Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Wednesday, August 10, 2016

MBEYA; Mlundikano wa Kodi, chanzo cha migogoro MwanjelwaNA GORDON KALULUNGA

MZIGO wa kodi kwa baadhi ya wafanyabiashara wa soko la Sido na Mwanjelwa Jijini Mbeya, umetajwa kuwa ni moja ya chanzo cha vurumai za mara kwa mara kati yao na Serikali, imebainika

Hivi karibuni, baadhi ya wafanyabiashara wa mitumba katika Soko la Sido, waligoma kutoa ushuru hadi hapo uongozi wa halmashauri ya jiji utakapowaondoa baadhi ya wafanyabiashara wadogo maarufu kwa jina la machinga walioweka meza za bidhaa nje ya soko hilo kinyume cha maelekezo ya uongozi huo.

Imebainika kwamba mbali na kero hiyo ya wamachinga, wafanyabiashara wa mitumba wanakabiliwa na mzigo wa kodi zisizopungua 15.

Uchunguzi umebaini kwamba miongoni mwa kodi hizo na kiasi kinachotakiwa kulipwa ni pamoja na kodi ya leseni ya biashara (Sh 50,000-300,000) kulingana na ukubwa wa biashara, kodi ya stoo (Sh 50,000-kuendelea), kodi ya taka kwa mwezi (60,000-240,000) kulingana na ukubwa wa biashara, kodi ya zima moto (Sh 40,000-200,000) kulingana na ukubwa wa biashara, kodi ya TFDA (Sh 20,000-150, 000) kulingana na ukubwa wa biashara na ushuru wa kila siku Sh 300-600.

Aidha, zipo pia kodi ya bango la biashara (Sh 700,000-100,000) kulingana na ukubwa wa biashara, ada ya maombi ya bango (Sh 100,000), kodi ya jina la biashara kwenye duka (kila herufi Sh 1,000), kodi ya huduma (asilimia 0.3 ya mapato ya kila mwezi), kodi ya mizani (Sh 7,000-15,000), kupima afya kwa mtu aliyeko dukani (Sh 10,000) kwa msimu mmoja ambapo wanapima kwa misimu minne kwa mwaka, kodi za ukarabati wa vibanda (Sh 10,000), choo (Sh 21,000) kwa mwezi pamoja na kodi za vyumba na maegesho.

Hata hivyo, utaratibu unaotumika katika ukusanyaji wa kodi hizo, unafananishwa na ukusanyaji wa vilabu vya pombe za kienyeji kutokana na kila mmoja au kila idara kufuata kodi zake zinazoihusu idara husika, badala ya kodi hizo kulipwa moja kwa moja benki katika akaunti ya kila idara.

Kwa mujibu wa wadadisi wa mambo, utaratibu huo wa ulipaji wa kodi umegubikwa na vishawishi vingi vya rushwa kwa watumishi wa umma wasiokuwa waaminifu katika vitengo vya ukusanyaji wa kodi hizo.

Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara ambao hawakutaka kutaja majina yao, wamesema jiji la Mbeya linapaswa kujifunza kutoka Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), ambapo wameweka utaratibu wa kila mfanyabiashara kupeleka kodi kupitia akaunti ya mamlaka, tofauti na awali ambapo watumishi wa mamlaka hiyo walikuwa wakifuatilia kodi hizo madukani hali ambayo ilikuwa ikisababisha mamlaka kukosa mapato yake.

Mwenyekiti wa soko hilo, Charles White Syonga, alipoulizwa kuhusu kodi hizo, amekiri kuwepo kwa kodi hizo ambazo amesema tayari wamewasilisha malalamiko yao katika ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya tangu mwaka jana 2015.

No comments: