Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Saturday, December 31, 2016

FIKRA ANGAVU: Waraka mfupi sana kwako RC Amos Makalla

Waraka mfupi sana kwako RC Amos Makala

Na Gordon Kalulunga

FIKRA ANGAVU kutoka Nyikani ni za mambo madogo madogo kwa baadhi ya viongozi ambayo kwetu wadogo ndiyo makubwa.

Zikiwa zimebaki siku mbili kuumaliza mwaka 2016, nimeona nikuandikie waraka huu mfupi sana.

Hivi karibuni kumezuka ugonjwa maarufu kama UTI.

Kirefu chake ni (Urinary Tract Infection).

Kwa Kiswahili ni maambukizo ya bacteria katika njia ya mkojo.

Ugonjwa huu humsababishia mtu kuumwa sana na kupata homa, maumivu kwenye kinena, maumivu wakati wa kukojoa na kusababisha uharibifu kwenye via vya uzazi.

Nia ya waraka huu mfupi sana ni kuzungumzia suala la ujenzi wa vyoo bora.

Moja ya wilaya zako mkoani Mbeya yaani Mbeya DC (Jimbo la Mbeya Vijijini), inatajwa kuwa ni wilaya ya pili kutoka mwisho wa wilaya zaidi ya 100 za Tanzania,  kutokuwa na vyoo bora.

Taarifa zilizopo ni kwamba ugonjwa mkubwa katika wilaya hiyo ni matumbo na kuhara.

Moja ya madhara ya kutokuwa na vyoo bora ni pamoja na wananchi kupata minyoo.

Minyoo ina madhara mengi kutegemea aina ya minyoo, inaweza sababisha matatizo ya kifua, Allergic reaction, kuwashwa, kuharisha, matatizo kwenye ubongo,  hata kichaa na jipu kwenye ini na kadharika.

Mheshimiwa Mkuu wa mkoa wa Mbeya ndugu Amos Gabriel Makalla, taarifa nilizozipata ni kwamba watumishi wa Halmashauri hiyo wametangaza kuanzia January 2, 2017 wanaanza msako wa kukagua na kuwatoza faini ya Tsh. 500,000 kwa kila ambaye hana choo bora. (Wanajijazia max kabla hawajafanya mtihani).

Choo bora kwa maelezo yao ni choo ambacho haina paa, kuta ya kusitili mwili, sakafu inayosafishika, tundu lisilotoa harufu na mfuniko wa kufunikia tundu.

Hali hii imekuja baada ya kuonekana kuwa mkoa wa Njombe umeongoza kuwa na vyoo bora.

Huko Njombe ni kwamba kuna vyoo bora katika kila kijiji vilivyojengwa chini ya halmashauri kwa ajili ya wananchi kujifunza choo bora kinatakiwa kiweje.

Hapo linakuja swali kuwa je Mbeya vijiji yenye vijiji 141, vitongoji 935, vitongoji vya mji mdogo wa Mbalizi 12, ni wapi palipo na choo bora cha mfano mpaka serikali ikimbilie kwenye faini? Kuna nini huko kwenye faini? Je kuna ulaji au ni kutimiza wajibu wa kazi yao?

Mheshimiwa Mkuu wa mkoa, waraka huu ni mfupi sana, nimeona nikudokeze jambo hili kidogo maana hivi karibuni umetangaza oparesheni ya kuliweka jiji la Mbeya katika hali ya usafi.

Mwisho ingawa sina maana halisi ya hitimisho, nong'ona na watendaji wa wilaya hiyo waanze kwanza kutoa elimu na kuonyesha mfano wa hicho wakiitacho choo bora hasa kwa wananchi wasio na uwezo.

Maafisa Afya katika Kata na vijijiji watenge muda wa (ma)saa manne kupitia hata kaya kumi kutoa elimu ya choo bora kuliko kukimbilia huko kwenye faini ambazo historia inajisimamia na kuonyesha kuwa huambatana na rushwa.

Waanzie mashuleni kutoa elimu na hata kukamata au kutoza faini basi wakaanzie huko kisha waingie mtaani.

Tuokoe watoto ambao muda mwingi wanakuwa shuleni na kizazi hicho kikijengewa mazingira ya kupenda usafi, katika makuzi yao watashauri na baadae watajenga vyoo bora.

Fikra hizi Angavu kutoka huku nyikani, zinazoangazia mambo madogo ambayo ni makubwa kwa wasio na sauti zikufikie huku ukitumia vema jicho lako badala ya kudanganyika na kiitwacho  Opras yaani (Fomu za kujitathimini) ambazo watumishi wanajitathimini wenyewe utendaji wao.

Huo ndiyo waraka wangu mfupi sana kwako mwaka huu 2016.

Karibu sana Nyikani.

No comments: