Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Saturday, December 06, 2014

SAUTI KUTOKA NYIKANI......BUNGE LINAPOKUBALI KUTUMIKA KUVURUGA NCHI

NA GORDON KALULUNGA

TUMESHUHUDIA mnyukano wa sakata la Escrow Bungeni mjini Dodoma, ambako kabla ya maazimio ya Bunge kutokana na kikao cha muhafaka, lilionesha dhahili kutaka kumng’oa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Kabla ya adhima hiyo kufikiwa, Naibu spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, akapewa safari ya kwenda nje ya nchi na kurejeshwa Anne Makinda.

Hakuna ubishi kuwa serikali na vyombo vyake vilifanya kazi nzuri ya kumpa safari Ndugai na kumrejesha Makinda, katika kiti cha Bunge kutokana na hali ilivyokuwa ikienda.

Kutokana na ukweli huu, kuna watu naamini watanipigia simu kunishutumu kuwa naungana na wanaotetea mafisadi katika nchi hii, lakini sintashangaa kwasababu hata maneno watakayotumia yatakuwa ni yale ya kukaririshwa.

Nilipokuwa katika moja ya majalala na vijiwe vya bao huku kwetu nyikani, kuna mtu akawa anatuambia kuwa wale wote waliokuwa wakikomalia suala hilo ni wale wafuasi wa Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, ambaye ni Waziri Mkuu aliyejiuzulu.

Kwa ujasiri mkubwa alianza kuwataja viongozi hao kuwa ni pamoja na Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe, Naibu spika, Job Ndugai ambao kwa pamoja na baadhi ya wabunge wengine, waliamua kumwogopa mwanasheria wa serikali ambaye aliweka wazi kuwa wasimshutumu mtu yeyote bali yeye kwasababu wengine walifuata ushauri wake.

“Hili suala hapana shaka kuwa lilijaa hisia za nafasi ya Rais 2015 na ndiyo maana lilikuwa na mtazamo wa kisiasa zaidi na likapelekwa haraka haraka na kutaka kumsulubu Waziri Mkuu Mizengo Pinda” alisema mwenzetu huyu, huku baadhi wakimpuuza lakini mimi sikuweza kumpuuza hata kidogo maana mambo yote makubwa na madogo yapo huku nyikani na majalalani.

Tukaendelea kumsikiliza akisema kuhusu ufahamu wake juu ya suala la Escrow kuwa, mbali na Waziri Mkuu Pinda, pia suala la kumshupalia Waziri wa Nishati na madini Prof. Saspeter Muhongo, lilikuwa na mambo makuu matatu ambayo ni kauli zake za kebehi kutokana na jeuri ya usomi, visasi vyake na Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi kuhusu vitalu vya gesi na ufutaji wa 'dili' la kampuni ya uwakili ya Mbunge Nimrod Mkono.

Duh! Wengi wakapigwa na butwaa baada ya jamaa huyu kueleza mambo haya hata kabla ya kufafanua kwa undani sababu zake hizi tatu.

Hapo nikakumbuka moja kwa moja kuhusu Umeme hapa nchini tangu enzi za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambapo mpaka hivi karibuni ili mwananchi aingize umeme katika nyumba yake alikuwa analazimika kutoa rushwa na kulipia kihalali zaidi ya 500,000/=, tofauti na sasa ambapo ili kuingiza umeme hasa huku nyikani unapaswa uwe na fedha zisizozidi 157,000/= chini ya Waziri Prof. Muhongo.

Rais Jakaya Kikwete, ameachiwa mtihani mzito wa kuwaingiza watanzania kwenye kansa au donda ndugu la tatizo la umeme nchini kwa kumtoa katika nafasi yake Waziri Prof. Muhongo.

Suala hili kwa baadhi ya wasemaji wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) na wale wenye malengo yao wanaweza kubeza na kutupa lawama kuwa nimelambishwa mshiko na watuhumiwa wa suala la Escrow.

Kuna kiongozi mmoja aliwahi kusema kuwa ni bora kusimamia kwenye kusema ukweli hata kama ukweli huo utakuwa unataka kusababisha kifo chako.

Pamoja na makosa matatu ambayo yanaelekezwa kwa Prof. Muhongo, lakini amethubutu kuleta na kutekeleza mradi wa umeme vijijini kwa bei nafuu.

Endapo Rais Kikwete atakubaliana na maoni ya Bunge ili kumuondoa Prof. 


Muhongo kwenye nafasi yake, Tanzania tunaweza kupata tatizo tena la umeme ambalo wapinzani watatumia kama turufu ya kuwaambia wananchi kuwa CCM iliamua kumuondoa waziri mchapa kazi ili wapate taabu.

Ikumbukwe kuwa, Jaji mstaafu, Joseph Warioba, alikosa Ubunge katika Jimbo la Bunda kwa mara nyingine kutokana na suala la umeme, ambapo umeme ulipita kwenda Musoma katika ardhi ya Bunda bila wananchi wa wilaya hiyo au jimbo hilo kupata umeme.

Nakumbuka kuwa, kwa kipindi hicho, ili umeme uwake Bunda ambalo lilikuwa Jimbo la Jaji Warioba, ilikuwa ikitakiwa kiasi ch fedha za kufungia Transfoma zenye gharama ya Shilingi Milioni 40.

Tunaelekea katika uchaguzi mkuu mwaka 2015, hii itakuwa turufu nzuri ya vyama vya upinzani kuitumia ili kusaka ushindi na tayari wameanza kuitumia escrow huku viongozi wa CCM hakuna anayetetea hoja hiyo ya wapinzani.

Kuna mahala niliwahi kusema ukweli wa udhaifu wa baadhi ya viongozi wa CCM mkoa wa Mbeya, nikaambiwa kuwa mimi ni mfuasi wa Chadema!, lakini niliwaambia kuwa waendelee kusema hivyo ili siku ikifika wananchi watakuja kuelewa kuwa kumbe wasema ukweli wapo ndani ya Chadema.

Tukilitafakari jambo hili kwa umakini, tutafahamu kwa pamoja kuwa, Bunge likiacha kutumika kuivuruga nchi tutakuwa salama na ikumbukwe kauli ya spikan wa Bunge aliyoitoa wakati wa kuahirishwa Bunge kuwa Wabunge waache kuraghaiwa na fedha ili kuvuruga mambo Bungeni.

No comments: