Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Sunday, December 28, 2014

ILI KUKIDHI HAJA YA WASOMAJI WA BLOG HII YA KALULUNGA MEDIA, TUNAWALETEA UKURASA WA MASHAIRI PIA. KARIBUNI MALARIA  NI HATARI  CHANDARUA ZIFUNGENI

1). Imezuka  tafrani, mbu wako kitandani,
     Zimetujaa huzuni, adui kumbaini,
     Kuleta zogo nyumbani, Juma kalogwa na nani,
           MALARIA NI HATARI, CHANDARUA ZIFUNGENI.

2). Chandarua funikeni, kitandani zibaneni,
      Tutaondoka taabuni, malaria epukeni,
      Nyumbani na safarini, hizo neti kumbukeni,
            MALARIA NI HATARI, CHANDARUA ZIFUNGENI.

3). Zahanati kimbieni, afya sasa chunguzeni,
     Kanuni zingatieni, malaria kutibuni,
     Madimbwi yafukieni, nyasi ndefu zifyekeni,
            MALARIA NI HATARI, CHANDARUA ZIFUNGENI.

4). Rungu sasa pulizeni, mazalia yaueni,
     Tiba bora tafuteni, bima ya afya lipeni,
     Wanakaya andikeni, kadi hizo zitunzeni,
             MALARIA NI HATARI, CHANDARUA ZIFUNGENI.

5). Suluhu itafuteni, homa kichwa na tumboni,
     Kukisia epukeni, majibu kayapateni,
     Kusababishwa na nani, hisia mbovu acheni,
            MALARIA NI HATARI, CHANDARUA ZIFUNGENI.

6). Bango sasa liwekeni, watu wote kumbusheni,
     Tajiri na masikini, mbu atawashusheni,
     Wanene walo sheheni, wembamba mko kwa nani,
              MALARIA NI HATARI, CHANDARUA ZIFUNGENI.

7). Ninaondoka mezani, vyuoni wakumbusheni,
     Vitandani kung’uteni, yasafisheni mabweni,
     Usafi hospitalini, kwenye dawa na wodini,
             MALARIA NI HATARI, CHANDARUA ZIFUNGENI.Na  Festo  E.  Mwalyego  (Fundi)

0-783 879 238    - 29/09/2014

mwalyegof@yahoo.com

No comments: