Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Tuesday, December 16, 2014

NIMEFURAHIA KUSHINDWA KUSHINDA KWA WALIOSHINDWA SERIKALI ZA MITAA


NA GORDON KALULUNGA..............0754 440749
EMAIL;kalulunga2006@gmail.com

NIANZE kwa kuwashukuru sana wasomaji wangu wa safu hii. Wiki iliyopita mpaka wiki hii, nimepokea simu zaidi ya 37 na sms zaidi ya 50 kuhusiana na makala iliyopita kuhusu kilichomponza Waziri wa nishati na madini, Prof. Sospeter Muhongo.

Simu na sms hizo zilikuwa za pande tatu. Mosi, zilielezea hisia za kuipenda makala husika, pili zilikuwa ni za hisia za jumla kwamba waandishi tumehongwa ili kumtetea Waziri huyo kutokana na sakata la Escrow na yale aliyoyasimamia kabla ya maazimio ya Bunge, na tatu ilikuwa kueleza jinsi watu tunavyofahamiana yaani kila mtu kujifahamu mwenyewe, wenzako na kufahamika na Mungu.

Mmoja wa wasomaji aliyesema anahakikisha kila juma hakosi kusoma safu hii, alieleza kuwa Rais Jakaya Kikwete, tutamkumbuka sana kutokana na kuinua demokrasia nchini ambapo baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari wanaweza kuamuru kitu gani kiandikwe au kutangazwa katika vyombo vilivyopo chini ya usimamizi wao, huku wamiliki wa makampuni hayo wakiwa ni Waingereza.

Mwingine alinipigia simu kuwa makala yangu imejibiwa kwenye moja ya gazeti la kila siku, na kwamba sasa sakata la escrow, limehamia kwenye baadhi ya vyombo vya habari akilengwa zaidi Waziri Prof. Muhongo.

Msomaji aliyejitambulisha kwa jina la Madodi, aliniandikia ujumbe uliosem vyombo vya habari vinaweza kumshughulikia mtu kwa visa mpaka jamii ikaamini kuwa ni mtu mbaya.

“Kalulunga, sakata la Escrow limenikumbusha kauli ya Chirchill, nanukuu “Usipokuwa mwangalifu, vyombo vya habari vinaweza kukufanya ukawachukia watu wanaonyanyaswa na kuwapenda watu wanaonyanyasa wenzao” ilieleza sms hiyo ambayo aliileta kwa mfumo wa WhatsApp.

Zipo nyingi zaidi. Lakini nirudie kusema kuwa ukitaka kuwa mtu huru ni vema ukayasimamia unayoyafanyia utafiti, kuyaona, kuyagusa na kuyaishi, kisha kuyaamini kuliko kufanyia kazi hisia za watu wengine.

Wakati fulani katika vitabu vya dini tunaelezwa kuwa, Mungu anaruhusu mahala fulani uharibifu ujitokeze au mtu fulani aondolewe ili watu wajifunze jambo, yawezekana hata Tanzania kuna mambo Mungu huwa anaamua yatokee ili Watanzania tujifunze jambo.

Tuachane na suala hili ambalo Rais Kikwete, ameutangazia ulimwengu kuwa atategua kitendawili hicho wiki inayoanzia kesho Jumatatu, ili hatima ya waliopendekezwa kuvuliwa nyadhifa zao ijulikane kisha tuendelee na fasheni zingine chini ya msemo wa ufisadi.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alitangazia taifa kuwa tuna maadui watatu ambao ni maradhi, ujinga na umasikini. Sina kipimo sahihi ambacho naweza kueleza au kutetea zaidi hoja yangu kuwa tumepambana na kumshinda angalau adui mmoja.

Wakati tunaendelea kuishi kwa matumaini ya kuweza kuwashinda vita vya  adui hao watatu, sasa wamezaliwa maadui wengine watatu ambao ni mapacha wasioweza kutenganishwa katika mfuko wa Watanzania.

Maadui waliozaliwa chini ya himaya ya maradhi, ujinga na umasikini ni adui rushwa, wizi na kufanya kazi kwa mazoea kwa ngazi zote, watumishi wa umma na sekta binafsi.

Kutokana na familia hii ya kifalme ya maadui hawa sita kwa sasa, wanaendelea kufanikiwa katika kampeni yao ya kuwafanya wananchi wa Tanzania kuamini kuwa umasikini ni haki yetu na kila tuambiwacho na matajiri ni sahihi na kila apigapo kelele kuwa anaonewa, basi wengi tunaamini.

Mbali na watanzania wengi kuamini kuwa umasikini ni haki yetu, tunaaminishwa pia katika uchuuzi badala ya kuaminishwa katika uzalishaji.

Kwa sasa, tunakoelekea kama taifa, kwa makusudi tumeamua kuijenga jamii yetu kwenye siasa badala ya kujenga jamii yetu kiuchumi na bahati mbaya kila mmoja hamjui mrithi wa Baba wa taifa, ambaye anaweza kukemea na kuweka msimamo wa Taifa badala ya hivi sasa kila mmoja ni msemaji katika nchi.

Juzi Desemba 14, mwaka huu, watanzania ambao walijiandikisha kwa ajili ya kupiga kura za viongozi wa serikali za mitaa, waliwapigia kura watanzania wenzao waliogombea nafasi mbalimbali kupita vyama vyao vya siasa.

Ukweli ni kuwa, katika uchaguzi huu wa serikali za mitaa 2014, mshindi wa kweli ni mwananchi wa eneo husika endapo tu, watapata kiongozi bora ambaye ni mwadilifu, hapo vyama vitakuwa vimeshindwa na wananchi kuibuka washindi.

Tangu Novemba 30, mwaka huu, tumeshuhudia misuguano iliyotokea kati ya wana vyama ikiwemo kuwekeana pingamizi na wengine kuumizana bila hata maana! Kisa eti vyama vya siasa, harakati na siasa!

Misuguano mingine ilikuwa kwenye kampeni. Maneno ya kejeli na uongo usioweza kuthibitishwa na vijembe, yote yanatokana na kizazi cha kurithishana siasa badala ya kujenga uchumi.

Naamini, walioshinda na kushindwa wote wana uchungu na Tanzania, mitaa na vijiji vyao, hivyo kuwe na kampeni kamili ya kuendelea kuielimisha jamii kuhusu elimu ya uraia na umuhimu wa uchumi badala ya kuendelea kuielimisha jamii kuhusu siasa pekee hasa kutoka katika vinywa vya wanasiasa.

Sasa ni kwanini nafurahia "kushindwa kushinda kwa walioshindwa"?

Sababu kubwa ni kwamba kutakuwa na mengi waliyojifunza kuhusu uchaguzi, mambo mema yatakayoongezeka ifikapo uchaguzi ujao 2015 na kuna dhihirisho kuwa amani yawezekana kuendelea kuwepo na tunasonga mbele kwa pamoja.

Mungu ibariki Afrika, Mungu bariki uchaguzi serikali za mitaa leo, Mungu ibariki Amani tuliyonayo Tanzania.

No comments: