Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Sunday, March 19, 2017

MIMBA ZA UTOTONI ZAONGEZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO MBEYA Mratibu wa Vijana kutoka Shirika la Marie Stopes, Daniel Emmanuel akizungumza katika tamasha la vijana Mbeya ambalo lilifanyika jana katika eneo la Soko la Kimataifa la Mwanjelwa jijini Mbeya.

Na Venance Matinya, Mbeya.

UTAFITI wa mwaka 2010 unaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 23 ya wasichana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 19 walipata mimba na mwaka 2015 idadi iliongezeka na kufikia asilimia 27.

Hayo yameelezwa jana na Mratibu wa kitengo cha uzazi wa Mama na Mtoto mkoa wa Mbeya Prisca Butuyuyu wakati wa ufunguzi wa tamasha la vijana lililoandaliwa na Taasisi ya Marie Stopes Tanzania na kufanyika katika viwanja vya Soko la kimataifa la Mwanjelwa jijini Mbeya.

“Mwaka 2016 Mkoa wa Mbeya pekee ulilipotiwa kuwa na vifo 94 vya wajawazito na kati yao 27 sawa na asilimia 31 walikuwa ni wasichana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 vifo ambavyo vilisababishwa na kuishiwa damu, kifafa cha mimba, maralia na vichomi.”

“Visababishi vya vifo hivyo kwa vijana ni kutokana na aibu ya kuficha mimba na kusababisha kukosekana kwa huduma na wengine kukimbilia kutoa bila kutumia njia sahihi hivyo kupelekea kupoteza maisha” alisema Butuyuyu.

Katibu tawala wa Mkoa wa Mbeya Mariam Mtunguja akifungua tamasha la vijana Mbeya ambalo liliandaliwa na taasisi ya Marie Stopes ya Jijini Dar es Salaam na kufanyika jana katika eneo la Soko la Kimataifa la Mwanjelwa jijini Mbeya..

 Akifungua tamasha hilo, Katibu tawala wa Mkoa wa Mbeya Mariam Mtunguja alisema mkoa huo unakabiliwa na hatari kubwa ya kuongezeka kwa vifo vya akina mama na watoto wachanga na ongezeko la maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kutokana na kupitiwa na barabara kuu inayounganisha nchi za Zambia na Malawi.
  
Mtunguja alisema wageni hao wakati wa mapumziko wanatumia muda mwingi kuwarubuni vijana hasa wasichana na hatimaye kuwaambukiza VVU na kuwapa mimba katika umri mdogo.

Alisema utafiti uliofanyika hivi karibuni ulibaini kuwa vijana wenye umri kati ya miaka 13 hadi 24 Tanzania asilimia 3.3 wana VVU, Mkoa wa Mbeya pekee ni asilimia 6.3 hali inayoashiria Mkoa huo kuwa katika hatari kwa vijana wadogo.

“Utafiti uliyofanyika mwaka 2015 unaonesha kuwa vijana wa kike wenye umri kati ya miaka 15 hadi 19 asilimia 33 nchini walipata ujauzito na wengine kujifungua ili hali Mbeya ni asilimia 36” alisema Katibu tawala huyo.


Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Zacharia Nachoa akizungumza katika tamasha la Vijana jana eneo la soko la Mwanjelwa jijini humo.

Kutokana na hali hiyo vifo vya akina mama na watoto wachanga vinaongezeka vikichangiwa na wasichana wengi wanaobeba mimba kabla viungo vyao kukomaa na kuwa na uwezo wa kuhimili ujauzito.


Kwa upande wake Mratibu wa Vijana kutoka Shirika la Marie Stopes, Daniel Emmanuel alisema tamasha hilo lililenga kuwafikia vijana wengi ili kuwapa elimu ya afya ya uzazi, ushauri kuhusu maambukizi ya Ukimwi na ukatili wa kijinsia.

“Walengwa ni vijana wote walioko katika shule za Sekondari, vyuoni na wanaojishughulisha na biashara mbalimbali walio na umri kati ya miaka 15 hadi 24 kwa kuwa ni kundi lililo kwenye hatari zaidi ya kukumbwa na mimba za utotoni na maamukizi ya virusi vya Ukimwi” alisema Daniel.

  
 Baadhi ya wanafunzi ambao walihudhuria tamasha hilo jana.

 Wanafunzi wakifuatilia mada kutoka kwa viongozi ambao walihudhuria tamasha la vijana jana eneo la Mwanjelwa Jijini Mbeya jana.


Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 inalenga kuhakikisha kwamba watoto wote wanastawi na kuwa na maisha bora, kutokana na kupatikana kwa haki zao za msingi ambazo ni kuishi, kuendelezwa, kulindwa na kushirikishwa katika mambo yanayowahusu bila ua ubaguzi wa hali yoyote. 

Kwa mujibu wa sera hiyo, mtoto ni yule mwenye umri wa chini ya miaka 18. Mtu yeyote mwenye umri wa chini ya miaka 18 anastahili kulindwa na familia yake pamoja na wanajamii wanaomzunguka ili kumuangalia ukuaji wake uwe wenye usalama zaidi.
 
 Madhara ambayo anaweza kuyapata mtoto kama hajapata uwangalizi kutoka katika familia yake na jamii inayomzunguka ni, kuathirika kiafya, kiakili, kimwili, kihisia na kijinsia.

No comments: