Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Monday, September 05, 2016

SAUTI KUTOKA NYIKANI; RC Mwenye kasi kama ya Rais Magufuli

NA, GORDON KALULUNGA


KATI ya mikoa ambayo kuiongoza ni migumu ni pamoja na mkoa wa Mbeya.

Mkoa huo unatajwa kuwa ni tanuru la uongozi ambapo kiongozi yeyote wa serikali akifanya vizuri Mbeya, basi cheo kinapanda na akifanya vibaya historia yake huishia hapo.

Ipo mifano mingi ya watu waliofanya vizuri Mbeya na vyeo vikapnda na wengine waliofanya vibaya historia zao zilifukiwa Mbeya.

Baadhi ya waliofanya vizuri mkoani Mbeya ni pamoja na aliyewahi kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, Said Mwema, Kamanda kanda maalum Dar es Salaam, Suleiman Kova, DCI Diwani Athuman, kaimu DPP Ayub Mwenda, Ezekiel Mgeni (Obama), Zelothe Stephen na wengine wengi.

Viongozi hao kilichowapandisha ni kutokuwa na utendaji wa kikoloni. Walipanda vyeo kutokana na uchapa kazi wao usio na dharau na upendo wao mkubwa kwa wananchi.

Upendo wao kwa wananchi wa rika zote bila kujali nyadhifa, waliweza kuwa viongozi wanaopokea taarifa nyingi za chini kabisa na za juu kutoka kwa wananchi kwasababu ya usiri wao na heshima zao kwa watu.

Kwa sasa nyota inawaka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, ambaye amekuwa kimbilio la wananchi hasa wanyonge ambao walikata tama na kuamini kuwa viongozi ni miungu watu.


Makalla ameamua kuendana na kasi ya anayemwakilisha yaani Rais Dkt. John Pomba Magufuli kwa kujali zaidi wanyonge walionyonywa kwa muda mrefu na baadhi ya watumishi wa serikali.

Moja ya jambo ambalo tangu amefika mkoani Mbeya, analishughulikia kwa karibu ni suala la soko la kisasa la Mwanjelwa ambalo limemalizika kujengwa hivi karibuni na kugharimu fedha ambazo zingine hata hazisemeki na hatimaye kumlazimu Waziri Mkuu Kasim Majaliwa kutolea macho.

Na tume ya Mkuu wa Mkoa katika taarifa zake inaonyesha kuwa  kuna baadhi ya viongozi wa idara za serikali mkoani Mbeya, wamegawana vyumba vya soko hilo la Mwanjelwa na kuwaacha baadhi ya wahanga ambao ndiyo walitakiwa kupewa kipaumbele cha vyumba hivyo.

“Baada ya kunusa harufu ya ufisadi na kuomba taarifa ya ujenzi, walinidanganya kuwa walijenga kwa Bilioni 23 na nilipoteua kamati kwa kuhusisha vyombo vya dola ikabainika kuwa soko limejengwa kwa Bilioni 26”…

“Siku niliyoenda soko la mwanjelwa, maana kuna baadhi ya viongozi wanaohusika walitoka katika kikao changu na ilikuwa meseji kuwa anayeingia anakanyaga mikono yetu” anasema Makalla.

Anasema baada ya awali kupata taarifa za Jiji hilo la Mbeya ambalo linaongozwa na Chadema, alibaini kuwa taarifa za Jiji hazikuwa sahihi na haikuzingatiwa uanzishwaji wa ujenzi wa soko lile na kwamba mhanga ndiye aliyetakiwa kupewa kipaumbele badala yake wahanga wamebaki mguu ndani na mguu nje katika eneo la Sido.

Baada ya kuchukua maamuzi ya kutembelea soko hilo na kunusa harufu ya ufisadi, anasema alidhani atapewa pongezi na hasa madiwani, lakini ndiyo walikuwa wa kwanza kutoka kwenye kikao na kukimbia.

“Sasa nataka niwahakikishie kuwa taarifa ya awali zinaonyesha kuwa kuna fedha Milioni 489 zinatoka akaunti Ya Jiji kulipwa CRDB, ndiyo maana Waziri Mkuu aliniagiza kuwa harakisha suala hili maana CRDB hazionekani na alitoa siku tatu” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

Anaeleza kwamba, kamati aliyoiunda baada ya agizo la Waziri Mkuu, imebaini kuwa fedha hizo zimelipwa CRDB hivyo CAG na watu wa mifumo wa Benki kuu watapiga kambi pale ili kubaini matatizo ya pale CRDB kubaini ukweli wa fedha hizo zilikoenda na kwamba ameshusha bei vyumba hivyo kutoka pango la Shilingi 500,000/= mpaka 350,000/= na 250,000/=

“Vyumba pale wamegawana viongozi na nitawataja hapo baadae. Kuna watu wana vyumba vitano wengine kumi na wiki ijayo nitakuja hapa kuwanyang’anya vyumba na kuwapa watu wengine” alisema Makala.

Kuhusu watu wanaouza bidhaa barabarani pembeni mwa soko la Mwanjelwa, tayari ameamuru wapatiwe nafasi ndani ya soko hilo.

Sauti ya nyikani inamnong’oneza Amos Makalla kuwa Jiji la Mbeya pia linalalamikiwa na baadhi ya wafanyabiashara katika soko la Sido kuwa wanalipishwa kodi zaidi ya 15.

Uchunguzi wa watu wa nyikani umebaini kuwa, miongoni mwa kodi hizo na kiasi kinachotakiwa kulipwa ni pamoja na kodi ya leseni ya biashara (Sh 50,000-300,000) kulingana na ukubwa wa biashara, kodi ya stoo (Sh 50,000-kuendelea), kodi ya taka kwa mwezi (60,000-240,000) kulingana na ukubwa wa biashara, kodi ya zima moto (Sh 40,000-200,000) kulingana na ukubwa wa biashara, kodi ya TFDA (Sh 20,000-150, 000) kulingana na ukubwa wa biashara na ushuru wa kila siku Sh 300-600.

Aidha, zipo pia kodi ya bango la biashara (Sh 700,000-100,000) kulingana na ukubwa wa biashara, ada ya maombi ya bango (Sh 100,000), kodi ya jina la biashara kwenye duka (kila herufi Sh 1,000), kodi ya huduma (asilimia 0.3 ya mapato ya kila mwezi), kodi ya mizani (Sh 7,000-15,000), kupima afya kwa mtu aliyeko dukani (Sh 10,000) kwa msimu mmoja ambapo wanapima kwa misimu minne kwa mwaka, kodi za ukarabati wa vibanda (Sh 10,000), choo (Sh 21,000) kwa mwezi pamoja na kodi za vyumba na maegesho.

Hata hivyo, utaratibu unaotumika katika ukusanyaji wa kodi hizo, unafananishwa na ukusanyaji wa vilabu vya pombe za kienyeji kutokana na kila mmoja au kila idara kufuata kodi zake zinazoihusu idara husika, badala ya kodi hizo kulipwa moja kwa moja benki katika akaunti ya kila idara.

Kwa mujibu wa wadadisi wa mambo, utaratibu huo wa ulipaji wa kodi umegubikwa na vishawishi vingi vya rushwa kwa watumishi wa umma wasiokuwa waaminifu katika vitengo vya ukusanyaji wa kodi hizo.

Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara ambao hawakutaka kutaja majina yao, wamesema jiji la Mbeya linapaswa kujifunza kutoka Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), ambapo wameweka utaratibu wa kila mfanyabiashara kupeleka kodi kupitia akaunti ya mamlaka, tofauti na awali ambapo watumishi wa mamlaka hiyo walikuwa wakifuatilia kodi hizo madukani hali ambayo ilikuwa ikisababisha mamlaka kukosa mapato yake.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa simu 0754 440 749
EMAIL; kalulunga2006@gmail.com

  WADHAMINI WA BLOG HII NI STEMAN ENTERPRISES

No comments: