Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Monday, December 19, 2016

TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KWA VYOMBO VYA HABARI “PRESS RELEASE” TAREHE 19.10.2016.

Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu. Hata hivyo siku ya tarehe 18.12.2016 huko Wilaya ya Chunya hali haikuwa shwari kutokana na wananchi kufanya fujo zilizosababisha madhara kwa binadamu na uharibifu wa mali.

Mnamo tarehe 18.12.2016 majira ya saa 11:45 asubuhi huko katika Kituo cha Polisi Makongolosi kilichopo Kata ya Makongolisi, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, Kundi la wananchi walioamua kujichukulia sheria mkononi walivamia kituo cha Polisi  Makongolosi na kufanya fujo kwa kuwarushia  mawe hovyo askari wa Kituo hicho kwa  lengo la kuwatoa watuhumiwa wawili   waliofahamika kwa majina ya 1. ERASTO ROBERT, [28] mkazi wa Kilombero na 2. BASI LINUS [24] mkazi wa Makongolosi waliokuwa wanakabiliwa na kosa la mauaji [MKI/IR/1249/2016] kwa lengo la kuwatoa nje na kuwauawa kwa kuwachoma moto. 

Awali mnamo tarehe 11.12.2016 majira ya saa 23:20 huko katika Kitongoji cha Manyanya, Kata ya Makongolosi, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la JACOB BROWN @ SALAMA [66] Mkazi wa Manyanya alivamiwa na watu wasiojulikana akiwa peke yake shambani kwake na kuuawa. Kutokana na tukio hilo Polisi walifanya msako na kuwakama watu wawili ambao ni 1. ERASTO ROBERT [28] na 2. BASI LINUS [24] kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo.

Awali inadaiwa kuwa wananchi hao walifika Kituoni hapa kwa lengo la kuwatoa nje watuhumiwa hao wawili lakini Mhe. Diwani wa Kata ya Makongolosi aitwaye LUSAJO NTOFYO @ KOMANDO aliweza kuongea na wananchi hao na kisha kutawanyika. Lakini mara baada ya muda wa nusu saa wananchi hao walirudi tena wakiwa na silaha mbalimbali pamoja na mafuta ya Patrol kwa lengo la kuchoma moto kituo hicho.Aidha wananchi hao walifunga barabara ya Chunya/Makongolosi kwa kuweka mawe makubwa na magogo hali iliyosababisha usumbufu mkubwa wa watumiaji wengine wa barabara hiyo.

Kutokana na hali hiyo Polisi walijipanga na kukabiliana na hali hiyo kwa kutumia mabomu ya machozi na risasi baridi ili kuwatawanya wananchi hao waliokuwa na hasira na jazba dhidi ya watuhumiwa hao. Polisi wa kituo cha Makongolosi, Polisi kutoka Chunya, Section mbili za askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia wakiwa wameongozana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishna wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mbeya BENJAMIN E. KUZAGA walifika eneo la tukio kwa ajili ya kuongeza nguvu na kufanikiwa kudhibiti vurugu hizo.

Aidha katika vurugu hizo watu wanne walijeruhiwa ambao ni 1. DIMITA MWANGABULA [24] fundi uashi, mkazi wa Makongolosi [aliumia miguuni na mikononi] 2. AMOSI KANDONGA [16] mkazi wa Kasumulu Wilaya ya Kyela [aliumia puani] 3. HAWA MASUMBUKO [21] mkazi wa Makongolisi [aliumia mkononi wa kulia] na 4. AMOKE MBILINYI [25] mkazi wa Makongolisi [aliumia kifuani] ambao walikimbizwa hospitali ya Wilaya ya Chunya kwa matibabu. Hata hivyo majira ya saa 17:15 jioni AMOKE MBILINYI alifariki dunia.

Katika tukio hilo askari 4 walijeruhiwa kwa kupigwa mawe ambao ni 1. G.4684 D/C DEOGRATIAS [aliumia mguu wa kulia na jicho la kushoto] 2. H.2361 D/C SHABAN [aliumia mguu wa kushoto] 3. H.5314 PC ASHERI [aliumia miguuni] na 4. H.3650 PC ADAM [aliumia mguu wa kushoto na jicho la kulia], majeruhi wamepatiwa matibabu na kuruhusiwa. Jumla ya watuhumiwa 41 kati yao wanaume 34 na wanaweke 7 wamekamatwa. Watuhumiwa 21 kati yao mwanamke 01 na wanaume 20 wamefikishwa mahakama ya Wilaya ya Chunya. Thamani ya uharibifu bado kufahamika. Hali imerejea kuwa shwari.

MAFANIKIO KATIKA MISAKO, DORIA NA OPERESHENI.

Mnamo tarehe 18.12.2016 majira ya saa 16:00 jioni huko katika uwanja wa mpira wa kumbukumbu ya Sokoine uliopo Kata na Tarafa ya Sisimba, jiji na mkoa wa Mbeya,  Askari Polisi wakiwa doria walimkamata mtu mmoja aitwaye EVARISTO MWALONGO [33] mkazi wa Lyoto na wenzake 4 wakiwa na bhangi kilo 3 na gram 455.

Mnamo tarehe 18.12.2016 majira ya saa 17:00 jioni huko katika Mtaa wa Mafiati, Kata na Tarafa ya Sisimba, jiji na mkoa wa Mbeya. Askari Polisi wakiwa doria walimkamata mtu mmoja aitwaye HENRY MWAMFUPE [19] mkazi wa Ilemi – Darajani akiwa na dawa zidhaniwazo za kulevya kete 3 aina ya heroine.

Watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya pia linaongeza jitihada za kuzuia na kupunguza ajali za barabarani kwa kuhakikisha madereva na watumiaji wengine wa barabara wanatii sheria za usalama barabarani. Aidha kumekuwa na tukio 01 la ajali ya kifo kama ifuatavyo:-

Mnamo tarehe 18.12.2016 majira ya saa 13:30 mchana huko Kijiji cha Chamoto – Kibaoni – Igurusi, Kata ya Igurusi, Tarafa Ilongo, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya, Powertiller aina ya Kubota iliyokuwa ikiendeshwa  na HAMPHEY MAGAMBO [17] mkazi wa Utengule ilimgonga mtembea kwa miguu mtoto aitwaye LULU SAMWEL mwenye umri wa miaka 3 mkazi wa Igurusi na kusababisha kifo chake.

Chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa mwendesha Powertiller ambaye alikimbia baada ya tukio. Upelelezi unaendelea ikiwa ni pamoja na msako wa kumtafuta mwendesha Powertiller.


WITO:

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishna wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa wananchi kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi kwani vinasababisha madhara makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia na usumbufu kwa wengine. Kamanda KIDAVASHARI anawataka wananchi kusubiri vyombo husika kuchunguza na kufuata taratibu za kisheria ili kutenda haki. Aidha anatoa wito kwa jamii kuacha kutumia dawa za kulevya kwani ni kinyume cha sheria na ni hatari kwa afya zao. Pia anatoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za mtu, watu au mtandao wa watu wanaojihusisha na uingizaji, usambazaji na uuzaji wa dawa za kulevya ili wakamatwe.

                                           Imesainiwa na:
 [DHAHIRI A. KIDAVASHARI - DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

No comments: