Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Saturday, October 29, 2016

TFDA yadaiwa kukwamisha ujenzi viwanda vidogoMjasiriamali Ivan Kibona akionesha bidhaa zake kwa mwandishi wa habari.

*Wawekezaji wazawa waijia juu
*Wasema inapunguza kasi ya Magufuli
*Wao wasisitiza kutotoa leseni za biashara

Na Gordon Kalulunga

Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) Kanda ya Nyanda za juu kusini, inatuhumiwa kukwamisha juhudi za Rais John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa za kujenga uchumi wa viwanda.

Tuhuma hizo zimetolewa na wawekezaji wazawa ambao wamewataka viongozi hao kuitupia macho mamlaka hiyo ambayo wamedai imekuwa ikiwakatalia kusajili bidhaa zao hata kama zimeruhusiwa na TBS.

Wakiongea na mwandishi wa habari hizi katika mahojiano maalum baadhi ya wawekezaji wazawa wenye viwanda vidogo mkoani Mbeya wamesema kuwa kitendo wanachofanyiwa na TFDA kinawakatisha tamaa hivyo kumuomba Rais Magufuli kuingilia kati tatizo hilo.

Mjasiriamali na mbunifu wa kusindika vinywaji aina ya (Wine) na vyakula katika wilaya ya Mbeya, Sarh Kalinga mwenye kampuni iitwayo Mama Neema Food Product, yenye namba ya usajili BRELA 193265, anasema kufikia maendeleo ya viwanda kama ilivyo ndoto ya Rais Magufuli ni kazi kubwa ikiwa mamlaka kama TFDA hazitajua umuhimu wa maendeleo ya viwanda.

Mjasiramali huyo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa wasindikaji bidhaa katika Halmashauri hiyo anasema kuwa changamoto kwa wawekezaji wadogo ni kubwa katika mambo mawili anayoyataja kuwa ni soko la uhakika na upimaji wa bidhaa kupitia TFDA.

“TFDA wanasema ili kupima bidhaa zetu lazima tuwe na kiwanda, sasa sijui maandazi yanatengenezwa kwenye viwanda gani! Sisi wenye mitambo hiyo midogo ya kusindikia hatuna fedha za kujenga majengo makubwa ya viwanda. Hivyo tutaendelea kutengeneza bidhaa na kuzisambaza maana hakuna namna,” alisema Mkurugenzi huyo.

Alisema jambo la kushangaza ni kwamba kuna bidhaa ambazo hazifai katika soko zinazotengenezwa na wawekezaji wakubwa ambao si raia wa Tanzania, zikiwemo nazi za maji na soda zinazowekwa harufu za machungwa wakati si halisi, lakini TFDA hawazigusi bali wanachachamaa na bidhaa za wawekezaji wanaotaka kuibuka ambazo zinatokana na malighafi halisi zinazopatikana kutoka kwa wakulima wa ndani ya nchi.


Mjasiriamali Sarah Kalinga

“Watu wengi jijini Dar es Salaam wenye viwanda vidogo wanasindikia majumbani na bidhaa zao zinapimwa na kuruhusiwa sokoni ila kanda yetu ya Nyanda za juu kusini hatujajua kuna shida gani. Tumeazimia kuendelea kuzalisha na bidhaa zetu na kuziingiza sokoni maana hatuwezi kujipatia vipato kwa njia ya kujiuza..”

Anaeleza kwamba kwa sasa wanajiandaa kwenda kupima na kusajili bidhaa zao nchini Kenya ambapo wakipata vibali bidhaa zao vinaruhusiwa kuuzwa katika soko la Afrika Mashariki na kati bila vikwazo.

“TFDA waondolewe huku kwenye usindikaji wabaki na kukagua dawa. Kuhusu kodi tuna mzigo wa kodi na kutakiwa kulipia leseni Halmashauri, Wizara ya Afya, Osha, Brela, TRA, Umeme, Maji, TBS na TFDA” alisema Sarah.

Wasindikaji na wakufunzi wa masuala ya usindikaji kupitia SIDO Mbeya, Rehema Msina na Anitha Mwasajone, wanasema changamoto ni nyingi ikiwemo kulipia upimwaji wa bidhaa zao kwa dola ya kimarekani ambazo hufikia kiasi cha Shilingi 600,000.

“Nafuu TBS wanapima bidhaa zetu kwa Tsh 50,000 tofauti na hawa TFDA ambao sisi tayari tumepata vibali vyao lakini baada ya kupitia changamoto mbalimbali ikiwemo ucheleweshaji wa upimwaji bidhaa huku mitaji ikiwa ni moja ya kikwazo kikubwa kwa wajasiriamali. Pia kuhusu kuwa na jengo kwa mjasiriamali ni kazi kubwa kwasababu wengi ni wapangaji” walisema wajasiriamali hao ambao wapo eneo la Nane Nane Uyole.

Aidha. walieleza kuwa changamoto nyingine ambayo ipo kwa upande wa mikopo ni wajasiriamali kutoaminiana na kwa upande wa serikali hasa mikopo ya vijana na wanawake kutoka katika Halmashauri na utengwaji wa maeneo ya ujenzi wa viwanda vidogo utekelezwaji wake ni hafifu.

Kuhusu ubora wa Malighafi wanasema kuna tatizo kubwa katika kuelekea mafanikio ya biashara za wajasiriamali ambao wanategemea malighafi za hapa nchini kwasababu wakulima wengi wanatumia mbolea na madawa ambayo bidhaa zikipimwa kimataifa hukosa ubora huku ubora wa vifungashio nao ukiwa unatia shaka na hapa watu wa TBS wanapaswa kutazamwa.

Mwekezaji mwingine mzawa jijini Mbeya, Ivan Kibona, ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya Ivan Products inayozalisha bidhaa za viwandani zikiwemo sabuni na mafuta ya kupakaa mwilini.

Mbali na mambo mengine, alipohojiwa kuhusu changamoto wazipatazo wawekezaji wazawa waliojikita katika utengenezaji wa bidhaa za viwandani zitokanazo na malighafi za hapa nchini, alisema Mamlaka hiyo isipotazamwa upya, itakwamisha juhudi za serikali kufikia malengo ya ujenzi wa viwanda.

"Tangu Rais Magufuli atangaze kuhusu kuinua uchumi wa Watanzania kupitia viwanda imekuwa faraja kubwa kwetu wawekezaji wa ndani na tayari soko limeanza kupatikana ndani tofauti na awali ambapo masoko yalikuwa nchini Kenya, DRC na Zambia," alisema Mkurugenzi huyo.

"Naomba, tena unirekodi na uwafikishie wakubwa wajue kuwa serikali ina nia njema na wawekezaji wazawa lakini TFDA haina nia njema kwetu”.

“Wanakuja tu kutukamata na tukipeleka maombi ya kupimiwa bidhaa zetu wanachukua pesa na kutukatalia vibali huku wakitutaka tuendelee kutuma maombi ya kupimwa bidhaa zetu, wakati TBS wanatutembelea na walipojiridhisha na bidhaa zetu wametupa namba za ubora" alisema Ivan.

Mkurugenzi huyo alionyesha barua ambayo inamkataza kuuza bidhaa zake pamoja na kukubaliwa na TBS kuwa zina ubora, Barua ya Machi, 29 mwaka huu kutoka TFDA iliyosainiwa na Meneja wa Mamlaka hiyo kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Rodney Alananga inasema kuwa pamoja na kutambua kuwa bidhaa za kiwanda hicho zimethibitishwa na TBS, bado wao hawatampatia kibali cha kuendelea na uzalishaji na usambazaji.

“Bidhaa zako zimethibitishwa ubora na TBS na kuwa zina ubora wa juu na pia unaomba Mamlaka itambue uwepo wa TBS katika bidhaa zako. Kumbuka kuwa kwa mujibu wa mwongozo wa usajili wa bidhaa za vipodozi wa mwaka 2015, kifungu namba 2.2, mchakato wa usajili hufanywa ndani ya siku 90 ikiwemo kujibu hoja zitakazotolewa, kama maombi hayajakidhi matakwa ya sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi mwombaji anatakiwa kuomba upya na maombi yaambatane na malipo mapya pamoja na fomu husika.” imeeleza barua hiyo yenye kumbukumbu namba EC.67/82/364/01/08.

Meneja huyo wa TFDA, alipokuwa akijibu maswali ya mwandishi alipofuatwa ofisni kwake alikiri kuendelea kumnyima usajili na kupima bidhaa za Ivan Products kwa madai kuwa jengo la kiwanda cha mjasiriamali huyo halijakaguliwa na TFDA.

“Huyo Ivan Products ninamfahamu na ni kati ya wajasiriamali zaidi ya 76 waliopo mkoani Mbeya ambao tuliwapa mafunzo ya namna ya ujenzi wa kiwanda unavyopaswa kuwa na kwamba hatutaweza kumsajili wala kupima bidhaa zake kama hatujakagua jengo la kiwanda” alisema Analanga.

Alisema mamlaka yake si chombo cha kutoa elimu bali kusimamia ubora na usalama na kwamba hata kama mjasiriamali kapewa kibali na TBS wao wataendelea kutomtambua kwasababu ni mamlaka mbili tofauti ambapo TBS wapo chini ya Wizara ya Viwanda lakini TFDA wapo Wizara ya Afya.

“Wanaotaka kuanzisha viwanda wajaribu pia kuiga mfano wa kiwanda cha kukoboa na kusaga unga cha NMC pale Iringa ambao kabla hawajaanza kuzalisha walikuja na tukaenda kukagua  kiwanda na kuwasajili. Hatuwezi kusajili bidhaa zinazosindikwa chumbani kwa mtu” alisema Meneja huyo.

Aidha alieleza kuwa bidhaa nyingi zinazosindikwa na baadhi ya wajasiriamali wa viwanda vidogo husindikwa katika hali ya uchafu na usindikaji wao ni wa mazoea badala ya kusindika kisayansi huku wakidanganya umma kwa kuandika maandishi kwenye vifungashio ambayo hayaendani na bidhaa husika na kwamba kati ya wajasiliamali wanaojihusisha na uzalishaji wa bidhaa za viwandani ni wajasiriamali watano tu ambao bidhaa zao zimesajiliwa na TFDA kwa mkoa wa Mbeya.

Kwa mujibu wa Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Viwanda, biashara na Uwekezaji nchini 2016/2017,  Waziri wa Wizara hiyo Charles Mwijage, ametaja kuwa, hapa nchini kuna viwanda vidogo 6,907.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu 0754440749 na barua pepe kalulunga2006@gmail.com.

No comments: