Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Wednesday, January 07, 2015

HIFADHI YA KITULO NA UPEKEE WA NYARA ZA SERIKALI

GORDON KALULUNGA, MBEYA
 
HIFADHI ya kitaifa ya Kitulo ipo kati ya mkoa wa Njombe na mkoa wa Mbeya, kusini Magharibi mwa Tanzania. Ina upekee wa vivutio vyake ambavyo kisheria ni nyara za serikali.
 
Hifadhi hii ndiyo eneo pekee Tanzania lenye ndege aina ya Tandawala machaka (Denhams Bustard) wenye uwezo wa kuruka kutoka bara moja hadi jingine.
 
Pia ndani ya hifadhi kuna Maua na viazi vya asili vinavyoaminika kuliwa na matajiri na kutibu ugonjwa wa Ukimwi, viitwavyo kwa jina la Chikanda.
 
Ilitangazwa rasmi kuwa hifadhi ya Taifa mwaka 2005, ikijumuisha sehemu ya eneo la shamba la mifugo, msitu wa Livingstone na bonde la Numbi.
 
Kitulo ina ukubwa wa kilometa za mraba 442. Awali ilijulikana kama Elton Plateau baada ya Mvumbuzi Fredirick Elton kupita eneo hilo mwaka 1870.
 
Mwaka 1960 Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) lilichukua eneo hilo kwa ajili ya ukulima wa ngano na ufugaji wa kondoo.
 
Ndege hao wamekuwa na tabia katika msimu fulani kuruka na kufika katika Hifadhi ya Taifa ya Kitulo kwa ajili ya kutaga mayai na kuangua vifaranga kutokana na mazingira ya hifadhi hiyo kuonekana kuwa ni mahali pekee duniani penye hali ya hewa rafiki kwa ndege hao kuzaliana. Hivyo baada ya kutaga mayai, kuangua vifaranga na ndege kukua, huruka na kwenda mabara mengine duniani.
 
Utafiti umebaini kuwa katika Hifadhi ya Kitulo ndege aina ya abdims stock, denhams (tandawili machaka) na blue swallow ambao wametoka Afrika Kaskazini, Afrika Kusini, Australia na Ulaya wanaitumia Hifadhi ya Kitulo kama makazi yao katika misimu tofauti.
 
Licha ya ndege adimu waliopo, pia kuna zaidi ya aina 40 za maua mbalimbali ambayo hayapatikani sehemu nyingine yoyote duniani na kiazi Chikanda ambacho kinaaminika kuwa ni dawa ya maradhi ya Ukimwi.
 
Kutokana na nadharia hiyo ya kiazi hicho kinachofanana na kiazi mviringo, ingawa chinyewe katika shina lake huzaa kiazi kimoja pekee, kumekuwa na (ujangili) wa biashara ya kuusafirisha kuuza mmea huo katika mataifa jirani na Tanzania ambayo ni Zambia na Malawi.
 
Akizungumza na Mwandishi wa makala haya mwanzoni mwa mwaka 2014, katika kijiji cha Ifupa, kata ya Ilungu wilaya ya Mbeya Vijijini, kuhusiana na kiazi Chikanda, Kaimu Mhifadhi mkuu wa hifadhi hiyo, Pius Mzimbe, alisema kiazi cha mmea huo, kipo kwenye kundi la nyara za serikali na kwamba anayevuna kiazi hicho akibainika anahesabiwa amefanya kosa la jinai.
 
Alisema, kimsingi matajiri ndio wanaojihusisha kwa kuwatumia vijana kuvuna zao hilo la asili ambalo ni kivutio cha taifa.
 

“Vijana wengi walikuwa wakitumika katika shughuli za ujangili, lakini kwa sasa baada ya kuwapa elimu ya kutunza mazingira na hifadhi ya kituo, vitendo hivyo vimepungua kwa kiasi kikubwa,’’ alisema.
 
 

“Viazi hivi vina soko Zambia ambako debe moja linakadiriwa kufikia sh 70,000 mpaka 100,000/= na watu wanaokula viazi hivyo ni matajiri, hapa Tanzania bado haijajulikana matumizi yake,” alisema.
 

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk. Norman Sigalla, alisema uongozi wa hifadhi hiyo umefanya vema kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa wananchi, hasa vijana.
 

Diwani wa Ilungu, Hashimu Mwashang’ombe, alisema awali wananchi wengi hawakutambua umuhimu wa kushirikiana na uongozi wa hifadhi, lakini baada ya kupata elimu na serikali kuonyesha mipaka kati ya wananchi na hifadhi, kwa sasa wananchi hawana tatizo na uongozi wa hifadhi.
 
Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa, licha ya kiazi hicho kuwa ni moja ya nyara za serikali, katika mji wa Tunduma wilayani Momba mkoani Mbeya, kiazi hicho kinauzwa kama chakula cha kawaida na hakuna mamlaka zinazohusika kukamata wala kutoa onyo kwa wanaofanya biashara ya kiazi hicho adimu duniani.
 
Katika kukabiliana na majangili wanaovuna mmea huo, alisema wanakitumia kitengo chao cha ulinzi na intelejensia ambacho kwa kiasi kikubwa kimeanza kufanikiwa kuwadhibiti wavunaji haramu wa mmea huo.
 
 
Mhifadhi wa utalii katika hifadhi hiyo, Rimus Mkongwe alisema ndani ya hifadhi hiyo kuna aina 40 za mmea huo, hata hivyo akasema unaotakiwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu ni ule unatoa majani mawili.
 
 
Anasema taarifa walizonazo kutoka katika nchi ambazo zinazonunua kiazi kitokanacho na mmea huo, zinaonesha kwamba kinaliwa zaidi na matajiri wakubwa wa nchi hizo.
 
 
Mbali na kiazi hicho kuaminika kuwa kinatibu maradhi ya ugonjwa wa Ukimwi, hakuna tafiti zilizofanyika na kuthibitisha kuwa kiazi hicho ni dawa ya Ukimwi.
 
Watalii wanaotembelea Hifadhi ya Taifa ya Kitulo, wanapata wasaa wa kuangalia ndege adimu katika Ziwa Zambwe na misitu, kuweka kambi kwa ajili ya malengo mbalimbali, utalii wa kutembea kwa miguu, kupanda farasi, michezo ya gofu na kukwea milima.
 
Mwandishi wa makala 0754 440749

No comments: