Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Wednesday, November 16, 2016

KIGOMA; Wakurugenzi watano wa Halmashauri kuburuzwa Mahakamani

Na Gordon Kalulunga, Kigoma

CHAMA kipya cha kulinda na kutetea haki za Walimu Tanzania (CHAKUHAWATA), kimesema kinakusudia kuwapeleka Mahakamani wakurugenzi wa Halmashauri tano nchini, baada ya kukiuka haki za walimu.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi katika mahojiano maalum, Mwenyekiti wa chama hicho Kalimwabo Sabibi, aliwataja wakurugenzi ambao wanatarajia kuwaburuza Mahakamani kuwa ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa Kigoma/Ujiji, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma (V), Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu (V), Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo na Halmashauri ya Wilaya ya Geita.

Alipoulizwa sababu alisema baada ya chama hicho kupata usajiri mwezi Juni 24, 2015 na kupatiwa namba ya usajili 033 na Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri chini ya sheria namba 6/2004 ya Ajira na Mahusiano kazini, Katibu Mkuu ofisi ya Rais, Menejimenti ya utumishi wa Umma alikipatia chama namba ya makato kwa wanachama wao (Dudaction code) Februari 03, mwaka huu.

“Tulipopewa namba ya makato tulianza kusajili wanachama waanzilishi kwa kujaza fomu maalumu (TUF 6) ya kuruhusu Mwajiri kufanya makato ya ada kutoka katika mshahara wa mwanachama kwenda CHAKUHAWATA lakini Wakurugenzi wa Halmashauri hizo hawataki kufanya hivyo” alisema Sabibi.

Alieleza kwamba pamoja na chama hicho kusajili wanachama na kupelekwa kwa fomu TUF 6 za wanachama hao kwa Waajiri wao kwa lengo la kufanyika kwa makato ya ada za Wanachama hao, Waajiri wameshindwa kutekeleza makato hayo kama wanavyo elekezwa na sheria 6/2004, ya Ajira na Mahusiano kazini, kifungu cha 61(1), licha ya viongozi wa chama kuwaandikia barua na kuonana nao kwa lengo la kuhimiza kufanya makato hayo.

“Tumefikia hatua hiyo baada ya jambo hili kuchukua zaidi ya miezi saba sasa bila kufanyika makato hayo na kuyapelekea katika akaunti ya chama na limeathiri chama kufanya shughuli zake mbalimbali na kwa kuwa Chama kimekwisha kumwandikia barua Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, TAMISEMI ya malalamiko juu ya Waajiri hao na yeye kushindwa kujibu barua hiyo, ndiyo maana tunaenda kutafuta haki Mahakamani” alisema Mwenyekiti huyo.

No comments: