Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Wednesday, November 19, 2014

SOMA SAUTI YA NYIKANI KILA JUMAPILI UK WA 10 GAZETI MTANZANIA.....SIKU 12 GUMU KWA WAKUU WA WILAYA MWAKA 2014

NA GORDON KALULUNGA

MATOKEO ya wanafunzi wa darasa la saba mwaka huu yametoka na nusu ya waliofanya mtihani wamefaulu na wanataraji kuendelea na masomo ya Sekondari kwenye maabara mpya za JK.

Tatizo ninaloliona ni msisitizo wa elimu yetu kutokuwa kwenye kuelewa na kuweza kutumia elimu katika maisha na kutatua matatizo ya jamii inayotuzunguka, bali kinachoangaliwa ni katika kufaulu mtihani kwa kupata alama kadhaa.

Mfano mzuri wa jambo nilisemalo ni waandisi ambao wamekuwa na alama nzuri darasani na kutunukiwa vyeti mbalimbali kuonesha ufanisi darasani, lakini wanapoingia kwenye "ulimwengu wa kazi" inakuwa ni shughuli nyingine kabisa, kwani wafunzwacho kwa nadharia na kufaulu, hakionekani kuwa halisi kwenye utendaji wao.

Haya machache ni matokeo ya kujitwika ukoloni na kuwafunza watoto kisicho na manufaa kwao, achilia mbali wanachofunzwa, angalia wanavyofunzwa.

Suala hili siyo mchapo wa watu wa nyikani, bali linahitaji mjadala mpana sana. Ngoja nirejee kwenye andiko la leo kuhusu urafiki wa wakuu wa wilaya, wakurugenzi na Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Kuna tafsiri pana sana juu ya suala zima la urafiki. Kila mtu aweza kuwa na namna anavyotafsiri, lakini mwisho wa siku, yaonesha tafsiri zote nilizokutana nazo zinahusisha kujaliana kwa watu ama pande husika.

Maana yake ni kwamba inajumuisha kuwa na wakati maalum na wa kutosha wa kujitolea kwa yule uaminiye kuwa rafiki yako.

Katika wimbo ulioimbwa na mwanamuziki Beres Hammond uitwao Friends, anasema kuwa "friends don't mean a thing if when I'm down you keep me down. Friends don't mean a thing, if I can't cry on your shoulder".

Anaenda mbali zaidi na kumuuliza mwenzake anayesema ni rafiki kuwa, kama ni rafiki wa kweli anafanya jitihada za kumjenga na kumwinua juu au anafanya jitihada za kumwangusha chini? Na kwamba je? Kama ni rafiki wa kweli, “kile ninachokihitaji nawe utakuwa nami jirani katika mahitaji hayo”?

Urafiki unaoimbwa na msanii huyo, naufananisha na porojo zilizopo hapa nchini, kwamba Rais Jakaya Kikwete ameteua watu wengi kuwa kwenye mamlaka za serikali kwasababu ni marafiki zake.

Sasa Rais Kikwete ameamua kuimba wimbo kama mwanamuziki Beres, ambapo Septemba1-3,mwaka huu, aliwaita Wakuu wa mikoa yote Tanzania, makatibu tawala, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wote wa Halmashauri za wilaya na miji.

Aliwaita viongozi hao makao makuu ya nchi yetu mjini Dodoma na kuwaeleza kuwa ifikapo mwishoni mwa mwezi huu, ujenzi wa maabara za sayansi katika shule za serikali za sekondari kote nchini ziwe zimekamilika.

Baadhi walipigwa na butwaa, kutokana na kutoweza kutafsiri vema kauli za kiongozi wao mkuu aliyoitoa mwaka 2012.

Agizo la ujenzi wa maabara kote nchini lilitolewa na Rais Kikwete tangu mwaka 2012 alipokuwa huko Itigi Manyoni Singida katika mahafali ya chuo cha uuguzi cha Higi.

Rais Kikwete aliwaagiza wanafunzi wa chuo hicho kuweka juhudi na maarifa katika masomo yao kwasababu watapata ajira, akasema kuwa wakuu wa wilaya wahakikishe maabara zinajengwa katika shule za sekondari ndani ya miaka miwili na kwamba pia kila kijiji na kata kuwe na zahanati na vituo vya afya.

Hakuishia hapo aliwaambia wakuu wa wilaya ambao hawatafanikisha kazi hiyo, watakuwa wamejifukuzisha kazi wenyewe.

Akakaa kimya mpaka pale mwezi Agosti mwaka huu, alipokuwa Kilombero mkoani Morogoro, akasema kuwa agizo lake la miaka miwili limeisha, bali ilikuwa bado miezi mitatu.

Baada ya kauli hiyo, wakuu wa wilaya wote 132 nchini, wakaanza kuhangaika huku na kule kwa ajili ya ujenzi wa maabara za sayansi katika shule za sekondari.

Swali la kujiuliza ni kwamba je, wameshindwa ndani ya miezi 21, wataweza kumaliza kwa siku 12 zilizobaki kuanzia leo?

Nalisema hilo kwasababu, naamini kuwa taasisi ya Rais, ina vyombo vyake na tayari imebaini wilaya ambazo hata wakiongezewa muda wa miezi mitatu hawataweza kumaliza ujenzi huo.

Uteuzi wa wakuu wa wilaya tunaambwa kuwa ni tayari, maana wale ambao wamechunguzwa na vyombo vya taasisi ya Rais, wamebainika ikiwezo suala la ukosefu wa maadili ya uongozi “wameng’olewa” na hawatarudi kwenye nafasi zao.

Desemba 9, mwaka huu, kutakuwa na sherehe za maazimisho ya siku ya uhuru wa Tanganyika, Rais Kikwete akiwa hai, ndiye atakagua gwaride uwanja wa Taifa kama ilivyozoeleka, na baada ya hapo atatakiwa kurudi ofisini ambapo bila shaka kitu cha kwanza ni kuangalia taarifa za ujenzi huo wa maabara katika shule za sekondari za serikali.

Kwa taarifa zilizopo ni kwamba wakuu wa wilaya wanatakiwa wapeleke taarifa zao ofisi ya Tamisemi ifikapo Novemba 30, mwaka huu, kisha zipelekwe ofisi ya Waziri Mkuu, na ifikapo Desemba 9, taarifa ziwe mbele ya meza ya Rais Kikwete.

Nitafurahia kushindwa kushinda kwa watakaoshindwa kukamilisha ujenzi wa maabara ndani ya siku 12 zilizobaki kutokana na agizo la Rais Jakaya Kikwete, alilolitoa kwa Wakurugenzi na wakuu wa wilaya mbele ya makatibu tawala na Wakuu wa mikoa kote nchini, kwasababu watakuwa wameshindwa kutafsiri vema agizo la rafiki yao mkuu aliyewaamini ili wamwinue.

0754 440749
kalulunga2006@gmail.com

No comments: