Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Friday, August 26, 2016

NEW IMARA SECURITY; KAMPUNI YA KIZALENDO INAYOAMINIWA NA TAASISI NYETI


 Mkurugenzi Mtendaji wa New Imara Security, Essau Kamwela.

Na Gordon Kalulunga, Mbeya

KATIKA nchi ya Afrika kusini, makampuni ya ulinzi binafsi ndiyo yanayoongoza kutoa huduma ya ulinzi na kutangaza uhalifu unaojitokeza katikavyombo vya habari.

Shabaha ya kufanya hivyo ni kutaka jamii iwe makini na kuweza kuajiri walinzi wenye taaluma katika makazi yao, taasisi na hata katika biashara binafsi.

Hapa nchini elimu hiyo bado haijafikia wananchi wengi pamoja na baadhi ya viongozi wa makampuni ya ulinzi, ingawa tayari baadhi ya watu hasa wenye vipato vya kati wameendelea kuajiri walinzi lakini wengi wao wameajiri walinzi katika maeneo yao ya biashara.

 Moja ya kampuni za kizalendo hapa nchini inayotoa huduma za ulinzi ni New Imara Security Company Ltd (NISCO) yenye makao yake makuu Jijini Mbeya.

Kampuni hiyo chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mtendaji Essau Kamwela, imeamua kuleta mapinduzi ya kiusalama na kuiaminisha jamii kwa vitendo kuwa kampuni binafsi ya ulinzi ikiwa na askari wenye taaluma, ni chachu katika usalama wa jamii na mali zao kwa ushirikiano na vyombo vingine vya dola.

Mkurugenzi wa fedha wa kampuni hiyo, Aliko Kamwela, anasema kuwa kampuni hiyo imeanza kutoa huduma mwaka 2001 mkoani Mbeya, lakini kwa sasa imeenea katika mikoa zaidi ya kumi na mbili.

Anasema mpaka sasa kutokana na uaminifu wa askari wao, wanatoa huduma ya ulinzi katika taasisi za serikali na watu binafsi ikiwemo Wizara ya fedha kitengo cha Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) na idara za wizara zingine.

‘’Tunatoa huduma TRA, chuo kikuu cha Sayansi na teknolojia(MUST), Mzumbe, Veta, Kiwira Coal Mine Mbeya, Bandari Mtwara, Mamlaka ya usafirishaji wa anga (TCAA), TRA mikoa ya Mbeya, Lindi na Mtwara, UDSM, St. John University na TIA, Dar es Salaam’’ anasema Aliko Kamwela.

Anasema mbali na malindo hayo, pia wanatoa huduma za ulinzi katika maeneo mbalimbali nchini hasa katika mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Iringa, Mwanza, Rukwa, Njombe, Mtwara, Lindi, Dodoma, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.

Anasema ubora wa huduma zao zinatokana na vitu vitatu vikubwa, ikiwemo uaminifu, kuajiri askari waliohitimu mafunzo na kuwa na vifaa vya kisasa vinavyohitajika katika kazi ya ulinzi.

‘’Tuna askari wakakamavu wenye mafunzo, mawasiliano ya redio call, CCTV Camera, mfumo wa Alarm, bunduki za kisasa, magari ya patrol na vifaa vingine vizuri’’ anaeleza mkurugenzi huyo wa fedha.

Meneja wa kampuni hiyo, Rajab Sijaona Mengele, anasema licha ya mafanikio ya kampuni hiyo, lakini pia wanakabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya wateja kutokuwa waaminifu kwenye maeneo yao ya kazi.

‘’Kuna baadhi ya wateja ambao wanakuwa siyo waaminifu ambapo wanaacha milango yao wazi au kufunga makufuli tofauti hasa wale ambao tunakuwa tunawadai kwa zaidi ya miezi miwili, na ikifika asubuhi anasema kuwa kaibiwa, lengo likiwa ni kuibambika makosa kampuni ili kukwepa kulipa’’ anasema Mengele.

Anasema kwamba changamoto zingine ni baadhi ya wahalifu ambao wanatumia funguo za bandia kuiba(Master Key), wanawashawishi askari wanapokuwa kwenye malindo ili waibe na kuwaahidi fedha nyingi.

‘’Jambo hili linatokea mahala pengi ambapo utakuta mhalifu anamwambia askari kuwa watampatia zaidi ya Shilingi Milioni Moja ili aachie lindo!’’ anasema Rajab.

Anaongeza kuwa kuna baadhi ya askari ambao ni waaminifu, wanatoa taarifa haraka yanapojitokeza mambo kama hayo, kisha uongozi unachukua hatua mara moja ya kukabiliana na vitendo hivyo ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na vyombo vingine vya dola hasa jeshi la polisi.
 

 Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo ya New Imara Secury Ltd, Essau Kamwela, anasema kuwa, katika suala la ajira, wanaajiri askari wazalendo kwa kufuata vigezo vinavyokubalika na nchi na mpaka sasa wana askari wengi ambapo kwa mkoa wa Lindi wanao askari 120, Mtwara zaidi ya 150 na mikoa mingine.

‘’Hivi karibuni tulitangaza ajira 100 kwa askari wenye mafunzo ya Kijeshi wakiwemo waliofuzu mafunzo ya Skauti kwa watanzania ambao walikuwa tayari kufanya kazi katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara’’ alisema Mkurugenzi huyo.


Alibainisha kuwa, mpaka sasa, wanaendelea kutoa ajira kwa askari ambao wapo tayari na wale wanaokuwa kwenye mafunzoni hasa ya mgambo, wanapeleka maombi na usajili unafanyika siku wanayohitimu mafunzo.

‘’Waliopitia mafunzo ya mgambo na kuhitaji ajira katika kampuni yetu, wanapaswa kuendelea kujitokeza na wale wote waliopitia mafunzo ya Kijeshi na kustaafu katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), JKT, Polisi, Magereza na waliohitimu mafunzo ya Skauti tunawapa ajira’’.anasema Kamwela.

Anaiomba serikali kuwa karibu na sekta hiyo binafsi ambayo ndiyo inaongoza nchini kutoa ajira kwa watanzania.

“Kwa sasa hapa nchini makampuni binafsi ndiyo yanayoongoza kwa kulinda usalama wa raia na mali zao mfano katika bandari, nyumba binafsi, Hoteli na kampuni zinapoanza kujenga viwanda ama barabara lazima wahitaji ulinzi wa askari wa makampuni binafsi’’ anasema.

Anasema kuwa licha ya kuendelea kufanya hivyo na kulipa kodi serikalini, lakini wanakabiliwa na changamoto ya kutopata mikopo katika vyombo vya fedha ili kuboresha huduma kwa kununua pikipiki za doria, magari ya kisasa zaidi, mitambo ya ulinzi na kuongeza silaha za kisasa.

Mkurugenzi huyo anatanabaisha kuwa lengo ni kuondoa tatizo la ajira kwa askari wastaafu na wenye taaluma hiyo ya kijeshi ambao watasaidia katika suala zima la ulinzi shirikishi na kujiongezea vipato vyao na familia.

Sanjari na hayo anatoa wito kwa wadau wa kampuni za ulinzi kuwa wanapopelekewa askari ambao wanamashaka nao, wanatakiwa kutoa taarifa kwa viongozi wa makampuni husika wanayoingia nayo mikataba ili kubadilishiwa walinzi kwa ajili ya usalama wa mali zao.

Kamwela ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa chama cha wamiliki wa makampuni ya ulinzi Tanzania, Tanzania Security Industry Association (TSIA) kanda ya Nyanda za juu kusini, anasema jamii inapaswa kubadili fikra na dhana iliyojengeka ya kuwadharau askari wanaozitumikia kampuni hizo kwasababu walinzi hao bado ni askari wakakamavu sawa na walioko Serikalini.

Mwandishi wa makala haya, anapatikana kwa simu 0754 440740. Barua pepe; kalulunga2006@gmail.com

No comments: