Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Monday, December 01, 2014

SERIKALI YA HILA HAIWEZI KUSIMAMA MPAKA ITUBU

NA GORDON KALULUNGA

JAMII tuliyonayo kwa sasa ni jamii yenye upendo wa mashaka kwa watoto wetu.

Waliobahatika kuzaa watoto, hasa wafanya kazi, baada ya watoto hao kufikisha umri wa miezi mitatu, wanawapeleka katika vituo vya kulelea watoto viitwavyo(shule).

Wakitoka makazini wanaenda kuwachukua watoto hao kwa ajili ya kwenda (kulala), nao.

Watoto hao wakifikisha mwaka mmoja, wanapelekwa kwenda kuishi katika shule za bweni, wazazi wakidhani kuwa wanao upendo wa Agape(uliotopea) kwa watoto wao.

Watoto hao wanaendelea kupunguza upendo kwa wazazi wao taratibu bila wazazi kutambua jambo hilo.

Nchi za ulaya, wazee wamejengewa makazi yao mbali na watoto wao, hali ambayo naiona kwa baadhi ya sisi wazee tarajali hapa nchini, ambapo watoto hawa tunaodhania kuwa tunawapenda na kuwapeleka shule za bweni wakiwa angali wadogo, wakikua, watatujengea mabweni ili tusiwe karibu nao kama ambavyo nasi hatutaki watoto hawa wawe karibu nasi.

Kutokana na upendo huo kupungua, huku nyikani kulikuwa na kijana mmoja aliyekuwa na mafanikio ya kifedha, alitembelewa na Baba yake mzazi ambaye aliishi kwa mtoto wake kwa mwaka mmoja.

Kutokana na kile kiitwacho adha ya kulea wazee, kijana huyo akashauliawa na mkewe na wakakubaliana kwenda kumtupa yule mzee porini.

Walifanya hivyo na kwenda kumtupa yule mzee katika pori lililokuwa nje ya mji. Baada ya kumtupa na kumpa kisogo, yule mzee akamwita mwanae na kwamba anahitaji kumwambia neno la mwisho.

Yule kijana alipomrejea mzazi wake, akaambiwa “Nashukuru kwa kuja kunitupa huku porini, lakini kabla hujaondoka, naomba unirejeshe nyumbani kwangu kijijini, ili laana hii isije kukurudia wewe na vizazi vyako” alisema yule mzee.

Alimwambia kuwa akimwacha pale, naye akizeeka, atatupwa na wototo wake kama anavyomtupa yeye. Yule kijana akafikiri na akafikia hatua ya kurejea nyumbani na Baba yake mzazi ili asije akapata laana ya kurejewa na tukio hilo.

Vivyo hivyo, watawala wakiwa na nia za hila katika suala la kuendesha nchi, laana hiyo haitakwisha.

Tumeendelea kushuhudia masuala ya tuhuma za ufisadi katika nchi yetu, hiyo yote ni moja ya laana ya hila za watawaa wetu kukalia poritiki za kunyoosheana vidole hata pasipokuwa na ushahidi.

Nakumbuka kauli ya Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, aliwahi kusema kuwa, “Sisi wote hapa ni wanasiasa, tukiendelea kusikiliza minong’ono ya mitaani nani atapona hapa’’, alihoji kabla hajatangaza kujiuzulu nafasi ya Uwaziri Mkuu.

Kwa sasa limejitokeza sakata la Escrow, ambalo limekuwa gumzo mtaani na serikalini, lakini kwasababu serikali inajisikiliza zaidi yenyewe badala ya kusikiliza hali ivumayo mitaani, matokeo yake chama kilichopo madarakani kinapunguza mashabiki wake.

Aibu hii, ingawa baadhi wanadhani ni aibu ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, lakini kwa uhalisia wake ni kwamba aibu hii itaendelea kuwa juu ya Rais Jakaya Kikwete.

Niliwahi kusema wakati fulani kuwa, mahala penye kidonda katika mwili wa binadamu panapaswa kutibiwa kidonda hicho badala ya kupaka dawa ya kutuliza maumivu huku mwili ukiendelea kuchimbika.

Sina tatizo na kugawana kwa waliogawana fedha za akaunti ya Escrow, bali tatizo langu kwenye suala hilo ni kodi. Huku nyikani, akina mama wenye mitaji ya Shilingi Elfu Mbili wanaouza mbogamboga na karanga, wanatozwa ushuru, lakini fedha hiyo inaonesha haijawahi kutozwa kodi!

Wengi tumeshuhudia malumbano ya Bungeni huku serikali ikiingilia kati kutetea watuhumiwa mbele ya chombo cha habari cha Taifa(TBC1)!

Nasema serikali ya hila haiwezi kusimama mpaka itubu kwasababu, CCM imeshauriwa mara kadhaa lakini wakubwa hawafanyii kazi ushauri wa wanachama na wananchi wa kawaida wasi viongozi.

Yawezekana yote hayo ni kutimia ka maandiko yasemayo kuwa “Hekima ya masikini haisikilizwi”. Hali hiyo inapelekea kuogezeka kwa wanaokubalia kutokubaliana na CCM, na nchi kuyumba kwa mfano.
Hila hizo ni pamoja na mgombea anapogombea na kushinda unakuja kuambiwa huyu alitoa rushwa jina lake limekatwa na kuchukuliwa jina la pili, hili linaleta sintofahamu kwa wananchi na mgawanyiko unatokea.

Matajiri kumiliki chama hilo nalo ni hatari na ndiyo maana hata vijana wengi wasio na pesa licha ya kuwa na uwezo wa kuongoza hawawezi kuwania nafasi kama za Ubunge na Udiwani ndani ya CCM.

Hila za kusingiziana zinaendelea kuzidi ndani ya CCM kwa ni moja ya kukomoana na kulipiziana visasi, bahati mbaya nao baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani navyo vinaiga yale yale yafanywayo na CCM ya hila na visasi! Hakika kila mwenye hila atapata na kuondoka kwa hila.

Kizazi hiki kinataka maji, Barabara, madaraja, umeme, shule, kazi, zahanati, usalama na madawa, wala hakitaki fitina zenu kama wanasiasa ambazo manufaa makubwa ni yenu wenyewe na wala si kwa faida ya wananch.

Hila hizo hazitawaacha salama kama ambavyo hila alizotendewa Lowassa, zinavyoendelea kuurudi utawala chini ya Rais Kikwete, ingawa tukiseama haya tunaonekana tumenunuliwa.

Mwandishi anapatikana kwa simu 0754 440 749 
EMAIL; kalulunga2006@gmail.com

No comments: