Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Tuesday, January 03, 2017

KIWANDA CHA NAFAKA IRINGA CHAHITA ZAIDI YA BILIONI 6

Na Gordon KalulungaKiwanda cha kukoboa na kusagisha unga, National Milling Co-operation (NMC) Iringa, kilichofunguliwa rasmi kwa ajili ya kuanza uzalishaji Julai 6, 1976 na aliyekuwa Rais wa Msumbuji, marehemu Samora Machel na kusimamisha uzalishaji mwanzoni mwa miaka ya 90, kinahitaji shilingi zaidi ya bilioni 6.8 ili kukiboresha.Baada ya kusimamisha uzalishaji kwa miaka mingi, April, 2011 serikali iliamua kukikabidhi kinu hicho kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania (CPB).Kinu hicho chenye kiwanda cha kusaga unga, kina vihenge virefu vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 13,500 za nafaka, na maghala mawili yenye uwezo wa kuhifadhi tani 3,500 za nafaka na tani 1,100 za unga.Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Elimpaa Kiranga anasema Bodi hiyo imeingia mkataba na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula itakayokuwa mzalishaji mkuu wa unga huo.Kiranga anasema, ili kuboresha shughuli zitakazofanywa katika kinu cha Iringa wanahitaji mtaji wa uwekezaji wa zaidi ya Shilingi Bilioni 6.8.
Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula, Abdillah Nyangasa naye anasema tayari wanazo tani 10,000 za mahindi zitakazotumika kama mtaji wa kuanzia kuzalisha unga huo.Anasema unga huo utakaouzwa kwa bei rahisi ikilinganishwa na viwanda binafsi utasambazwa katika mikoa mbalimbali nchini, huku mikoa ya Lindi na Mtwara yenye mahitaji makubwa ya bidhaa hiyo ikipewa kipaumbele.Hata hivyo, tayari kiwanda hicho kimeanza kufanya kazi chini ya bodi hiyo kikiwa na mashine zote za zamani ambazo bado zina ubora na zinamudu kazi.Ubora wa unga wa kiwanda hichoAfisa ubora wa kiwanda hicho, Karungi Gotifrida, anasema kwa sasa wameanza na uzalishaji wa unga wa ugali maarufu kama dona bora.“Watu wengi hawataki dona kwasababu huko mitaani unga unaoitwa wa dona mahindi yake yanakuwa hayajasafishwa ipasavyo hata kutolewa mawe na vumbi, tofauti na dona ambayo tunazalisha hapa CPB.” alisema Karungi.Anaeleza kuwa ili kujitofautisha na viwanda vingine binafsi vinavyozalisha unga, wao wakinunua mahindi kwa wakulima wanayahifadhi mahali salama kisha wanapotaka kuyakoboa na kuyasaga, wanayapeleka kwenye mashina ambako wanapuliza vumbi.“Baada ya kuyapuliza vumbi/taka ngumu na kutoa mawe, tunayachukua mahindi hayo na kuyaloweka kwa muda usiopungua saa nane na kuyatoa kwa ajili ukoboaji. Kuloweka mahindi kunafanya kama kulikuwa na mahindi yaliyohifadhiwa kwa dawa, kufyonzwa dawa hiyo na katika ukoboaji huwa mashine haipasui mahindi kama mashine zingine huko uraiani, tunatoa ganda la nje tu katika mahindi ndipo tunasaga mahindi yakiwa na Protini yake,” anasema afisa ubora huyo.Anasema upasuaji wa mahindi kama wafanyavyo wasagishaji wengine huondoa vitamin yote ya mahindi hayo na kutupwa katika pumba na ndiyo maana mifugo inanenepeana kwasababu inakula chakula bora kuliko binadamu, hali ambayo mashine za kiwanda chao haziruhusu kupasuliwa kwa muhindi.

Masoko.Afisa masoko wa kiwanda hicho, Evance Mwanibingo, anasema kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha tano 60 za unga ingawa kwa sasa kinazalisha tani 20 na wanaendelea kufanyia marekebisho baadhi ya mashine.“Kingine kinachotutatiza katika kuongeza uzalishaji ni uhakika wa soko la bidhaa zetu, maana hatuwezi kuzalisha mzigo mkubwa kabla ya kuwa na uhakika wa soko”, anasema Mwanibingo.Anasema unga huo kwa sasa una soko kubwa katika mikoa ya Iringa, Dar es Salaam, Tanga  na Dodoma na wana mpango wa kuuza unga huo katika shule za bweni kote nchini na kwa kuanzia masoko tarajali kwao ni mkoa wa Mbeya, Njombe, Morogoro, Lindi na Mtwara.“Kutokana na ukweli kuwa kiwanda hiki ni cha serikali, bei yetu ni ndogo kuliko bei za viwanda vya watu binafsi ambapo kwa sasa mfuko wenye ujazo wa unga kilogramu 5 tunauza kwa Shilingi elfu tano (sh. 5,000), Kilogramu 10 tunauza Shilingi elfu kumi (sh. 10,000/= na Kilogramu 25 tunauza Shilingi elfu Ishirini na tatu (sh, 23,000/=) badala ya shilingi 25, 000 kama viwanda vya watu binafsi.Anasema licha ya kuzalisha unga na kuuza, pia wanazalisha pumba zaidi ya tani 15 ambayo nayo ni bora kuliko pumba ya viwanda au mashine za uraiani kwasababu pumba yao ina mchanganyiko na mahindi ambayo ni dhaifu yanayotokana na kuchambuliwa kutoka kwenye mahindi yenye afya ambayo yanasagwa kwa ajili ya chakula cha binadamu.UmemeKuhusu nishati ya umeme wameeleza kuwa kwa sasa katika kiwanda hicho hawajapata tatizo lolote la nishati hiyo.Waziri wa Nishati na madini, Prof. Sospeter Muhongo, alipoulizwa jinsi gani serikali imejipanga kwa ajili ya upatikanaji wa nishati hiyo katika kuelekeza uchumi wa kati kupitia viwanda,  alisema serikali imejipanga vema.“Ndugu yangu, fuatilia hotuba yangu ya bajeti… umeme vijijini… miradi ya kihistoria kwa mara ya kwanza tunazo zaidi ya shilingi trilioni moja. TANESCO miradi mipya ya power generation na transmission.” Anasema Waziri Prof. Muhongo.Ajira.Kwa upande wa ajira, afisa wa fedha wa kiwanda hicho, Imani Mwakaje, anasema mpaka sasa waajiriwa katika kiwanda hicho ni watu watano ambao ni yeye, Afisa Masoko, Meneja, Afisa manunuzi na afisa ubora huku vibarua wakiwa 28.Kilimo.Wakati Serikali imeamua kukifanya kiwanda hicho kama soko la mahindi kwa wakulima wa kanda ya Nyanda za juu kusini, Hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula mifugo na uvuvi ya mwaka 2016/2017 inaeleza kuwa ukuaji wa sekta ya kilimo mwaka 2015 ulipungua kufikia asilimia 2.3 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 3.4 katika mwaka 2014.Aidha, akizungumza katika ufunguzi wa maonyesho ya wakulima kanda ya Nyanda za juu kusini maarufu kama Nane Nane, ndani ya Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya, Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Charles Tizeba alisema Halmashauri nchini hazijakipa kipaumbele Kilimo.“Nimegundua hilo baada ya kufanya ziara katika wilaya ya Mbozi mkoa wa Songwe. Wenyeviti wa Halmashauri na Wenyeviti wa CCM toeni ushawishi wa kuendeleza Kilimo.” alisema Waziri Dkt. Tizeba.Changamoto inayokikabili kiwanda hicho ni upatikanaji wa masoko wa bidhaa inayozalishwa na upungufu wa magari kuwafikia wateja, huku kikiwa na matarajio ya kuzalisha zaidi na kukifanya kiwanda hicho kama soko la mazao ya wakulima.
Mbali na kiwanda hicho kusimamiwa na bodi hiyo, vinu vingine vinavyosimamiwa na bodi hiyo ni pamoja na cha Arusha, Mwanza, na Dodoma.Mwananchi Anna Sekalinga, anasema haoni faida ya kiwanda hicho kwa jamii inayokizunguka bali anaona kimefufuliwa kwasababu za kisiasa tu.


Naye Mariam Mkolwe anasema hata ajira hawajaziona na hakigusi maisha yao moja kwa moja.


Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alipoulizwa kuhusu manufaa ya kufufuliwa kwa kiwanda hicho kwa wananchi alisema kuwa wakulima wataongeza kipato kupitia mazao yao hasa Mahindi na kwamba ajira za vibarua pia zitaongezeka.


“Pia maghala yaliyo jengwa na halmashauri yatatumika ipasavyo

Ismani, kihorogota , Itunundu, idodi na nina kata 28 vijiji 133 iringa DC, Manispaa kata 18,” alisema Kasesela.


Mkuu huyo wa wilaya, alisema changamoto kubwa ni mtaji mdogo Kwa kiwanda inayowafanya wawe na hofu ya kuhamasisha wakulima.


“Bodi haina fedha nyingi kununua mazao. Bodi iruhusiwe kuuza bidhaa hii nje ya nchi mfano malawi, Zimbabwe nk nchi hizi zina uhaba wa chakula kwa kufanya hivyo mtaji utaongezeka. Wakulima wana mazao mengi hawana pa kuyauza” alieleza Mkuu huyo wa wilaya.

No comments: