Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Sunday, December 28, 2014

SAUTI KUTOKA NYIKANI................RAIS KIKWETE BABA WA DEMOKRASIA ASIYETHAMINIWA AKIWA MADARAKANI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 2005-2015. Jakaya Mrisho Kikwete

NA GORDON KALULUNGA

KUNA wakati niliwahi kusema kuwa, ubora wa Taifa lolote lile hutegemea ubora wa mawazo ya watu wanaounda Taifa hilo pamoja na nidhamu ya watu wao.

Kwa kuwa mtu ni mawazo anayofikiri na jamii pia huundwa na mawazo basi kama jamii yetu sio bora tuangalie upya mawazo yetu sote na hiki tukipandacho leo, ndicho tutakachokivuna.

Baadae yetu itategemea ubora wa fikra zetu na maamuzi yetu tutakayofanya kwa faida ya kesho. Taifa hili litafika mbali ikiwa tu tutabadili mwelekeo wa mawazo yetu, kujali muda na maamuzi yetu.

Kwa sasa taifa limefikia mahala pa baadhi ya viongozi wetu kuendesha nchi kutokana na mashinikizo, wala si maamuzi sahihi kama nyumba kuu inavyotaka kuendesha nchi kwa umuhimu wa nchi yetu.

Ili kudumisha mila na desturi zetu huku nyikani, viongozi wengi wanatuimarisha kwa kutumia sentensi isemayo (mwiko na atakayethubutu asije akalaumu). Hakika anayepuza sentesnsi ya namna iyo ya viongozi mwisho wake unakuwa mbaya.

Wanatumia sentesi hiyo kwa sababu kuu moja ambayo najengwa katka msingi wa msemo wa wahenga kuwa hofu ina nguvu kuu ya kuonya.

Wiki iliyopita, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, alichukua maamuzi ya kumfuta kazi aliyekuwa Waziri wa Nyumba na Makazi, Prof Anna Tibaijuka, kwa kosa la kukiuka maadili ya uongozi. Hongera sana Rais Kikwete.

Siku moja baadaye, Katibu Mkuu Kiongozi, kwa mamlaka aliyonayo kisheria, alimsimamisha kazi, Katibu mkuu wa Wizara wa Nishati na madini, Eliakimu Maswi, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomhusu kama ilivyokuwa imependekezwa na Bunge kutokana na sakata la Tegeta Escrow.

Hatua hizi zimechukuliwa na viongozi hao dhidi ya viongozi walio chini yao kwa wao kudhani kuwa wamechukua hatua kwa muda muhafaka, lakini kimsingi hatua hizo zimechelewa kuchukuliwa, hasa kwa watu wa nyikani wapenda Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Zimechelewa kwasababu watu hawa wa nyikani wanakumbuka jinsi gani maamuzi ya haraka na haraka haraka yalichukuliwa dhidi ya tuhuma za Richmond, Dowans, oparesheni tokomeza na akina Kagasheki.

Sitaki kusema kuwa Rais wangu Kikwete sasa amekua na kuamua kufuata misingi ya haki za binadamu na sheria, licha ya watanzania wengi kwa sasa kuhitaji Rais Dikteta kidogo na nakumbuka kauli ya aliyekuwa Spika wa Bunge, Samwel Sitta, aliwahi kumwambia, Rais Kikwete anapaswa kuwa mkali kidogo.

Nasema Rais amekua kwasababu naamini anakumbuka mkenge wa shinikizo la kuchukua hatua haraka na haraka haraka, bila kujali na kupatanisha kwanza mihimili ya serikali inapogongana kisheria au kimaslahi kama maamuzi ya suala la Richmond.

Suala la Richmond lililopjitokeza, Serikali ilifanya haraka na haraka haraka kufuta mkataba, ilipopelekwa Mahakamani Serikali ikashindwa, mjomba wangu Dr.Harrison Mwakyembe, alisikika akisema kuwa ataishangaa serikali ikikubali kuilipa Richmond.

Kwa hekima kabisa, Rais Kikwete akamteua Dr. Mwakyembe na wenzake ili kukata rufaa, ambapo baada ya kukamilisha taratibu za rufaa, rufaa hiyo ikatupiliwa mbali na Mahakama na mpaka sasa Serikali inalipa fedha nyingi na hayo yote ni matunda ya kukurupuka kimaamuzi kutokana na mashinikizo.

Katika maamuzi aliyoyatoa hivi karibuni Rais Kikwete ingawa kwa kuchelewa, naiona dhamira ya Rais kutaka zaidi kuzingatia misingi ya sheria na utiririshaji wa demokrasia kwa binadamu wote bila kjali kuwa tuhuma hizo zinatoka upande gani.

Lakini ikumbukwe pia kuwa si kila jambo linalosemwa na Mbunge ni sahihi. Kwasababu si wabunge wote wanaingia bungeni kutokana na taaluma zao, hivyo wabunge siyo wahasibu, wabunge siyo wanasheria, wabunge siyo madaktari, wabunge siyo walimu wala wabunge siyo wajuzi wa masuala ya upelelezi na ulinni wa mipaka ya nchi.

Wanaomshinikiza Rais kufanya watakayo, wanapenda sana kumuona anakosea na kuaibika kila kona. Jambo ambalo si jema kwa mustakabali wa maendeleo ya jamii yetu.

Tuna mifano hai ya akina Zito Kabwe, Kafulila kufukuzwa katika vyama vyao vinavyojiita vya demokrasia, ambavyo sawa na mtu anayetangaza amani huku akiwa na upanga nyuma. Yaani vyama vinavyotangaza demokrasia huku vikiishi na kutekeleza udikteta kwa kufukuza yeyote anayeonekana yupo kinyume na matakwa hasi.

Pamoja na mambo hayo, Rais Kikwete anapaswa kujitafakari pamoja na jopo lake la watu wanaomzunguka, kama yeye ni mchezaji mzuri na amezingirwa na wachezaji waliochini ya kiwango, hakika atapwaya mpaka mwisho wa utawala wake.

bila elimu sahihi kwa umma kuhusu suala la maamuzi ya Escrow, watu bado watakumbuka kile kinachoitwa miujiza inayofanywa na Rais Jakaya Kikwete kuruhusu uchunguzi juu ya uchunguzi, kwasababu suala la escrow, CAG alichunguza, TAKUKURU walichunguza, kamati ya Bunge PAC chini ya wabunge 19 wa CCM dhidi ya wapinzani watano ilichunguza, TRA na BRELA walishathibitisha, hivyo kusema Rais anafanya miujiza isichukuliwe kama dhihaka.

Katika maandiko matakatifu kutoka kwenye Biblia, yanasema kuwa, wakati fulani, Mtume Paulo akawauliza Wagaratia, kuwa ‘’ Enyi Wagaratia, ni nani aliyewaroga’’

Nitumie fursa hii kumuuliza Rais wangu Kikwete kuwa ni nani aliyembadilisha? Maana alipokuwa akingia madarakani wengi ndani ya chama, serikali na hata nje walimpachika majina mengi yakiwemo ya kumwita chaguo la Mungu wengine walimwita Mussa kutokana na ziara za kushitukiza na maamuzi aliyokuwa akiyafanya kwa kushirikiana na aliyekuwa Waziri Mkuu wake, mchezaji mwenzake, Edward Lowassa.

Leo hii, sijajua majina hayo yote mazuri yameyeyukia wapi! Kwa mwendo huu, wapinzani hawataacha kutoa mashinikizo ya jinsi gani serikali ifanye kazi yake badala ya serikali kutoa mwongozo, lakini nina matumaini kuwa, Rais ajaye, hatoweza kurudia yanayoonekana kuwa ni makosa yaliyopo chini ya Rais Kikwete.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa Barua pepe; kalulunga2006@gmail.com
0754 440749

No comments: