Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Sunday, March 05, 2017

TPDC; GESI ASILI IMEPUNGUZA ADHA YA KUKATIKA UMEME TANZANIA

SHIRIKA la maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema kuwa gesi asili iliyogundulika na kuanza kuchimbwa mkoani Mtwara kusini mwa Tanzania, imepunguza adha ya kukatika kwa umeme kwa kiasi kikubwa.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mjiofizikia wa shirika hilo kutoka idara ya mkondo wa juu Fausta Kayombo, alipokuwa akitoa elimu ya gesi hiyo kwa waandishi wa habari wanaofanya kazi katika mikoa ya kanda ya Nyanda za juu kusini, walipokutanika katika ukumbi wa mikutano wa Mkapa Jijini Mbeya.

 Alisema watanzania wengi wanahoji faida ya gesi hiyo kutokana na kutonufaika moja kwa moja lakini ukweli ni kwamba faida ipo kubwa na zaidi ya asilimia 50 gesi hiyo inatumika katika kuzalisha umeme.

“Awali tulikuwa tunategemea maji kuzalisha nishati ya umeme, lakini kwa sasa zaidi ya asilimia 50 tunatumia gesi kuzalisha nishati hiyo ndiyo maana tatizo la kukatikakatika kwa umeme siku hizo kumepungua sana” alisema Kayombo.

Alisema gesi hiyo inatumika pia kwa kupikia lakini kupitia mfumo wa mabomba tofauti na gesi ambayo inatoka nje ya nchi ambayo inasindikwa kwenye mitungi inayotumika kwa sasa na kwamba watakaoweza kufikiwa na gesi asili majumbani mwao watatumia kwa bei nafuu kuliko gesi iliyopo sasa.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbeya William Ntinika, alisema ili jamii iweze kupata uelewa juu ya masuala ya gesi asili ni vema waandishi wa habari wakaeleweshwa vema ili nao waweze kuufikishia umma taarifa sahihi.

Hata hivyo katika majadiliano na waandishi wa habari, baadhi ya waandishi wa habari walisema ipo haja ya elimu waliyoipata iwafikie pia wakuu wa wilaya, wakuu wa idara katika Halmashauti na wanasiasa kwasababu baadhi yao wanakataza wananchi kutumia mkaa kwa madai kuwa gesi asili ipo jambo ambalo ni upotoshaji kwasababu mpaka sasa watanzania wasiozidi 200 kati ya Watanzania zaidi ya Milioni 40 pekee ndiyo waliofikishiwa mabomba ya gesi hiyo asili kwa ajili ya matumizi ya kupikia.

No comments: