Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Wednesday, August 10, 2016

CHANZO CHA UTATA WA SOKO LA MWANJELWA HIKI HAPA

 Sura ya soko jipya la MWANJELWA kama inavyoonyesha kwa juu wakati wa ujenzi wake ambapo mkapa sasa haijulikani ni lini litakamilika na lilitakiwa likamilike Desemba 2011.
Meneja wa mradi huo Bwana Mohamed Hasheed


Na Gordon Kalulunga, Mbeya 
VIJANA wengi wanapenda ujinga kuliko mambo ya msingi ndiyo maana utawasikia vijiweni wakisema ni bora wangezaliwa mbwa ulaya kuliko Afrika.

Hivi kijana wa kiume anayetamani kuwa mbwa akiambiwa aolewe na Mzungu atakataa?

Kijana wa namna hii au raia wan chi yeyoyte mwenye mawazo ya sampuli hii daima huwa namfananisha na mtu anayetembea kwa muda mrefu lakini hajui alipofika maana alikuwa akitembea kinyume nyume.

Ndivyo ilivyoanza kujengeka katika jamii yetu ya kitanzania kwa kupandikizwa mawazo mgando na baadhi ya wanasiasa wanapofanya ziara zao katika baadhi ya mikoa ambayo wao hawatoki kwa kusema kuwa Serikali haijafanya kitu. Hao wanawafananisha watanzania na mtu anayetembea kinyume nyume.

Mtu anayetembea kinyume nyume ni sawa na mtu anayetembea kwenda mbele huku akiwa amefungwa kitabaa cheusi usoni kwake ambapo hakika atakuwa anabahatisha anakoenda badala ya kuwa na uhakika na anakoenda.

Hali hiyo inatokana na kuamini mapandikizi ya ujinga ambapo kila mara mtu anaamini kuwa Serikali haifanyi kitu na mtu wa namna hiyo hata akila chakula huwa aamini kama ameshiba maana amepandikizwa roho ya kutojithamini wala kuthamini wengine.

Hakuna kitu kizuri au kibaya kama imani, mtu akiamini katika wema atakuwa mwema na mtu akiamini katika ubaya atakuwa mbaya.

Mfano mzuri ni kwamba, huku kwetu nyikani kuna mchungaji mmoja alikuwa akimwambia Bibi kizee mmoja kuwa akiwa na chembe ya imani mfano wa punje ndogo ya mchicha anaweza kuuambia mlima na miti ing’oke nayo itatii.

Bibi kizee huyo alilifurahia sana neno hilo la faraja hivyo kuna siku Mchungaji huyo alimtembelea tena nyumbani kwake na kumweleza maneno hayo hayo.

Ndipo bibi huyo akamwambia Mchungaji huyo akisema ‘’Mchungaji neno hili la imani umenifundisha sana na mimi naamini kuwa wewe una imani kubwa kuliko mimi na hapa kwangu kuna kilima kinanizuia kuota jua naomba ukiambie king’oke’’.

Mchungaji kusikia maneno hayo alimwambia kuwa maneno hayo yana maana nyingi ikiwemo kutumbukiza imani kwenye matatizo mbalimbali na Mungu anaweza kuonesha nguvu zake na kutatua.

Bibi huyo alisema kuwa kwa imani yake pamoja na mchungaji waombe pamoja na kuuambia mlima ule ung’oke ndani ya siku saba.

Wakaomba kwa pamoja huku wakinyosha vidole vyao kwenye mlima huo kisha kuendelea na mambo mengine.

Ndani ya siku saba Serikali ikawa na ujenzi wa barabara sehemu hivyo katika uchunguzi wake ikaonekana udogo wa kile kilima ulikuwa mzuri hivyo siku ya saba serikali ikaaza kuchota udongo wa kilima hicho na hatimaye kilima kikaondoka na Bibi akawa anapata mwanga wa jua bila kipingamizi.

Bila shaka unaona nguvu ya imani. Vivyo hivyo mtu anayeamini au kuaminishwa kuwa serikali haijafanya lolote ataendelea kuona hivyo hata kama atajengewa barabara mpaka nyumbani kwake na yule anayeona serikali inandelea kufanya maendeleo hata yeye atajibidiisha kufanya kazi za kimaendeleo.

Lakini mbali na jambo hilo, kuna uzembe kama si makusudi ya watendaji wa serikali kutoweza kutimiza wajibu wao kikamilifu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali katika Halmshauri zetu.

Nimekuwa nikitolea mfano wa suala la miradi ambayo inafunguliwa na mwenge kila mwaka, miradi hiyo karibia yote inakuwa chini ya kiwango huku watendaji hao wakifanya hadaa na dhihaka kwa watanzania kwa kusoma risala tamu mbele ya viongozi wanaokimbiza mwenge na mbele ya kamera za Luninga kana kwamba miradi hiyo ni nuru kwa watanzania.

Nasema ni dhihaka kwasababu viongozi wakuu akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na waziri mkuu wamekuwa wakisikika na kuuambia umma kuwa serikali imetekeleza hiki na kile kumbe wamedanganywa.

Niliwahi kueleza wasiwasi wa kutokamilika kwa wakati soko jipya la kisasa la Mwanjelwa Jijini Mbeya linalojengwa na mkandarasi Tanzania Building Works (TBW) baada ya kuteketea Desemba, 2006 lakini nikapuuzwa na sasa yametokea.

Soko hilo limeelezwa kuwa halina ubora uliotarajiwa na kufadhiliwa na benki ya CRDB.

Uchunguzi uliofanywa, umebaini kuwa soko hilo lina nyufa zilizotokana na ujenzi ulio chini ya kiwango kisha kuzibwa kwa saruji ili kuficha ubovu huo kabla ya kukabidhiwa.

Kutokana na soko hilo kutojengwa kwa ubora uliokuwa ukitakiwa, Mafundi wa soko hilo wanasema lawama za soko hilo kutokuwa bora zinapaswa kuwaendea wahandisi wa Serikali wa Jiji la Mbeya ambao mara kwa mara wamekuwa wakifika eneo la ujenzi na kuishia ofisi za mkandarasi kisha kuondoka.


Wanasema kuwa uozo huo upo tangu soko linaanza kujengwa lakini hakuna kiongozi wa Serikali ambaye amewahi kuwauliza hata mafundi kwa siri ili kujua uhalisia wa ujenzi wa soko lenyewe.


Kutokana na uzalendo wa mafundi hao, waliamua kumwandikia barua ya uhalisia wa soko hilo Katibu mkuu wa tawala za mikoa na Serikali za mitaa ‘’Tamisemi’’ wakieleza kuwa soko hilo halina ubora na endapo Serikali italipokea maafa yatakayotokea lawama ziwe juu ya Serikali.


Barua hizo ambazo nakala zake zipo, zimeeleza kuwa kama Serikali ni sikivu itafute wataalam wake na kukagua kwa kuchimbua Msingi wa Soko ambapo soko hilo halina mhimili imara wa kuunganisha jengo zima (Ring Bim) ili kulifanya kuwa imara.

Mmoja wa mafundi hao anasema wakati wa kufanya jambo hilo yeye na mafundi wenzake wawepo kwa ajili ya ushahidi pamoja na waandishi wa habari ili kusiwepo hali ya kulindana na mazingira ya Rushwa kwa watendaji hao wa Serikali na kama kiunganishi hicho kitakutwa, Serikali iwapeleke mafundi hao mahakamani.


Barua moja ambayo imeandikwa na fundi Saimon Uledi ambaye ni mmoja wa mafundi waanzilishi wa soko hilo, kwenda Tamisemi iliandikwa June 6, 2011 na kueleza undani wa kutokuwa na ubora wa ujenzi wa soko hilo na kuhofia kuwa endapo kutatokea tetemeko basi wananchi watakaotumia soko hilo watapata maafa makubwa.

‘’Nakuomba Katibu Mkuu fuatilia ujenzi wa soko la Mwanjelwa kuanzia tofali la kwanza chini ya Ardhi ili upate uhakika kama Ring Bim lipo, Maslahi ya wafanyakazi, mikataba mibovu isiyo na picha na ubora wa jengo kwa ujumla’’ imesema moja ya haya ya barua hiyo.

Kutokana na barua hiyo, Tamisemi iliamua kumwandikia Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya barua yenye kumbukumbu namba MCC/M.50/17/VOL II/226 ya Julai 7,2011 ili aweze kuzitolea ufafanuzi tuhuma hizo na nakala yake ikaenda kwa Katibu tawala wa mkoa wa Mbeya.

Mbali na barua hiyo, Tamisemi ilimwandikia barua katibu tawala wa mkoa wa Mbeya Septemba 23,2011 yenye kichwa cha barua Ujenzi wa  soko la Mwanjelwa Mbeya kutokuwa na ubora ikimweleza kuwa kuna malalamiko ya soko hilo kuwa na ujenzi hafifu ikiwa ni pamoja na kutokuwa na mkanda wa chini (Ground beam) kwenye jengo hilo.

‘’ Kwa kuwa jengo hilo ni kwa matumizi ya umma na dhamana ya ujenzi wake unasimamiwa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa, yaani Halmashauri ya  Jiji la Mbeya, OWM-TAMISEMI ilifanya mawasiliano na Mamlaka hiyo ili kupata taarifa za awali na vielelezo vya kiufundi ili kujiridhisha na uwepo wa ‘’ground beam’’kwenye michoro ya usanifu ‘’architectural’’ na mhimili ‘’structural.

‘’Halmashauri ya jiji la Mbeya iliwasilisha maelezo kuwa malalamiko hayo sio ya kweli na kwamba ujenzi umezingatia taratibu zote na viwango vya ubora vinazingatiwa’’ imesema barua hiyo yenye kumbukumbu namba HA.78/225/01/07/13

Kutokana na kile kilichoonekana kuwa Serikali inachelewa kuchukua maamuzi dhidi ya wahusika wa ujenzi wa soko hilo licha ya kuwepo ushahidi wa wazi, mafundi hao walimwandikia barua katibu mkuu wa ofisi ya Waziri Mkuu Desemba 1, 2011 wakieleza kuwa endapo wakikuta mhimili wa jengo hilo wapo tayari kufungwa, lakini hawajapatiwa majibu.

Mafundi hao baada ya kuona barua zao zinapuuzwa, waliamua kutoa taarifa katika ofisi za Jeshi la polisi mkoa wa Mbeya kwa ajili ya usalama wao ambapo taarifa kutoka ndani ya jeshi hilo zimethibitisha kuwepo kwa taarifa hiyo na kwamba baadhi ya vigogo wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya tayari wamehojiwa.

Ajabu katika sakata hilo Jiji la Mbeya kwa kushirikiana na mjenzi, waliamua kupeleka waandishi wa habari na kuwapatia posho 20,000 na mkandarasi akatoa 80,000 kwa kila mmoja ili kuziba kashifa hiyo na hapa ndiyo maana nasema kuwa tunatembelea lakini hatujui tulipofika sawa na mwendo kinyume nyume.
 
Hongera Mkuu wa Mkoa Amos Gabriel Makalla na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa kwa hapo mlipoanzia.
0765 615858
BARUA PEPE.kalulunga2006@gmail.com

No comments: