Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Tuesday, January 03, 2017

BARABARA MBOVU YAWAKIMBIZA WAWEKEZAJI MBEYAMeneja Mkuu wa kiwanda cha TBL Mbeya Plant, Waziri Jemedari.
   
*Wangeajili watanzania zaidi ya 200

Na Gordon Kalulunga


Ubovu wa barabara inayoelekea katika eneo maalum la viwanda mkoani Mbeya (Iyunga Industrial Area), umewakimbiza wawekezaji wa kampuni ya SAB Miller kutoka nchini Uingereza, kujenga kiwanda cha kuzalisha kimea cha kuzalishia vinywaji.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hii ambaye anatafiti na kuandika habari za Viwanda, Miundombinu na ubunifu nchini, Meneja Mkuu wa kiwanda cha TBL Mbeya Plant, Waziri Jemedari, alikiri wawekezaji hao kukataa kujenga kiwanda kutokana na ubovu wa barabara.

Jemedari alisema wawekezaji hao walitembelea kiwanda hicho ambacho kinachoongozwa na watanzania na kuhitaji kuwekeza zaidi, lakini walikataa kufanya hivyo baada ya kuona ubovu wa barabara hiyo ambayo haizidi Kilomita 3 kutoka barabara kuu.

“Wawekezaji hao walitoka Uingereza ambako ndiko makao makuu ya SAB Miller na kuja kuangalia kiwanda chetu ambacho ni cha 12 kwa ubora duniani kati ya 120 na kuhitaji kujenga kiwanda kwa ajili ya kimea,  lakini wakakataa kutokana na ubovu wa hii barabara na wanaenda kujenga mkoani Iringa” alisema Jemedari.

Meneja huyo alisema kiwanda hicho kingejengwa eneo hilo, kingeongeza ajira kwa watanzania zaidi ya 200 hasa wakazi wa Mbeya kwasababu kingekuwa na mzunguko wa (Shifti) Nne.

“Kwanza tuliulizwa kama tunalipa kodi serikalini, tukawajibu kuwa
tunalipa vizuri, wakauliza kwanini barabara haitengenezwi, tukakosa jibu sahihi ndipo wakasema hawataweza kujenga kiwanda hicho, tukakosa fursa” alisema Meneja huyo.

Alisema licha ya barabara hiyo kuwa mbaya hasa nyakati za masika, wasema ukweli katika sekta ya viwanda wanawekwa kwenye kundi la wapinzani wa serikali wakati lengo lao ni kutoa dira sahihi kwa serikali ili kufikia lengo la tamko la Rais Dkt. John Magufuli kuwa na viwanda pamoja na kulinda soko la ndani.Vibao vya kiwanda cha Pepsi, Coca Cola na TBL kama vinavyoonekana njia panda ya kwenda eneo la Viwanda Iyunga (Ituta), Mbeya mjini.

Meneja rasiliamali watu wa kiwanda cha Pepsi kilichopo eneo hilo la viwanda, Edwin Arbogast, alipohojiwa kuhusu hasara wazipatazo kutokana na ubovu wa barabara hizo, alisema anaomba asinukuliwe chochote kuepuka kusigana na serikali.
Diwani wa kata ya Iyunga iliyopo ndani ya Jiji la Mbeya, ambako ndiko lilipo eneo hilo maalum kwa ajili ya viwanda, Essau Kalinga
alipoulizwa kuhusu barabara hiyo alisema tayari ipo kwenye mpango na mchakato wa kujengwa.
“Barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha Lami mwanzoni mwa mwaka kesho 2017 maana tayari ipo kwenye mpango mzuri wa ujenzi na mwaka huu tuliweka changarawe lakini bila mitaro ya kupitishia maji na kwa kweli imeanza kuharibika tena” alisema diwani huyo.
Aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo hilo kupitia NCCR Mageuzi, Mwalimu Posian Mwaiseje, alisema ili kufikia lengo la uchumi wa kati kupitia viwanda ni lazima maarifa ya wataalam yashushwe kwa wananchi ikiwemo elimu kwa watu wazima.
“Namaanisha kuwa bila elimu kwa mfumo wa Kiswahili watanzania hawatakuwa na uelewa sawa. Hivyo ili kufanikiwa lazima kwanza watanzania wawe na maarifa sawa kupitia Lugha ya Kiswahili hapo tutaweza kwenda pamoja katika tamko la Rais Magufuli” alisema Mwaiseje.
Naye Kamishina wa chama hicho mkoa wa Mbeya, Daimon Mwasampeta, alisema barabara hizo hazitengenezwi kwasababu nia njema ya Rais John Magufuli kuhusu viwanda anayo mwenyewe huku watendaji wake wakiwa hawana dhamira hiyo.
“Dhamira njema ya Rais Magufuli anayo mwenyewe sawa na kipindi cha Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa na dhamira ya peke yake ya Azimio la Arusha huku wasaidizi wake wakimwitikia machoni na kuishi kibepari” alisema Mwasampeta.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa habari za Utalii na uwekezaji Tanzania (TAJATI), Christopher Nyenyembe, alipohojiwa alisema eneo la Iyunga licha ya kwamba ni eneo lililotengwa kwa ajili ya viwanda, lakini kwa sasa wananchi wanalima Mahindi na Maharage kwasababu serikali inaonyesha kuwa haina dhamira ya dhati kuweka miundombinu ya barabara katika maeneo ya uwekezaji mkubwa hasa viwandani.
“Maeneo yale kuna kiwanda cha (malumalu) Marmo, Coca Cola, Pepsi, TBL, Reli ya Tazara imepita na bandari kavu (Malawi Cargo) ilikuwepo”
“Mbeya wanaendelea kujenga barabara kwa kiwango cha kokoto katika maeneo mbalimbali, cha ajabu ni kwamba barabara zinapelekwa katika vilabu vya pombe za kienyeji badala ya kujengwa katika maeneo yenye uwekezaji mkubwa ili vijana wapate ajira na serikali iendelee kupata kodi” alisema Nyenyembe.

Makamu Mwenyekiti huyo wa TAJATI, alisema wao kama waandishi wa habari za utalii na uwekezaji Tanzania, wanaiomba serikali itupie jicho katika ujenzi wa miundombinu ya barabara maeneo ya viwandani ikiwemo maji ya uhakika, umeme wa uhakika na miundombinu imara ya maji safi na maji taka.

Aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda na biashara katika Bunge la 10, Vick Kamata, aliishauri serikali kuweka kipaumbele katika suala la kutenga ardhi kwa ajili ya viwanda kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya na mikoa ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu bora kama vile barabara, reli, maji, umeme na mawasiliano.

Uchunguzi umebaini kuwa, hali ya ubovu wa barabara ziendazo viwandani kama eneo la viwanda la Iyunga mkoani Mbeya, ipo pia katika Halmashauri ya Moshi mkoa wa Kilimanjaro katika barabara ya kwenda kiwanda cha Bonite na kiwanda cha bia cha Serengeti Breweries mkoani Kilimanjaro.

Baadhi ya madereva wa magari ya kampuni za  TBL, Coca Cola, Pepsi, Marmo Granito waliohojiwa na mwandishi wa habari hii kwa ombi la majina yao kutoandikwa gazetini, walisema kuwa wao wanalinda vibarua vyao lakini hali ya barabara ni moja ya kikwazo kikubwa.

“Tunabeba vinywaji, vikivunjika tunahesabiwa hasara sisi wakati
mivunjiko hiyo inatokana na kugongana kwa vinywaji gari zinapoyumba tunapokwepa mashimo yah ii barabara” walisema baadhi ya madereva hao.

Hata hivyo, uchunguzi umebaini kuwa mbali na barabara hiyo kuwa mbovu, viwanda vilivyopo eneo hilo vinakabiliwa na tatizo la ukosefu wa umeme wa uhakika na serikali kushindwa kulinda soko la ndani ambapo bidhaa nyingi zinaingizwa nchini na kuuzwa bei sawa na zinazozalishwa katika viwanda vya ndani.

No comments: