Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Sunday, December 21, 2014

SAUTI KUTOKA NYIKANI.......... RAIS KIKWETE ANASTAHILI KUJIUZULU UENYEKITI CCM TAIFA

NA GORDON KALULUNGA

KUELEKEA sikukuu ya Krismasi, napenda sana kuikumbuka zamani, ingawa baadhi wanaibeza zamani na kwamba zamani hakukuwa na maendeleo kuliko sasa.

Labda ni akili yangu, lakini naona uwiano kati ya mazuri na mabaya ya kiitwacho maendeleo, unaonekana kunufaisha zaidi upande wa mabaya.

Lakini "Maendeleo" ya sasa ni yale ambayo watu wanafanya kile walicho na uhuru nacho, hata kama hakina manufaa kwao. Wanaiga hata yasiyoigika kwao kwa kisingizio cha uhuru na haki, hata kama ni cha athari kwao.

Haya ni baadhi ya mambo yanayonifanya niuchukie U-sasa na ndio maana naikumbuka sana zamani.

Naikumbuka na kuitamani zamani ambayo sherehe kama Krismas na Idd, zilimaanisha uchaji wa kiroho na kukua kwa mauzo ya bidhaa ziendanazo na masuala ya kidini na sio kama ilivyo sasa ambapo sikukuu hizi ni fasheni.

Naikumbuka hiyo zamani, kwasababu familia zilijaliana na si kubaguana na kuchujana kama ilivyo sasa kwa vigezo kama kipato na muonekano wa wanafamilia.

zamani tendo la ndoa lilikuwa na maana sawa na jina lake na si sasa ambako linatumika kuonesha urijali katika jamii.

Zamani, teknolojia ilikuwa yenye nia ya kuboresha maisha na sio sasa ambayo yazidi kuwekeza katika saratani (cancer). Kila kitu ni mionzi na kila muonzi una athari na tunasema "tunaendelea"!

Wasomaji wangu, hapa naizungumzia zamani ile ambayo tulikuwa wazi "kudumisha fikra za Mwenyekiti" na sio sasa ambapo mwenyekiti na watawala wenzake wanadumisha fikra zao kwa mgongo wetu. Tuliona siasa isiyo na visa na mikasa ya ulafi, wizi, uchoyo na ujinga uliopo sasa.

Wiki iliyopita ulifanyika uchaguzi wa serikali za mitaa, wananchi walivishinda vyama vya siasa kwa kuwachagua viongozi waliowataka.

Cha kushangaza kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wasionufaika moja kwa moja na chama, ndiyo wenye uchungu na chama hicho kuliko hata wanaonufaika kwa mishahara, safari na posho!

Wanaonufaika na CCM hawakitakii mema chama hicho, bali wale ambao hawanufaiki nacho ndiyo wanaumia kwa kuona wanashindwa katika nafasi mbalimbali, lakini wanaonufaika utawakuta jioni katika kuta za kumbi za starehe wakicheza na kusema chama kina watu wengi!

Kuna sinema inahusu vita vya Vietnam. Inajulikana kwa jina la (Picha ya Vietnam), kwa wale ambao walikuwa wapenzi wa kuangalia sinema bila shaka wanaikumbuka.

Sinema hiyo inaonesha ni jinsi gani jeshi la Vietnamu lilivyo na askari wengi, wenye mbwembwe za kila namna ya mapigano, licha ya kuwa wengi hawana maarifa ya mapigano bali wanachojivunia ni kwamba wao wapo wengi.

Askari wa jeshi hilo, waliangalia kusonga mbele, hali ambayo askari wa mbele haoni kama nyuma yake askari wanateketea kisha anajikuta amebaki peke yake.

Sinema ya askari wa Vietnam, ni mfano mzuri sana na fundisho kwa CCM, yenye wanachama wengi, endapo (viongozi wakuuu akiwemo Mwenyekiti wangekuwa wanasikia na kutendea kazi mawazo ya watu wa nyikani).

Katika uchaguzi serikali za mitaa uliomalizika wiki iliyopita, wanasema wameshinda kwa asilimia kubwa badala ya kuangalia idadi ya nafasi zilizochukuliwa na vyama vya upinzani.

Uchaguzi  huo, unadhihilisha ni kiasi gani askari wa CCM wanapungua, lakini wakubwa wanazidi kusema chama kipo imara na wanasonga mbele.

Kuna kiongozi mmoja wa chama cha upinzani aliwahi kusema kuwa CCM itafia mikononi mwa, Rais Jakaya Kikwete, lakini watanzania wengi hawakuelewa alikuwa na maana gani……Hasa pale naye (Kikwete), alipoibuka na kusema wanaosema CCM itafia mikononi mwake watakufa wao.

Sanjari na hilo, ikumbukwe kuwa, katika uchaguzi wa CCM kumpata Mwenyekiti mpya mwaka 2012, kuna wana CCM walisema kuwa ili Rais Kikwete asiendelee kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, kwa lengo la kukinusuru chama chao, alistahili kupigiwa kura inayoitwa ya ‘’maruani’’.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM kabla ya kugeuzwa gamba nambari wani, mzee Yusufu Makamba, alitumia muda mwingi wa kumwombea kura za huruma na kwamba Mwenyekiti huyo alifanikisha uchaguzi mwaka 2010 kwa kununua magari aina ya Land crusser.

Alienda mbali na kuwataja kwa kutumia fasihi waliohisiwa na kuonekana kumpinga Kikwete, kuwa nao huko walikokuwa wametoka walikuwa wamepata kura za ndiyo akiwemo Hamis Mgeja, hivyo wampe mwenzao kura za ndiyo.

Akipokea rasimu ya pili ya katiba kutoka kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge maalum la katiba 2014, Samwel Sitta, Rais Kikwete alisema kuwa, wanachokitaka Ukawa na kukisema kwa wananchi ni chema sana, lakini wananchi bado hawajawaelewa.

Yawezekana kutokana na kauli yake hiyo, sasa baadhi ya wananchi wameanza kuelewa vema na wanaikumbuka zamani ya Rais Kikwete, kuwa kumbe wanachokisema wapinzani ni muhimu kwao bali mwanzo walikuwa hawajaelewa.

Ukiwauliza wananchi wengi na baadhi ya viongozi wa CCM kuwa wameanza klini kukichukia chama hicho na serikali yake, wanasema hasa ndani ya utawala wa Rais Kikwete na sababu kubwa ni kwamba kwa sasa CCM imegeuka serikali na Serikali imegeuka kuwa chama.

Serikali inakiongoza chama, kila kukicha viongozi wakuu wa chama wanalalamikia serikali, watumishi wa serikali hawatimizi wajibu wao maana wanajua kuwa chama kinachounda serikali kimegeuka kuwa chama cha walalamikaji.

Kwanini Rais Kikwete anastahili kujiuzulu nafasi ya uenyekiti wa CCM Taifa?

Kuna sababu ambazo zipo wazi kutokana na serikali ya CCM hii ya Rais Kikwete, kushindwa kuchukua hatua stahiki na kwa wakati, yakiwemo masuala ya ufisadi na CCM kuendelea kuporomoka umaarufu na kunyimwa kura kila kona ya nchi.

Sipendi kukuna mahala palipoacha kuwasha, lakini kama ilivyo kwa binadamu kutoweza kusahau historia, kule mkoani Mtwara, serikali yake iliwaachia makovu ya miili baadhi ya wananchi wa mkoa wa Mtwara, kisa ama (kilichoelezwa kuwa eti ilikuwa ni suala la..) gesi asilia.

Hakuna ubishi kuwa katika opareshini ya kutokomeza ujangili nchini baadhi ya wauza duka la CCM yaani watendaji wa serikali waliopelekwa kwenye oparasheni hiyo wameneemeka na kuwaumiza wananchi. Vivyo hivyo, oparesheni Kimbunga na escrow.
Namshauri Rais wangu Kikwete, kabla hajaniteua katika nafasi ya ukuu wa wilaya katika (second selection), ajiuzulu nafasi ya uenyekiti wa CCM Taifa, ili amwachie mwingine arejeshe imani ya chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu 2015, vinginevyo kauli yake ya kuwataka wana CCM kujiandaa kisaikolojia kushindwa,  hakika itatimia zaidi na historia haitamwacha salama.

Nimeyasema haya baada ya kusoma vema ahadi ya nane ya mwana chama wa Chama Cha Mapinduzi, isemayo (Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko).

Mwandishi anapatikana kwa simu 0754 440749/0655 440749
Email; kalulunga2006@gmail.com

No comments: