Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Monday, November 24, 2014

SAUTI KUTOKA NYIKANI....KIKWETE ANALAZIMISHA LOWASSA AWE RAIS


NA GORDON KALULUNGA.. 0754 440749

NCHINI India makabila madogo hayapati uongozi wa juu ya nchi, kutokana na kasumba tu, ya kwamba kama hujasoma shule fulani ambayo ni ya karo kubwa huwezi kushika madaraka.

Maana yake ni kwamba masikini wote kamwe hawataweza kushika madaraka katika nchi hiyo tofauti na hapa nchini Tanzania.

Mfano wa nchi ya India unashabihiana na jirani zetu wa Kenya, ambao kabila moja kubwa la wakikuyu, ndiyo wanazidi kuwa watawala na wamiliki wakuu wa ardhi ya nchi hiyo kwa asilimia 90, vivyo hivyo ni tofauti sana na hapa nchini Tanzania.

Kwa mfumo huo, mahala pengine wananchi wanaamua kuchagua mtu anayetokana miongozi mwao na hali kama hiyo imejitokeza katika taifa la Indonesia ambako wananchi wamempa fundi seremala kuwa rais.

Baada ya kuona hivyo, serikali ikakatalia fedha kwa ajili ya kuapishwa kwake, lakini wananchi wakiwemo wauza vibama, walichanga fedha kwa ajili ya sherehe.

Mwanzoni mwa wiki hii, nilipata simu ya rafiki yangu mmoja ambaye ni afisa wa Jeshi la Polisi, pamoja na salamu, alisema kuwa kama nipo karibu na baadhi ya viongozi wa CCM niwaambie kuwa muda ukifika hawapaswi kumsimamisha mbunge wa Jimbo la Monduli, Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa katika katika nafasi ya Rais.

Alitoa sababu moja ambayo alisema kuwa ni sababu kubwa sana na itakuwa turufu ya siasa za vyama vya upinzani. Sababu hiyo ni kwamba kabla hajajiuzulu(Lowassa), aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya uchunguzi kuhusu Richmond, Dkt. Harrison Mwakyembe, alitoa majibu ya tume yake mbele ya Bunge huku akirekodiwa na waandishi wa habari na baadhi ya mikanda ya siku hiyo ipo mitaani.

“Ile mikanda inamaana itakusanywa? Maana wapinzani watawawekea wananchi ili waangalie na kusikiliza, itakuwa pigo kubwa kwa CCM na wapenzi wa chma hicho, anayefaa ni mtoto wa mkulima, Mizengo Pinda” aliniambia rafiki yangu huyu.

Sikumpuuza bali niliheshimu mawazo yake na uhuru wa kusema mtazamo wake, ambao kimsingi ulinitia shaka kwasababu yeye pia ni mzawa wa mkoa wa Rukwa, ambako anatokea kiongozi aliyemtaja kuwa nikipata nafasi ya kuzungumza na viongozi wa CCM wenye maamuzi, niwaambie kuwa anafaa fulani na fulani hafai.

Ieleweke kwamba, hakuna kitu kizuri kisicho na ubaya na hakuna ubaya usio na uzuri kwa upande mwingine wa shilingi, sawa na picha mnato ingawa haizungumzi lakini anayeona anaweza kuifurahia au kuichukia.

Kuna wakati niliwahi kusema kuwa nawafurahia sana wezi maana wamenifikisha mahala ambapo katika nyumba yangu niliweza kuweka mlango imara ili wezi wasiweze kuingia kwa urahisi ndani mwangu na kuiba vitu, ingawa sifurahii wizi.

Wizi ni jambo baya na kisheria ni kosa ambalo wanaobainika wanafungwa na baadhi wanaohisiwa wanakamatwa na kuhojiwa na vyombo vya kisheria vinavyohusika(sina imani kama Lowassa alihojiwa na akina Dkt. Mwakyembe).

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimekuwa kikitangazwa na baadhi ya wanasiasa wa vyama pinzani(kwa sasa) kuwa ni chama cha siasa kinachofumbia macho (mafisadi) ambao wamekuwa wakila bila kunawa, lakini sijawahi kuwasikia wakimtaja Lowassa, bali kiongozi huyu anatajwa sana na baadhi ya wapinzani wake wa siasa ndani ya CCM.

Licha ya kuwa ufisadi huo ni jambo baya inapothibitika, lakini nakipongeza sana chama hicho kwa kuwa na kimya kingi ambacho kinaleta mshindo mkubwa kwa vyama vingine vya siasa hapa nchini.

Wanaokitangaza chama hicho kuwa ni chama cha mafisadi hawakosei sana kwasababu kila jambo lina uzuri na ubaya wake kama nilivyosema hapo juu.

Uzuri ninaouona kwa ufisadi wa CCM ni kuruhusu hata baadhi ya makabila ambao kimsingi na kwa historia walikuwa manamba au wapagazi nao sasa ni moja ya wanaotajwa kuwa mafisadi.

CCM imeweka mfumo hata wa wapagazi ambao ni masikini na makabila madogo kama Wakwele, waandali, waha, wanyamanyafu na makabila mengine madogo kuwa viongozi wa nchi hii na baadhi yao kutajwa kwenye ufisadi.

Hofu yangu baada ya kuondoka CCM madarakani ni kwamba taifa linaweza kuwa na mafisadi wa upande mmoja na kabila moja la kusini, kusini magharibi, kaskazini au mashariki.

Leo hii tuna utitiri wa wanaoitwa wagombea wa nafasi za rais kupitia vyama mbalimbali, akiwemo, Edward Lowassa.

Kiongozi huyu tangu mwaka 2008 tuliposikia na kuambiwa kuwa alihusika katika kashfa ya mradi wa kufua umeme wa Richmond, mpaka leo hii hajapelekwa mahakamani na kama amepelekwa basi kwa siri kubwa sana na hata hukumu yake tunashindwa kuelezwa.

Waziri mkuu huyu aliyejiuzuru chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, huku nyikani tunashindwa kuelewa ukweli wake maana miruzi iliyopo huku kwetu ni mingi sana imuhusuyo Lowassa na Rais Kikwete.

Sasa imebaki miezi isiyopungua kumi, ili tuingie katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Ni vema ukweli kuhusu Lowassa dhidi ya tuhuma za ufisadi wa Richmond, ukajulikana ili tumkate kwa nguvu zetu zote au tumkubali kwa vibwebwe na nderemo kuu.

Kama siyo serikali kumpelekea mahakamani kiongozi huyu ili ijulikane ukweli wa miruzi ya ufisadi anaotajwa nao, nimuombe Lowassa mwenyewe, asimame na kueleza ukweli wa tatizo la Richmond na kwanini kama yeye alihusika hajawahi kuomba radhi kwa watanzania kabla hajapiga kipyenga rasmi cha urais.

Kuna maeneo ambayo nimepita hapa nchini, jina la Lowassa limekuwa kama dini, amekaa mioyoni mwa watu hata wasiomfahamu lakini wanaimba Lowassa! Hivyo kabla wengine hawajajawa na imani ya jina Lowassa, ni vema ukweli wa Richmond na Lowassa ukawa peupe kwa mustakabali wa CCM 2015.

Vinginevyo katika jambo hili, Rais Jakaya Kikwete analazimisha Lowassa kuwa mrithi wake na kama siyo hivyo, basi pia analazimisha wananchi wamtafute rais wanayemtaka na wala si yule anayetakiwa na chama fulani cha siasa hapa nchini.

No comments: