Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Monday, January 05, 2015

SAUTI KUTOKA NYIKANI.....WAANDISHI WENZANGU NISIKILIZENI KWA AJILI YA MWAKA 2015


NA GORDON KALULUNGA

NAWAPONGEZA wasomaji wangu, viongozi wangu na wafanyakazi wote wa kampuni ya New Habari (2006) Ltd inayochapisha magazeti ya Mtanzania, The African, Dimba, Bingwa na Rai kwa kuuona mwaka mpya wa 2015.

Mimi pia na familia yangu tunajipongeza kwa kuwa miongoni mwenu na tunatubu kwa yote tuliyoyafanya kwa kujua ama kutofahamu, yale ambayo inawezekana kuna mengine yalisabahisha baadhi ya watu kukosa amani au hata kumuudhi Mungu.

Kila mmoja atafakari kuwa ni mambo mangapi yaliyo mema aliyofanya mwaka 2014 na aliyokosea. Hakuna mashaka kuwa kila mmoja ana majibu katika mapito yake ya mwaka mzima uliomalizika Jumatano, wiki hii.

Katika Biblia Takatifu, Kitabu cha Mithali 28:13 kinasema ifuatavyo: “Afichae dhambi zake hatafanikiwa, bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema”

Mstari wa 18 katika kitabu hichohicho pia maandiko yanasema: “Aendaye kwa unyoofu, ataokolewa, bali mkaidi wa njia zake ataanguka mara”.

Wananchi wengi hivi leo wanaamini katika nyanja tatu za kuwapeleka wanakotaka kwenda na kule wasikotaka ambazo ni dini, habari na siasa.

Wanawaamini viongozi wa dini, wanasiasa na waandishi wa habari kwa takribani kila wanachokisema.

Mtu makini akiwa ugenini, kisha akaona mti wenye matund hata kama yameiva hawezi kuyala mpaka awaulize wenyeji, kama matunda hayo yanaruhusiwa kuliwa ama la. Kama ataambiwa kuwa yana sumu kamwe hawezi kuyala.

Lakini kuna watu wenye pupa wakiona matunda, mradi anaamini yameiva papo hapo anaanza kuchuma na kisha kuyala, lakini mwisho wake hatimaye unakuwa ni kifo au kunusurika kufa.

Kwa kawaida baadhi ya waandishi wa habari kabla hatujaandika habari au makala zikiwemo za uchambuzi na kadhalikia, kwanza tunajiuliza kwamba ninataka nini? Shabaha yangu hasa ni ipi? Lengo langu ni lipi? Baada ya kujijibu maswali hayo ndipo sasa tunaanza kuandaa mpango kazi, kisha tunakwenda kuhoji au kusikiliza.

Kuna mkumbo ambao umeingia katika nchi yangu ya Tanzania ambapo, hivi leo kuna baadhi ya waandishi wa habari wameamua kufuata mkumbo katika kazi zao lakini bila ya kujua kwamba wanachocheza ni mchezo wasioufahamu.

Idadi kubwa ya waandishi wa habari ama vyombo vyao hapa nchini, vimeamua kwa makusudia au kwa kutokufahamu; kuiga mchezo ambao baadhi ya wenzao kule Rwanda mwaka 1994 waliucheza sana, kisha wakalipasua taifa lao kabla ya wao wenyewe kuja kupasuka “msamba”.

Bila shaka baadhi ya wasomaji mmeanza kuuakisi mchezo huo kuwa ni baadhi ya waandishi wa habari kuweka zaidi fikra zao kutaka kuuza magazeti yao, kusikilizwa kwa vyombo vyao au kutembelewa zaidi katika blogu zao kwa kuandika mara kwa mara kile kinachoitwa kuwa matamko ya viongozi wa dini.

Ikumbukwe kwamba mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda mwaka 1994, yalitokana na uchochezi mkubwa wa viongozi wa dini kwa kushirikiana na baadhi ya waandishi wa habari wa magazeti au watangazaji wa redio na kadhalika.

Kutokana na hali hiyo, nchi hiyo iliingia kwenye machafuko makubwa ya kihistoria na watu wasio na hatia wakauawa kikatili.

Bahati nzuri kabisa kwangu ni kwamba hata wale waliothibitika kuwa walishiriki kuchochea ghasia hizo kuna wengine pia hawakubakia salama, wale ambao ni pamoja na waandishi wa habari na viongozi wa dini na baadhi yao wamefungwa jela kwa miaka tofauti.

Hata hapa nchini hivi leo, habari zinaoitwa kuwa ni tamu kwa baadhi ya vyombo vya habari ni matamko ya viongozi wa dini mpaka unajiuliza: Hivi matamko haya ni mahubiri au mwandishi wa habari na chombo chake walikwenda na kumhoji kiongozi huyo wa dini wakiwa tayari na dhamira yao?

Jawabu linalopatikana ni kuwa idadi kubwa ya waandishi wa habari wanaoandika hicho kinachoitwa kuwa ni matamko ya viongozi wa dini, mara zote wanaandaa mpangokazi wa mahojiano na maswali ya kuuliza badala ya kuyapata kutokana na mahojiano kati yao.

Mchezo huo unachezwa na baadhi ya wanataaluma wa habari hapa nchini, wale wanaofikiria zaidi kuhusu mauzo ya magazeti yao badala ya hatari au hatma yetu sote kama taifa moja wakiwemo wakulima huku nyikani.

Sina tatizo na viongozi wa dini wala matamko yao, lakini siamini kabisa kwamba wao ni watakatifu na watenda mema kuliko Watanzania wote wasiokuwa viongozi wa madhehebu hayo ya dini.

Katika kashfa za uuzaji na usafirishaji wa dawa haramu za kulevya nchini ama ufisadi,  baadhi ya viongozi wa dini nao wanahusishwa, hivyo hicho ni kipimo cha kutosha kuonyesha kuwa miongoni mwao pia siyo safi.

Baadhi pia wanahusishwa katika masuala ya ubingwa wa kupiga ramli na kuamini ushirikina, ugoni kwa wake za watu ama waumini wao na hata uchafu mwingine.

Kamwe sitoi hukumu kuhusu mambo hayo, lakini ieleweke kuwa hata viongozi hao wa dini pia ni binadamu kama wengine. Tofauti pekee iliyopo ni kwamba wao wanafanya kazi au wamepata ajira katika taasisi za dini.

Baadhi ya nchi ambazo waandishi wa habari wanajua kuwa baadhi ya viongozi hao wa dini wanaweza kuleta machafuko kutokana na matamko yao, siku zote huwa nadra sana kuona habari na kile kinachoitwa matamko yao magazetini.

Kama kunakuwepo au zinaandikwa habari zao, mara zote huuwa ni zile ambazo tu zinahusu viongozi hao kuhubiri upendo, amani na mshikamano miongoni mwa waumini wao na taifa lao.

Katika hali hiyo, viongozi hao huwa wana mchango mkubwa kabisa katika ustawi wa taifa lolote duniani endapo watatumika vizuri kama watangulizi wao ambao ni pamoja na hayati Martin Luther King wa Marekani, Askofu Desmon Tutu wa Afrika Kusini na wengineo wengi.

Hatari ya matumizi mabaya ya mahojiano na viongozi hao kwa taifa ni kutoweka kwa amani. Hii ni kwa vile vyombo vya habari ndilo eneo pekee lililobaki ambalo bado linaaminika zaidi kwa wananchi hasa wa kada za kawaida ukiachilia mbali viongozi wa dini na siasa.

Ndiyo maana nawashauri waandishi wa habari nchini kuwa mwaka 2015, pamoja na mambo mengine uwe wa kutubu makosa. Unapaswa utumike kuliweka salama taifa hasa ikizingatia pia kwamba utakuwa wa uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani.

Naomba kila mwenye sikio anisikie na kuwafikiria walio nyuma yake, kushoto kwake na kulia kwake, kisha tusonge mbele.
Mungu bariki wanahabari, viongozi wa dini, viongozi wa Serikali, wakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara. Mungu ibariki Tanzania.

Mwandishi anapatikana kwa simu 0754 440749
Email. kalulunga2006@gmail.com

No comments: