Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Thursday, January 15, 2015

SAUTI KUTOKA NYIKANI.... SHETANI AMEANZA KUHUBIRI INJILI YA KUMJUA MUNGU


NA GORDON KALULUNGA

HALI ya kisiasa imegeuka nchini. Imerejea hali ya mwaka 1995 ambapo Agustino Lyatonga Mrema, chini ya chama NCCR-Mageuzi, alikuwa akisukumwa na wananchi na baadhi kufikia hatua ya kuachana na ajira serikalini baada ya kuona mwanga wa nyota ya kuelekea Ikulu.

Chadema iliyosemwa kwa kila aina ya uovu, sasa imeanza kuaminika kwa kiasi kikubwa na baadhi ya wananchi huku baadhi wakiwa hawana hoja yeyote zaidi ya hasira na CCM.

Mwenge wa uhuru unaokimbizwa na vijana kila mwaka, awali mpaka sasa, tumefundishwa kuwa, mahala unapopita, kama kulikuwa na chuki huleta Amani, heshima mahala palipojawa na dharau na umoja penye mafarakano.

Ishara hiyo ya Mwenge, ndiyo inategemewa kuwa nuru ya viongozi wa mahala pote na kwamba kama vile Mwenge unavyokuwa mbele, vivyo hivyo hata viongozi wanatakiwa kuwa mbele kumulika na kuunganisha watu wote.

Watu wa huku nyikani wana msemo unaosema kuwa, kila mchunga ataulizwa juu ya kondoo wake.

Msemo huo, unashabiiana na kipimo pekee cha uimara wa chama cha siasa kuwa ni uchaguzi. Uchaguzi wa serikali za mitaa CCM kwa ujumla wake imeongoza kwa wajumbe wake kuchaguliwa.

Hali hiyo imetoa faraja kubwa kwa chama tawala na kuacha ujumbe katika mioyo ya makada, wanachama na mashabiki wa chama hicho kuwa kwa sasa CCM ina faraja lakini haina jeuri.

Chama hicho kimeongoza kutokana na baadhi ya sehemu kupita bila kupingwa baada ya vyama vingine kutoweza kusimamisha wagombea katika maeneo hayo huku pingamizi pia zikikinasua kwa baadhi ya maeneo.

Dalili hizo zinaondoa jeuri ya CCM kwa umma na kukiachia faraja, ambayo inaweza kuondoka kutokana na uchaguzi mkuu wa mwaka huu hasa katika nafasi za madiwani ambapo vyama vya upinzani vinaonyesha kujipanga zaidi na kutaraji kusimamisha wagombea katika kata nyingi.

CCM imeshindwa hata kuuisha maisha ya viongozi wake wa ngazi mbalimbali, jambo ambalo linafanya hata wana CCM wenyewe kukata tamaa, tofauti na vyama vingine ambavyo vinawekeza kwenye mioyo ya wananchi na viongozi wake wa ngazi za chini kwa ahadi hata kama ni za kufikirika na vinajitahidi hata kutoa pikipiki.

Leo hii viongozi wa vijana wa UVCCM hata ngazi ya taifa na mikoa, hawana hata baiskeli, hao ndiyo wanategemewa kuwa chama kiwe mioyoni mwao na kuwashawishi wenzao wa wilaya, kata, matawi na mashina kuipenda CCM.

CCM wakubwa, hawataki kukutana na makada wake na kuwauliza walipokosea ni wapi. Viongozi wa ngazi za juu wanajisahihisha wenyewe huku wakiwa hawapatani.

Wanafanya mikutano ya kujihutubia na kupeana mawazo wenyewe huku wanachama wakisubiri kufanyia kazi maelekezo kutoka juu ambako kuna viongozi pekee badala ya wanachama walio wengi.

Ngazi za chini kwa wanachama wa kawaida, ambao ndiyo wanafahamu matatizo halisi ya chama hawashirikishwi kutoa maoni yao juu ya mwenendo halisi wa chama chao, badala yake viongozi ndiyo wanapanga na kuamua kila kitu wakiziamini taarifa hasi za viongozi wenzao kutoka ngazi za matawi, wilaya na mkoa.

Imefikia mahala sasa, hata wale makada wenye uwezo hata wa kuonana na Nape Nnauye, wanaogopa kutoa ushauri kwa chama chao kwasababu hawana vyeo na wakitaka kuthubutu wanaogopa kuambiwa au kuhisiwa kuwa njaa ndizo zinawapeleka.

Waandishi wa habari hasa wachambuzi kadhaa wa masuala ya siasa wanapoandika, sidhani kama wahusika wa vyama husika wanatilia manani, badala ya kuishia kubeza kwa kusema kuwa siku hizi hakuna waandishi wa habari.

Kuendelea kuporomoka kwa CCM kunatokana na chama hicho kubaki kuwa chama cha viongozi badala ya kuwa chama cha wanachama.

Katika uhakika wa kuwa chama hicho ni mali ya viongozi, awali chama kilikuwa na chipukizi, kwa sasa limebaki jina na idara hiyo makao makuu na akina Paul Makonda na waliopo wengine ni wale wa watoto wa wakubwa wakiwaandaa kuwa viongozi wa jumuiya ya vijana (UVCCM) na hatimaye chama, na mahala pengine waliobaki ni wale wanaovalisha skafu katika matuki maalum tu.

Mikutano ya mabalozi wa nyumba kumi kwa ajili ya wanachama haipo. Mashina ya vijana wakereketwa hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi yapo na yanaendelea kujengwa kwa ajili ya kupata chochote kutoka kwa wagombea, lakini hata wao hawajuani kuwa wapo wangapi na majukumu yao ni nini!

Kwenye matawi ya chama hicho, kuna takwimu za idadi ya wanachama ambazo hata walioandika na kupokezana madaraka hawajui kama ni sahihi ama la! Maana hata mikutano ya wanachama wote haipo, bali mikutano ya viongozi pekee.

Kwa sasa Taifa linashuhudia baadhi ya wanachama wa CCM, hasa wanaohitaji kuwania nafasi za urais, Ubunge na udiwani, wakihaha kwenda katika nyumba za ibada kila jumapili kama ya leo, kusaka maombi ya viongozi wa dini.

Badala ya kwenda kuomba toba za mambo yao waliyolikosea taifa, kila mmoja analalamika kuhusu wenzake anaoona kuwa wanamzidi ushawishi kwa umma na kudai kuwa wenzao wanatumia fedha (rushwa) kutaka uongozi.

Wanaomba huruma za viongozi na waumini wa dini, huku wakiwa na vyombo vya habari pembeni yao ili taifa liwasikie.

Kati ya viongozi hao, hakuna anayewaza kuwaomba viongozi wa dini kuombea viongozi wakuu wa chama chao ambao kila mmoja anawaza familia yake, panya road na makundi ya urais.

Kilichobaki kwa CCM ni kuviziana badala ya kurekebishana na kuambiana ukweli ili kwa pamoja wajirekebishe na kupunguza makundi kabla ya chaguzi, kila mmoja anawaza kumkomoa mwenzake au mwanachama mwingine wakati wa nafasi za uchaguzi.

Kwa wale wanaoenda kutangazia nia zao katika nyumba za ibada, wakumbuke kuwa hata Rais Jakaya Kikwete, aliitwa na baadhi yao kuwa ni chaguo la Mungu na mwisho tunashuhudia walivyomgeuka na kwamba hafai na nchi imemshinda huku kila kukicha wakitoa matamko dhidi ya serikali.

No comments: