezi kwa umbali wote huo sembuse mtu mwenye hali hiyo” Alisema.

Kadhia ifananayo na marehemu Mariam, ilimkumba pia,  Zainabu Chipele, mkazi wa Kijiji cha Mtulihinju, sehemu ambako kuna miinuko,  ambaye alibeba ujauzito akiwa na miaka 17, yeye alipoteza kichanga chake kutokana na kujifungulia nyumbani baada ya kukosa usafiri wa kumfikisha katika zahanati.

Huku akiwa hana kumbukumbu za kuwepo baadhi ya maeneo bajaji za wajawazito maarufu kwa jina la (Bajaji za Kikwete), ambazo maeneo mengi zimekataliwa na wajawazito, anasema kuna umuhimu wa kuwepo usafiri utakaowasaidia wajawazito kufika katika zahanati au vituo vya afya kwa wakati vinginevyo  wajawazito w maeneo hayo, wataendelea kuwa katika hatari ya kupoteza maisha.

Zainabu anakiri kuwepo kwa madhara ya kujifungulia nyumbani kwa kueleza kuwa alimpoteza mtoto wake kutokana na yeye kupata kifafa cha mimba, na kwamba ifo cha mtoto wake kisingetokea endapo angepata usafiri  salama wa kumfikisha Zahanati.

Naye Mkunga wa jadi katika kijiji hicho, Somoe Maywaywa, ambaye alipata mafunzo ya mwezi mmoja ya ukunga mwaka 2002 katika kata ya Mkunwa, iliyopo kwenye halmshauri hiyo na hivi sasa anatumika pia katika zahanati endapo kunakuwepo dharura ya kutokuwepo kwa mmoja wapo wa wahudumu wa afya, anasema bila ya kuwepo kwa usafiri wa gari kina mama wajawazito wataendelea kupoteza maisha.

Anaeleza kuwa, usafiri wa pikipiki au baiskeli siyo salama kwasababu mama anapokua amekalishwa kwenye usafiri huo, kama mtoto anakuwa amesogea anaminywa kichwa na kwa kuwa vichwa vyao vinakuwa laini (havijakomaa) hupoteza maisha.

Anatoa rai kwa serikali kuhakikisha zahanati hiyo iliyopo pembezoni, inapatiwa  gari, ili kupunguza vifo vya kinamama wajawazito na watoto, visivyo vya lazima.

Mwenyekiti wa kijiji hicho cha Mnima Selemani Nakuha,  anatoa wito kwa serikali kupitia wizara ya afya nchini, kuweka mazingira yatayohakikisha hakuna mama mjamzito au kichanga kinachopoteza maisha kutokana na tatizo la miundombinu.

Kwa upande wake mganga mkuu wa halmshauri ya Mtwara vijijini (DMO) Mohamed Mang’una, anawalamu wananchi kwa kutowafikisha kina mama wajawazito mapema katika zahanati au vituo vya afya na kusababisha kupoteza maisha  pamoja na vichanga vyao.

Anasema licha ya kuwepo changamoto ya magari ya kubebea wagonjwa kuchelewa kufika linapohitajika,kumpeleka mgonjwa katika hospitali ya mkoa ambayo ndiyo inayotumika kama hospitali ya wilaya kutokana na wilaya hiyo kutokuwa na hospitali, lakini endapo mama mjamzito angefikishwa zahanati mapema, wahudumu  wangeweza kuokoa maisha yao.

 “Unakuta watu wanamleta mama akiwa na hali mbaya baada ya kuona mkunga wa jadi ameshindwa kumsaidia, wanapotoka huko ndio wanakuja zahanati au kituo cha afya na gari la wagonjwa litoke umbali wa kilometa zaidi ya thelathini unategemea nini kama siyo mama kupoteza maisha?” Anasema mganga huyo.

“Katika halmashauri ya Mtwara vijijini tuna magari ya wagonjwa matatu, moja lipo kituo cha afya Kitere lingine lipo Mahurunga na Nanyamba na yanatoa huduma kikanda, magari hayo hayo utakuta yanafanya shughuli nyingine za kiserikali au wakati mwingine linalofanya kazi wilaya nzima ni moja, mengine yameharibika sasa mama asipowahi kufika unatoaje taarifa ghafla na gari liwe limefika?” Alihoji mganga huyo.

Anaitaja sababu nyingin inayochangia vifo hivyo katika wilaya yake kuwa ni pamoja na tatizo la wananchi kupenda kuwatumia wakunga wa jadi wakati wa kujifungua, jambo ambalo linaongeza hatari ya kupoteza maisha.
Anasema ili kukabiliana na changamoto ya umbali wa kufuata hospitali kwa wakimama wanaopewa rufaa halmashauri ya Mtwara vijijini inatekeleza mradi wa kupunguza vifo vya kina mama unaoitwa Three regions Study, ambao pia unatekelezwa katika mikoa ya Tabora na Kigoma.

Mradi huo unaziwezesha halmashauri za wilaya katika mikoa hiyo kujenga vyumba vya upasuaji kwa ajili ya kuwasadia wakina mama wajawazito wanaohitaji huduma ya upasuaji na katika halmashauri yake anasema tayari wamekwishajenga chumba hicho katika kituo cha afya Nanyamba ambacho si muda mrefu kitaanza kufanya kazi na pia wanatarajia kujenga katika kituo cha afya Mahurunga na Kitere.

Dk Mang’una anaeleza kuwa endapo vyumba hivyo vitakamilika katika vituo vyote hivyo na watoa huduma wataongezwa, vifo vya wakinamama au vichanga vinavyosababishwa kutokana na kukosa huduma ya upasuaji vitapungua kwa kiasi kikubwa.

Anawataka wananchi kuunga mkono jitihada za serikali za kuhakikisha tatizo la miundo mbinu linaondoka, na kwamba wanancho nao waache tabia ya kujifungulia nyumbani kwa kutumia wakunga wa jadi wasio na utaalamu na kuchelewa kufika katika sehemu za huduma ili kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.

Kwa mujibu wa ripoti ya takwimu za vifo vinavyotokana na uzazi katika halmashauri ya Mtwara vijijini iliyotolewa mwaka 2013 inaeleza kuwa jumla ya kina mama 32 kati ya laki moja (100,000) walipoteza maisha huku watoto 9 kati ya elfu moja (1000) walikufa kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo ya wakina mama wajawazito kuchelewa kufika katika zahanati au vituo vya afya.

No comments: