Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Saturday, January 17, 2015

MTANDAO WA ASASI NKASI, WANUIA KUONGEZA WIGO WA UFUATILIAJI WA MATUMIZI WA RASILIMALI ZA UMMA

LICHA ya baadhi ya watendaji katika idara za kiserikali kuuona mradi wa Ufuatiliaji wa Matumizi ya Rasilimali za Umma(PETS) kama mwiba kwao,mtandao wa asasi zisizo za kiserikali wilayani Nkasi mkoani Rukwa(Nkango) umesema utaendelea kutoa elimu ya mradi huo.

Mwenyekiti wa Nkango Victor Sadalla anasema watendaji wengi katika idara za kiserikali hawaupendi mradi wa PETS kwakuwa wanaamini ni mradi unaolenga kufichua maovu yao kwa jamii wanayoitumikia kwa kuwafumbua macho wananchi.

Hata hivyo jana katika warsha ya mafunzo ya mwongozo wa PETS kwa viongozi wa asasi zinazounda mtandao wa Nkango na maofisa watendaji katika ngazi za vijiji na kata za wilayani hapa, Sadalla alisema mradi huu unalenga kuboresha utendaji kazi wa idara za kiserikali.

Alisema bado kunahitajika elimu zaidi kwa jamii kufuatilia matumizi ya rasilimali zinazowazunguka na huo utakuwa ni ushiriki mzuri katika utekelezaji wa mipango sahihi ya serikali yenye lengo la kuleta maendeleo.

Alisema pamoja na changamoto za kutokubalika kwa mradi wa kwatendaji mtandao huo utaendelea kutoa elimu hiyo na kuwataka watendaji katika idara za serikali kuutambua kama kichocheo cha maendeleo.

Kwa upande wake Afisa Tawala wa wilaya ya Nkasi Mwanaisha Luaga akifungua warsha hiyo anasema PETS haipo kumhukumu mtu bali kufichua mambo yasiyokwenda sawa katika utendaji na wanaoichukia hawatambui umuhimu wake.

“PETS haimhukumu mtu.Ipo kutoa changamoto kwenye utendaji kazi wetu wa kila siku.Sisi kama watendaji wa serikali kuu na serikali za mitaa tunapaswa kuuona mradi huu kama chombo chenye manufaa kwakuwa kinatukumbusha hata pale baadhi yetu tunapojisahau” alisema afisa tawala na kuongeza

“Ni imani yangu kuwa kadiri elimu inavyoendelea kutolewa,kama vile wananchi wanavyotambua umuhimu wa kufuatilia matumizi ya rasilimali zilizopo ndivyo na sisi watendaji tutaendelea kutambua umuhimu wa mradi huu na kuanza kutoa ushirikiano”

Katika warsha hiyo ya siku mbili inayofanyika kwa ufadhili wa shirika la The Foundation For Civil Society,washiriki wanajifunza maana halisi ya PETS,Vijana na PETS,Mifumo ya serikali kuu na serikali za mitaa na pia Utaratibu wa uendeshaji mradi wa PETS kwa maslahi ya jamii.

No comments: