Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Friday, October 21, 2016

Mbeya Textile; Kug’olewa mtambo kuliua kiwanda*Yadaiwa ulipelekwa kufungwa Mwatex
*Habari zaidi zadai uliuzwa nchini Kenya
*Kiwanda kikauawa na kufungwa 2011

NA GORDON KALULUNGA

CHANZO cha kufa kwa kiwanda Mbeya Textile Ltd kilichopo Halmashauri ya wilaya ya Mbeya, kimetajwa kuwa ni ung’oaji wa mtambo bora wa kuzalisha vitenge na kupelekwa Mwanza.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa baada ya serikali kukibinafsisha, uongozi na wawekezaji uliingia mkataba wa makubaliano wa kung’oa mtambo huo kisha kuupeleka Mwanza.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana katika kiwanda hicho Makubaliano hayo yalifanyika kati ya New Mbeya Textile Mill. Ltd na Mwatex (2001) Ltd Machi 27, 2003 ambapo mkataba huo uliandaliwa kwa umahiri wa mwanasheria RK Rweyongeza & Co.Advocate wa S.L.P 75192 Jijini Dar es Salaam, barabara ya Morogoro, mtaa wa Indira Gandhi.

Mkataba huo ambao una kurasa nne na vipengele saba vya makubaliano, katika kipengele cha tatu kinaeleza kuwa Mwatex watakuwa wakiilipa New Mbeya Textile Ltd kiasi cha Dola za kimarekani 2,000.

Mkataba huo ambao upo kwa Lugha ya Kiingereza, kipengele cha tatu cha makubaliano kimeandikwa "In consideration of the letting of this machonery by the LESSOR to the LESEE shall pay to the LESSOR, a sum of USD 2000 paid monthly in areas with affect from the date of which the machine shall bocome operational” kinasomeka kipengele hicho.

Kusafirishwa kwa mtambo

Kufanikiwa kwa mwanadishi wa habari kuuona mkataba huu kulimfanya aongeze jitihada kufahamu mtambo huo ulivyosafirishwa kutoka mkoani Mbeya.

Hata hivyo, uchunguzi wa mwandishi ulipata taarifa zisizo rasmi zilizodai kuwa mtambo huo badala ya kusafirishwa kwenda Mwanza ulipelekwa nchini Kenya ambako inasadikika kuwa uliuzwa huko.

Taarifa za awali zinaonyesha kuwa siku 27 baada ya mkataba huo kutiwa sahihi na pande mbili za wawekezaji hao wa kiwanda cha New Mbeya Textile Mill Ltd na Mwatex (2001), mtambo huo uliondolewa katika kiwanda cha New Mbeya Textile Mill Ltd kwa ulinzi mkali baada ya baadhi ya wafanyakazi kupinga mtambo huo kuondolewa kiwandani hapo.

Nyaraka ya kusafirishia mtambo huo pamoja na vifaa vyake ambayo gazeti hili limeshuhudia, zimeonyesha wazi kuwa mtambo huo ulisafirishwa April 24, 2003 kwa gari kubwa lenye namba za usajili TZ 68933/TZE 5862.

kwa mujibu wa barua hiyo ambayo ilitoka katika uongozi wa New Mbeya Textile Mill Limited, Songwe Industrial Area yenye kichwa cha habari kisemacho, TO WHOMSOEVER IT MAY CONCERN inasema “As per the agreement dated 27th March 2003 between M/s. New Mbeya Textile Mill Ltd., P.O. Box. 950, Mbeya, Tanzania and M/s Mwatex (2001) Ltd., P.O. Box 1420, Mwanza, Tanzania, we are sending herewith the used Printing Machinery parts and accessories to M/s Mwatex (2001) Ltd. Through Truck No. Tz 68933 / TZE 5862.
We hereby declare that there is no sale involved in this transaction” imeeleza barua hiyo.


Kufungwa kwa kiwanda

Kwa mujibu wa barua hii baada ya mtambo kuondolewa kiwandani hapo, uzalishaji ulianza kuwa hafifu, hatimaye Machi 31, 2011. barua yenye kumbukumbu namba PF/05/004 iliyosainiwa na aliyekuwa meneja wa kiwanda hicho C.V. Isinika, iliwataarifu wafanyakazi kusudio la kufunga kiwanda na April 1, 2011 kiwanda kikafungwa rasmi na kugeuzwa ghala la kuhifadhia Tumbaku.

Mwekezaji wa kiwanda hicho, Barakat Ladhan ambaye pia ni Mkurugenzi wa kiwanda, alipotafutwa kuelezea ulipo mtambo huo na kama kuna mpango wa kufufua kiwanda hicho hakuweza kupokea simu ila alijibu meseji fupi na kusema “Sorry couldnt pic the call as I am not well. May be will speak tommorrow. Who is this pls? maana yake, “Samahani sikuweza kupokea simu. Sijisikii vizuri. Huenda tutaongea kesho. Nani Mwenzangu? alimalizia ujumbe wake.

Licha ya Mwandishi wa habari kujitambulisha na kesho yake kumpigia simu bado hakuweza kupokea simu wala kujibu tena ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu yake ya kiganjani.
  
Viongozi watoa ya moyoni

Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Gabriel Makala, ametembelea katika kiwanda hicho na kujionea hali ilivyo tangu kiwanda kifungwe na kuiomba Wizara ya Kilimo, chakula na uvuvi kupitia idara ya utafiti, kutoa ufafanuzi kwa wakulima wa zao la Pamba katika wilaya ya Mbeya na Chunya mkoani Songwe juu ya katazo la kulima zao hilo kwa miaka zaidi ya kumi sasa kwa madai kuwa kulikuwa na funza mwekundu kutoka nchini malawi ambaye alitajwa kuwa ni moja ya tatizo la kufunga kiwanda hicho kwa kukosa Malighafi mwaka 2011.

Diwani wa kata ya Bonde la Songwe, Ayas Njarambaha mahala ambapo ndipo kilipo kiwanda hicho, alisema hakubaliani na uamuzi uliotolewa na uongozi wa wawekezaji hao kuwa wanataka kukifufua kiwanda hicho lakini kiwe kinasagisha nafaka hasa mahindi ya unga wa ugali na kuzalisha Pumba.

“Hii haijakaa vizuri hata kidogo, mwekezaji anasema anataka kubadili  matumizi ya kiwanda cha nguo kwa kisingizio kuwa pamba iliyokuwa ikilimwa Chunya haipatikani. Sasa watueleze kuwa je kiwanda cha Urafiki pamba inalimwa Kibaha? Alihoji diwani huyo.

Aliyekuwa Katibu wa chama cha wafanyakazi wa kiwanda hicho (TUICO) Kenny Kayanga, alisema wao hawakushirikishwa katika uondoaji wa mtambo huo na kwamba hata baadhi ya wananchi wa kijiji cha Songwe walipojaribu kuandamana kuzuia mtambo huo usiondoke kiwandani hapo, walitawanywa na askari Polisi ambao walifika katika eneo hilo na kuuondosha.

“Tulikuwa tunazalisha mita nyingi sana za vitambaa na mtambo huo uliondoka chini ya ulinzi wa Polisi na waliokuwa mstari wa mbele kuhoji walifukuzwa kazi na mpaka kiwanda kinafungwa tulikuwepo wafanyakazi wenye ajira 200 na wengine wengi walikuwa ni vibarua” alisema Kayange.

Anasema baada ya kiwanda kufungwa, walimwandikia Mkurugenzi wa kiwanda hicho barua ya April 1, 2011, iliyohusu mapendekezo ya ulipwaji wa mafao ya wafanyakazi.

Mapendekezo ambayo yapo katika barua hiyo walitaka malipo yote yalipwe kwa mujibu wa sheria, kupewa mishahara ya miezi miwili kwa kilamwaka wa mfanyakazi aliofanya kiwandani hapo, wafanyakazi wa kutwa kupewa mkono wa kwaheri.

Viinua mgongo vya machozi
Hata hivyo, mapendekezo hayo hayakuzingatiwa na badala yake uongozi wa kiwanda uliwalipa mafao wafanyakazi hao jinsi ulivyotaka ambapo wafanyakazi waliofanya kazi kwa miaka kumi walipata kiinua mgongo cha Tsh 444,000.

Taarifa ya malipo hayo yanajidhihilisha katika barua ya ndani ya kiwanda hicho iliyosainiwa na aliyekuwa meneja utumishi na utawala C.Y Isinika, ambayo mwandishi amebahatika kuiona.

Barua hiyo ya Machi 31, 2011 yenye Kumbukumbu namba Ref No. PF/05/004 ambayo nakala ilipelekwa kwa Meneja wa fedha, Mwenyekiti wa TUICO New Mbeyatex na kwa mkuu wa idara.

Barua hiyo inaijulisha idara ya uhasibu kumlipa mtu aliyefanya kazi kwa miaka kumi kiwandani hapo kiasi cha Tsh 126,933 kwa ajili ya mshahara wa siku 28 kufidia taarifa ya kuachishwa kazi, Tsh 366,154 kwa ajili ya kiinua mgongo kwa miaka kumi, Tsh 68,000/= kwa ajili ya mabaki ya likizo ya siku 15 ambapo jumla mfanyakazi aliyefanya kazi kwa miaka kumi alistahili kupata 561, 087/=.

“Toa mchango wa NSSF Shs 56,109/=, Kodi P.A.Y.E Shs 60,496, Loan/Salary Advance…..Shs 116,605/=. Malipo yake halisi baada ya makato ya hapo juu ni Shs. 444,000/=” imeeleza moja ya haya ya barua hiyo.

Parandesi ya pili kutoka mwisho wa barua hiyo inaeleza kuwa, hata hivyo malipo ya NSSF yangelipwa baada ya kukamilika taratibu zinazotakiwa na mfuko huo, jambo ambalo baadhi ya waliokuwa wafanyakazi wa kiwanda hicho wamesema halijafanyika mpaka sasa.

Wabunge wanena.
Naye Mbunge wa Viti maalum mkoa wa Mbeya, Dkt. Mary Mwanjelwa, alipohojiwa kuhusu sababu za kufungwa kiwanda hicho kama anazifahamu na nini maoni yake kuhusu kiwanda hicho kubadilishwa matumizi alisema ni muhimu msajili wa hazina aeleze mkataba ukoje maana miundombinu ilijengwa kwa ajili ya kiwanda cha nguo.

“Dar es Salaam kuna viwanda vya nguo lakini hakuna mashamba ya pamba. Nimewahi kuhoji sababu za kiwanda hicho kufa nikaambiwa ni ukosefu wa pamba na mdudu mwekundu. sasa je, hao watafiti tangu walipofanya utafiti wao na kugundua kuwa kuna ‘mdudu’ huyo na hatimaye kiwanda kikafa, kwanini hawajafanya utafiti mwingine wa jinsi ya kumuua huyo mdudu?” alihoji Dkt. Mary Mwanjelwa.

Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini Oran Njeza, naye alipohojiwa alisema “Yote yanategemea mkataba wa ubinafsishaji, na mwongozo anao msajili wa Hazina. Kinachohitajika ni kipi katika mipango mikakati 2 ina faida kwa wananchi na taifa letu” imesomeka sms yake ambayo alijibu swali la mwandishi kwa njia ya mtandao wa Whats App.


Waziri Mkuu atoa agizo.
Agosti 8, mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alipokuwa akifunga maonyesho ya wakulima wa kanda ya Nyanda za juu kusini Nane Nane katika viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya, alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla kutembelea na kukagua viwanda vyote kikiwemo kiwanda cha Mbeya Textile.

Septemba 7, mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Makalla alitembelea viwanda vya New Mbeya Textile, Tanganyika Packers na ZZK Mbeya na kuwataka wawekezaji wote walionunua viwanda kutoka serikalini kuanza uzalishaji au kuonyesha mipangp ya muda mfupi wa kuanza uzalishaji.

Kiwanda hicho kilikuwa kikiajiri wafanyakazi 600, lakini taarifa zinasema kuwa, endapo mwekezaji huyo atabadili matumizi na kuanza kusagisha unga wa Sembe, kitaweza kuajiri wafanyakazi 200.

Wizara ya Viwanda yaungama.
Kwa mujibu wa tovuti ya bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, http://www.parliament.go.tz/index.php/supplementary_questions/291/1360/read  serikali inapoteza bilioni 133 kutokana na ukwepaji wa kodi unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wanaoingiza nguo hapa nchini.

Ungamo hilo lilitolewa na serikali baada ya Mbunge wa viti maalum mkoa wa Mbeya Dkt. Mary Mwanjelwa kuitaka serikali kueleza mkakati wa kukifufua kiwanda cha Mbeyatextile ambacho alisema kimetelekezwa kwa muda mrefu.

“Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nimeletewa ripoti, TRA kuanzia mwezi Januari mpaka mwezi wa Mei, walikuwa wameshindwa kuwakamata watu waliopitisha nguo ambazo hazikulipa bilioni 133. Natoka hapa nakwenda kuripoti kwa Waziri wa Fedha, bilioni 133, nguo zilikuwa under-valued, nguo moja nimeoneshwa na wataalam, kilo moja ya nguo ilikuwa imeingizwa nchini kwa kadirio la bei ambayo ni ndogo kuliko pamba, finishing cloth, nguo iliyokwisha tengenezwa kilo moja yake ilikuwa imeingizwa nchini kwa thamani ambayo ni ndogo kuliko bei ya pamba ya Mwanza. Sasa mazingira yote kwa ujumla ndiyo yanafanya ufufuaji wa viwanda hivi iwe vigumu, lakini yote hayo tunayamudu, tutayafanyia kazi, Mbeyatex na yenyewe itafanya kazi” alisema Waziri wa Viwanda, biashara na uwekezaji Charles Mwijage.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, kutokana na uwepo wa taarifa za utoroshwaji wa mitambo kadhaa ya kiwanda hicho, Mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Gabriel Makalla, ameunda tume ya kuchunguza ilikopelekwa mitambo ya kiwanda hicho.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa simu 0754 440749

No comments: