Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Wednesday, October 05, 2016

TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KWA VYOMBO VYA HABARI “PRESS RELEASE” TAREHE 04.10.2016. Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu. Mafanikio yaliyopatikana katika Misako ni kama ifuatavyo:-

KUPATIKANA NA BHANGI.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mtu mmoja mkazi wa Ilemi Jijini Mbeya aliyefahamika kwa jina la FRANK EDSON [20] akiwa na dawa ya kulevya aina ya Bhangi yenye uzito wa Gram 30.

Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 03.10.2016 majira ya saa 10:00 asubuhi katika msako uliofanyika huko eneo la Ilemi, Kata ya Ilemi, Tarafa ya  Sisimba, Jiji na Mkoa wa Mbeya.

Aidha katika msako mwingine uliofanyika mnamo tarehe 03.10.2016 majira ya saa 10:00 asubuhi huko Kabwe, Kata ya Ruanda, Tarafa  ya  Iyunga, Jiji na Mkoa wa Mbeya, Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la MOSES MWANGOKA [17] mkazi wa Ilolo Jijini Mbeya anashikiliwa na Jeshi la Polisi akiwa na dawa ya kulevya aina ya Bhangi yenye uzito wa Gram 15.

Watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na matukio ya uhalifu pamoja na wahalifu. Jitihada zinaendelea kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha Mkoa wetu unakuwa mahala salama. Kumekuwa na tukio 01 la wizi wa mtoto kama ifuatavyo:-


WIZI WA MTOTO MCHANGA.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mwanamke mmoja Mkazi wa Kijiji cha Mchangani aliyefahamika kwa jina la MODE BARNABA kwa kosa la wizi wa mtoto mchanga aitwaye PETER BELINO mwenye umri wa miezi mitatu.

Tukio hilo limetokea mnamo tarehe 02.10.2016 majira ya saa 10:00 asubuhi huko katika Kijiji cha Ndaga, Kata ya Ndanto, Tarafa ya Ukukwe, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya.

Inadaiwa kuwa mama mzazi wa mtoto huyo aitwaye ANNA BELINO FABIAN [25] Mkazi wa Ndaga wakati wa tukio hilo alikuwa anasukwa nywele nyumbani kwake na ndipo mtuhumiwa aliomba amshike mtoto na kisha kutoweka nae.

Baada ya mama mzazi kutoa taarifa Polisi, msako mkali ulifanyika na Mtuhumiwa alikamatwa majira ya saa 12:00 mchana akiwa na mtoto huyo eneo la Stendi kijiji cha Mchangani akiwa katika harakati za kupanda Gari kuelekea Mbeya Mjini. Mtuhumiwa amefikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Wilaya ya Rungwe tarehe 04.10.2016 na kesi imetajwa kusikilizwa tarehe 18.10.2016.


WITO:

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishna wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa wazazi na walezi kuwa makini na watoto wao ikiwa ni pamoja na kuweka uangalizi wa kutosha ili kuepuka vitendo vya wizi wa watoto. Aidha anatoa wito kwa jamii kushirikiana na Jeshi la Polisi hasa kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuzuia vitendo hivyo.

                                                
                                                Imesainiwa na:
[DHAHIRI A. KIDAVASHARI - DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

No comments: