Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Tuesday, November 11, 2014

SAUTI KUTOKA NYIKANI............KUPAA NA KUTUNGULIWA KWA CCM MBEYA, KUNATOKANA NA UDINI NA UKABILA

MWENYEKITI WA CCM MKOA WA MBEYA, GODFREY ZAMBI.

NA GORDON KALULUNGA

KUNA makosa ya makusudi ambayo yanafanywa na baadhi ya wanasiasa hapa nchini ya kushindwa kuwaeleza vijana kuwa huwezi ukaelewa kwa undani na ufasaha hali iliyopo bila kuelewa na kuchambua hali iliyotangulia na iliyozaa hali ya leo.

Nampongeza Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM, Abdallah Majura Bulembo, ambaye katika mikutano mingi ambayo anapewa nafasi ya kuhutubia, huwa anaaza kueleza historia ya chama chake na Jumuiya ilikotoka na mpaka leo hii.

Ni dhahiri kwamba tumefanya makosa katika kuchagua silaha; kwani silaha tuliyochagua ni fedha. Vijana wengi ambao wapo kwenye siasa, wanataka kuondoa unyonge kwa kutumia silaha ya wenye nguvu, silaha ambayo sisi wenyewe hatuna, silaha fedha.

Katika mazungumzo yetu, mawazo yetu, na vitendo vyetu ni kama tumekata shauri kwamba bila fedha mapinduzi yetu hayawezekani.

Ni kama tumesema, ‘Fedha ndiyo msingi wa maendeleo. Bila fedha hakuna maendeleo’! Hii ndiyo imani yetu ya sasa.

Viongozi wa Serikali, wanasiasa na watumishi, mawazo yao na matumaini yao ni kwenye fedha. Viongozi wa wananchi na wananchi wenyewe uraiani, Bungeni, baadhi ya vyama vya siasa na makundi mengine ya wananchi, mawazo yao na maombi yao na matumaini yao ni fedha.

Mwalimu Julius Nyerere, katika azimio la Arusha aliwahi kusema kuwa, “Ni kama wote tumekubaliana na tunasema kwa sauti moja, ‘Tukipata fedha tutaendelea, bila fedha hatutaendelea’!

Kama tumetaja na tunapotaja vyombo vingine vya kututimizia shabaha hizo tunavitaja kama nyongeza tu; lakini chombo kikubwa katika akili zetu, silaha kubwa katika mawazo yetu, ni fedha.

Mbunge anaposema kuwa wananchi wa sehemu yake wana shida ya maji, je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa shida hiyo? Jibu analotaka ni kwamba: Serikali inao mpango wa kuwapa maji wananchi wa sehemu hiyo kwa fedha.

Mbunge mwingine anaposema kuwa sehemu yake haina barabara au shule au hospitali au vyote, je, Serikali ina mpango gani? Naye pia jibu ambalo angependa kupewa ni kuwa Serikali inao mpango safi kabisa wa kutengeneza barabara au kujenga shule au hospitali au vyote kwa wananchi wa sehemu ya Mbunge Mheshimiwa huyo kwa fedha.

Kila shida inayolikabili Taifa letu wananchi tunawaza Fedha, watawala majibu yao katika vinywa vyao yamejawa neno fedha!

Cham Cha Mapinduzi (CCM), kimeendelea kujipanga hasa kurejesha majimbo yake ambayo yanaongozwa na wabunge wa vyama vinavyoitwa vya upinzania, viongozi wake hawawazi kutatua matatizo yaliyopelekea kuanguka, wengi wao wanawaza fedha.

Katika mkoa wa Mbeya majimbo mawili yanatawaliwa na Chama cha demokrasia na Maendeleo(Chadema), lakini baadhi ya viongozi na wanachama wanawaza fedha na wala si mahusiano kwanza na wapiga kura.

Majimbo yanayoiumiza kichwa CCM Mbeya ni Jimbo la Mbeya Mjini, linaloongozwa na Joseph Mbilinyi(Sugu) na Jimbo la Mbozi Magharibi linaloongozwa na Silinde.

Majimbo haya yanawapasua vichwa baadhi ya wanachama wa CCM huku baadhi ya wagombea wanaotajwa kuwa wanayataka majimbo hayo, wakibakia na hali ya “kama sintoteuliwa mimi, basi ni bora tukose wote” kama ilivyokuwa mwaka 2010.

Jimbo ambalo linaonekana lina ukakasi kurejea CCM ni jimbo la Mbeya mjini, ambako kwa sasa suala la kupendana kwa wanachama wa ‘CCM’ bado ni kitendawili kama ilivyo ngazi ya urais.

CCM inaonekana kutokuwa kitu kimoja hasa baadhi ya viongozi wanapoelezwa uhalisia, huishia kukasirika.

Suala la ukabila na udini nalo linachukua nafasi kubwa katika chaguzi zijazo majimbo ya mkoa wa Mbeya.

Ni mtu mpuuzi na mjinga pekee ndiye hawezi kutilia maanani suala la ukabila na udini na anaishia kujilaghai nafsi yake mwenyewe kwa kudai kuwa katika nchi hii hakuna udini wala ukabila.

Sina uhakika kuwa ukiwapeleka wakristo wakawa makatibu wa chama na jumuiya zote katika mkoa wa Mjini Magharibi mjini Unguja Zanzibar, chama kitasimama imara.

Sina hakika kama Mchungaji anaweza kukaa katikati ya msikiti wa wayahudi au waislamu akazungumza kisha wakamsikiliza na kutenda kile awaambiacho.

Kuna kosa ambalo CCM imelifanya katika mkoa wa Mbeya, ambalo naamini ni makusudi na kama siyo makusudi basi ni kuonesha ukomo ujao wa chama hicho kutawala katika mkoa wa Mbeya.

Kosa lenyewe ni suala la chama hicho kuweka asilimia 99 ya watendaji wa chama hicho ngazi ya mkoa ambao ni waislamu katikati ya wanachama wa CCM walio wakristo asilimia 99.

Hili ni jambo dogo sana kwa baadhi ya viongozi wa CCM, hasa ambao mawazo yao yamejaa udini na fedha, lakini siku si nyingi baadhi yao watavuna matunda yake na kuamini hiki nisemacho leo, chini ya kiapo cha chama chenyewe kinachojinasibu kuwa “Nitasema ukweli daima fitina kwangu mwiko”.

Sina kisilani wala jambo lolote lililogumu na ndugu zangu waislam, lakini tunapotaka kusema ukweli ni muhimu wakati fulani macho yafumbwe ili mambo yaeleweke bila kuwa na akiba ya ukungu wa wakisemacho watu wa nyikani.

Jambo hili ni moaja ya kigezo ambacho kitachangia CCM iendelee kushindwa katika majimbo ya mkoa wa Mbeya na mahala pengine, kwa kuamini kuwa eti katika nchi hii hakuna udini wala ukabila.

Mwenyekiti wa CCM taifa, Jakaya Kikwete, Katibu Mkuu, Abdurahman Kinana na wengine, kama hawalioni jambo hili kama moja ya kikwazo cha ushindi wa chama chao, wawatume watu wasio makabila wala dini ya walio wengi katika mkoa wa Arusha, Iringa, Kilimajaro, Kagera na kwa mkoa wa Mbeya, waende Majimbo ya Kyela, Rungwe na Mbozi, wakagombee huko na waacheni watendaji wa CCM Mkoa kama walivyo, kisha matokeo yake yataonekana na kufanyiwa tathimini baada ya uchaguzi mkuu 2015.

No comments: