Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Wednesday, December 07, 2016

HADITHI TULIVUTumia matatizo yako kupata mafanikio au kujididimiza zaidi.

Mungu anataka kilakitu unachotaka uwe nacho hapa duniani, ukipate.

Hivi ndivyo nilivyowahi kuambiwa miaka ya nyuma kidogo.

Haikuwa rahisi kuamini kuwa maneno hayo yalikuwa na nguvu ya kuweza kubadili maisha yangu.

Siku moja nilijiuliza moyoni kuwa kwanini Mungu hakutaka niwe kama wenzangu ambao wana nyumba nzuri na magari mazuri nk.

Lakini sikupata jibu! Nikaiambia nafsi yangu kuwa je mimi nina laana? Je Mungu ana upendeleo? Mbona watu wanasema Mungu hana upendeleo?

Nilizidi kuwaza, huku baadhi wakinikejeli! Mawazo yakanizidi kichwani.

Kuna siku nikawa naelekea mjini, wakati navuka barabara nikiwa na lindi la mawazo huku nikijihisi mtupu, niliponea chupuchupu kufa kwa kugongwa na gari.

Dereva yule alinikwepa kisha akasimamisha gari na kuaza kunitukana sana matusi ya nguoni, na kunitolea maneno makali ya kashfa, hakika yalinichoma sana moyoni.

Nikaanza kuhisi kuwa nina mkosi zaidi, mtu ambaye sina bahati na hatimaye machozi yakanidondoka huku nikiendelea kutembea.

Ukiona mwanaume analia basi kuna jambo! Ghafla nikaona lile gari lililotaka kunigonga, likinifuata tena kwa kasi! Na yule dereva akaniambia anipe rifti.

Nikakubali kwa shingo upande na nikiwa ndani ya gari, dereva akaniuliza kama kuna jambo limenikuta, kwani alihisi nina mawazo sana.

Nikavuta pumzi na kumwambia. Ndipo naye akaniambia kuwa, kuna siku moja Ng’ombe wake alitumbukia ndani ya shimo refu na akajaribu kumtoa lakini akashindwa.

Baadhi ya majirani zake ambao hawakumpenda na kupenda mafanikio yake walifurahi sana na wakaanza kutupa matakataka na udongo ndani ya shimo ili kumdhuru yule Ng’ombe afe.

Alisema wakati akiwa kazini, wabaya wake hao, walipokuwa wakitupa takataka hizo na udongo, bila kujua, kumbe yule Ng’ombe alikuwa akijikung’uta zile takataka na udongo ukawa unashuka chini yeye anakanyaga na kupanda juu.

Kadri walivyozidi mumtupia takataka na udongo, akazidi kupanda! Kufumba na kufumbua, yule Ng’ombe akatokeza kichwa na kulia Mmoooooo!

Watu walitaaruki, kuwa iweje Ng’ombe yule katoka mzima! Ndipo yule dereva aliponiambia kuwa, kuna wakati inafikia kila aina ya uchafu utatupiwa, lakini ni maamuzi yako kuamua kijikung’uta na kutumia uchafu huo huo kama daraja la kukuvusha nje au ukubali kufunikwa na huo uchafu kisha ufe.

Maneno ya dereva huyu, yanatukumbusha kuwa kuna wakati wa kulia na wakati wa kucheka,  pia kuna wakati wa kupada na wakati wa kuvuna.

Sikiliza nikuambie, unaweza kuinuka tena, sikio lako halisi naamini limesikia.

No comments: