Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Wednesday, April 26, 2017

Sauti ya Nyikani; Je Taifa limepatwa na ukichaa?

Na Gordon Kalulunga

MIAKA ya nyuma kidogo, Mkoani Mbeya katika Jimbo kuu Katoliki
kulikuwepo Padre aliyeitwa Emily Shitundu, ambaye alikuwa na elimu
kubwa ya masuala ya dini ambapo alikataa kuwa chini ya Askofu wa Jimbo hilo James Sangu (kwa wakati huo).

Wote hao kwa sasa ni marehemu. Shitundu alipokataa
kuwa chini ya Askofu Sangu, aliamua kuasi kanisa na kuanzisha madhehebu kadhaa na kufanya mambo mengine ya kidunia lakini mwisho wa yote alirudi katika kanisa lake Mama na kutubu.

Akitubu mbele ya Askofu Sangu alitamka sala ambayo kwa Wakristo wengi wanaijua ambayo inasema ‘’Baba yetu uliye mbingu,…….utusamehe makosa yetu….’’

Baada ya kutubu na kuomba radhi ndipo aliruhusiwa kuhubiri katika madhabahu na mara nyingi akianza kuadithia mapito yake, alikuwa akiishia kulia na kububujikwa na machozi mpaka mwisho wa maisha yake.

Mfano huu nauona kama mwanga na Nuru inayoweza kuwaka kwa taifa letu la Tanzania ambalo misingi yake ya kiuchumi inajieleza kama nchi ya msingi wa ujamaa na kujitegemea, ingawa kwa sasa tunaishi kibepari na ujamaa kwa mbali.

Hali hii ni moja ya (uasi) na itafikia hatua huko tuendako tutaishia kulia katika maisha yetu yote na kububujikwa na machozi sisi na vizazi vyetu kutokana na uasi ambao tumeamua kuufanya na kuondoka katika misingi ya ujamaa na kujitegemea kwa kisingizio kuwa tunakwenda na wakati (Utandawazi-Utandawizi).

Leo hii tumekuwa kama taifa ambalo limepatwa na ukichaa, siioni misingi ya sisi kama Taifa kuwa tunaishi nini! Yaani tunaishi kwa falsafa ipi?

Tunaishi mchanganyiko, kama ni chakula basi ni chakula ambacho kimechanganywa na mchanga ili mradi tuna njaa, basi tunalazimika kula, kila mtu anaishi kivyake, kila kiongozi anasema lake, kila mpiga kura anasema lake, mladi liende.

Kuna mifumo mitano ya uchumi na utawala duniani, mfano nchi ya china inaishi na falsafa ya ujamaa na kujitegemea, huo ndiyo moyo wa nchi hiyo.

Mifumo hiyo mitano ni Ujima (Primitive Communalism), Ukabaila (Feudalism), Utumwa (Slavery), Ujamaa (Socialism) na Ujamaa uliotopea au uliokomaa (Communism).

Kulingana na mifumo hii, kila mfumo una namna yake ya utawala na uzalishaji mali kulingana na nyakati. Mfumo wa ujima ambao ndio unaaminika kuwa wa kwanza pale mwandamu alipoanza kuishi pamoja, jamii yote iliishi kwa kutegemeana bila kuwa na matabaka. Wote walifanyakazi na kugawana mali bila upendeleo bila kujali nafasi ya vyeo wala umri, jinsi ama jinsia.

Katika mfumo huu swala la utawala halikuwa kitu bali umoja wa jamii
husika na maendeleo yake.

Mambo ni tofauti katika mfumo wa pili wa ‘Ukabaila’ ambapo ardhi ndiyo mama wa utawala na nguvu. Kutokana na hali hii hapa ndipo dhana ya utawala na mtawaliwa inapoibuka.

Kulingana na mfumo huu, mwenye ardhi ndiye mtawala na asiyekuwa na ardhi ndiye mtawaliwa. Hapa tunapata lugha ya ‘Bwana’ na ‘Mtwana’.

Dhana nyingine tena inaibuka ya mtawala na mpinzani wa utawala, japo kuwa katika hatua hii hakuna vyama vya siasa bali watu na ardhi.

Mfumo huu dhahili umejaa unyonyaji kati ya matabaka haya mawili.
Tabaka tawala na tawaliwa. Hapa inamaanisha mwenye ardhi na asiye kuwa na ardhi.

Mwenye ardhi anataka kulinda ardhi yake kwa udi na uvumba na asiyekuwa nayo naye anatafuta kwa udi na uvumba. Hapa nieleweke vizuri, mwenye ardhi ndiye mtawala, hivyo asiyekuwa na ardhi naye akiipata pia atakuwa mtawala.

Mfumo unaofuata ni ule wa utumwa (slavery) hapa cha msingi ni watumwa ambao kazi yao kubwa ni kuwatumikia mabwana hivyo nao unaibua misamiati ya mabwana na watumwa.

Siku zote katika mfumo huu ni kuona mabwana (watawala) wakiwanyanyasa, wadhulumu, wadharau, na kuwafanyisha kazi watumwa kwa maslahi yao. Hapa napo dhana ya utawala na upinzani inaibuka tena.

Bwana huhakikisha kuwa ana mdhulumu mtumwa haki zake kwa gharama yeyote. Na kwa upande wa mtumwa naye hutafuta njia ya kujiokoa katika mateso na maonevu hayo.

Kama akibahatisha kujitoa katika mateso na dhuluma hizo, naye hugeuka kuwa bwana (mtawala) na kumiliki watumwa.

Katika mfumo huu tunapata hisia kuwa hakuna mtumwa ambaye anaweza kutawala! Bali mtawala ni bwana tu.

Mfumo wa nne ni ujamaa (socialism). Mfumo huu si mgeni kwa watanzani. Ni mfumo uliodumu kwa takribani miaka 27 tangu 1965 hadi kifo chake 1992.

Misingi ya mfumo huu ni umoja katika uzalishaji mali na mgawanyo sawa wa kazi miongoni mwa jamii. Mfumo huu unafananishwa sana na mfumo wa ujima, lakini tofauti iliyopo ni kuongozwa na chama cha siasa na watawala (viongozi wa chama na serikali).

Watawala huwa na uwezo wa kusimamia masuala mbalimbali yanayoihusu jamii hiyo. Kutokana na imani na misingi ya mfumo huu, mara nyingi huamini katika mfumo wa chama kimoja kutawala dhidi ya vyama vingi vya siasa.

Uzalishaji mali katika mfumo huu ni kwa serikali kumiliki njia kuu za uchumi (centralized economy). Hapa sasa ndipo unaweza kuona kila mtu katikam fumo huu analazimika kufuata maagizo ya chama tawala na viongozi wake hata kama hataki.

Mawazo mbadala ya watu, huwa hayapewi nafasi mpaka kamati za chama na watawala wa juu waamue. Katika mfumo huu chama pinzani hakipo na wapinzani hawapo. Hivyo chama tawala ndiyo ‘tawala’.

Mfumo wa mwisho ni ujamaa uliotopea (komaa). Mfumo huu hauna tofauti sana na mfumo wa ujamaa. Tofauti ni kwamba hapa ujamaa umepea na nchi imekuwa na uchumi imara na inaweza kujiendesha bila kutegemea misaada kutoka nje. Hali ya mambo ya kiutawala haina mabadiliko na mfumo wa ujamaa.

Kama taifa sasa, inatupasa tuishi kwa falsafa, maana falsafa ndiyo moyo wa nchi, mimi falsafa yangu kutoka hapa nyikani ni kwamba mwanaume kama ameshindwa kuishi kama mwanaume, basi atakufa kama mwanamke, ndiyo maana nauliza kuwa je tumepatwa na ukichaa?

Ili tufanikiwe kimaendeleo, ni lazima tuanze sasa kufikiria zaidi
tunayoyataka badala ya kufikiria zaidi mambo ambayo hatuyataki.
Karibuni Nyikani, Gordon Kalulunga, fimbo ya Mussa.

No comments: