Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Monday, May 29, 2017

PEMBEJEO FEKI ZAWALIZA WAKULIMA MBEYA

Aliyewahi kuwa Mbunge wa jimbo la Mbeya kwa miaka 15 mzee Patrick Nswilla akiwa na Mwandishi wa habari hii Gordon Kalulunga vijijini Iwindi jimbo la Mbeya Vijijini mwishoni mwa juma.


*Jinai hiyo ipo tangu mwaka 2004
*Hakuna anayejali, rushwa yahusishwa

NA GORDON KALULUNGA

WAKULIMA wa zao la Kahawa wilaya ya Mbeya wamelalamikia uzagaaji wa pembejeo feki katika maduka mbalimbali wilayani humo zinazoathiri mazao yao.

Hayo waliyasema mwishoni mwa juma katika mkutano mkuu wa chama cha ushirika Usongwe AMCOS uliofanyika katika ofisi za chama hicho zilizopo Kijiji cha Iwindi wilayani humo.

Akichangia hoja katika mkutano huo, mkulima Julius Mzumbwe, alisema kuwa inashangaza kuona uongozi wa chama hicho unawauzia pembejeo kwa ongezeko la Shilingi 500 tofauti na gharama wanayouza katika maduka ya watu binafsi.

Akijibu hoja hiyo, Katibu msaidizi wa ushirika huo Godfrey Mwakalonge alisema kuwa hali hiyo inatokana na uendeshaji pia pembejeo wanazowapatia zinakuwa hazina shaka katika ubora wake.

“Ndugu zangu wajumbe, mbali na gharama za usafiri, upakiaji, upakuaji na ugawaji, lakini tunazingatia ubora wa pembejeo tofauti na kuzinunua kwenye maduka kama mnavyokumbuka tumewahi kununua pembejeo kwa akina Kalinga Agro yaliyotukuta sote ni mashahidi kumbe Coper walituuzia matofali” alisema Mwakalonge.

Akikazia jawabu hilo, Mwenyekiti wa bodi ya ushirika huo Jailos Mwashigala alisema mbali na pembejeo nyingi madukani kuwa feki, pia wafanyabiashara wanapunguza ujazo kwa kila pembejeo zikiwemo mbegu dawa mbalimbali.

“Mkitaka kujua zaidi waulizeni wakulima wa vijiji vya Shongo na Holongo Kata ya Igale hao wanajua zaidi athali za kununua pembejeo katika baadhi ya maduka ya pembejeo hasa yaliyopo Mbalizi” alisema Mwenyekiti huyo.

Mbunge wa kwanza wa jimbo la Mbeya aliyetawala kwa miaka 15, ambaye pia ni mwasisi wa chama hicho cha ushirika mwaka 1968 Patrick Nswilla ambaye alihudhuria pia mkutano huo aliwaambia waandishi wa habari kuwa pembejeo feki zinazidi kushamiri wilayani humo kutokana na vitendo vya rushwa.

“Tangu muda mrefu wakulima wanalalamika maana wafanyabiashara huwa wanasaga matofali ya kuchomwa na kuyaweka kwenye mifuko wakiuza kama Copper huku unga huo wa matofali wakipaka mahindi na kuziuza kama mbegu bora” alisema Nswilla.

Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini Oran Manase  Njeza alipoulizwa kama anafahamu kadhia hiyo alisema kuwa kosa hilo ni la jinai na amewataka wakulima ambao wanapata matatizo hayo wayapeleke Polisi ili hatua ziweze kuchukuliwa.

“Kuwepo  kwa pembejeo feki ni kosa la jinai. Hiki ni kilio Tanzania nzima na wabunge wote tumeendelea kupiga kelele” alisema Njeza.

Mwandishi wa habari hizi aliutafuta uongozi wa Kampuni ya Kalinga Agro ya mjini Mbalizi ili kutolea ufafanuzi wa tuhuma zilizotolewa katika mkutano huo, ambapo Meneja wa oparesheni ..………. Alisema tuhuma hizo wamezipata mara kadhaa lakini wao hawahusiki na kama kuna mkulima mwenye malalamiko aweze kujitokeza akiwa na stakabadhi wanazotoa.

Ofisa ushirika wa wilaya ya Mbeya ambaye alihudhuria na kusimamia pia mkutano huo alisema kuwa anampongeza Rais Dkt. John Magufuli kupitia wizara ya Kilimo kwa kufuta baadhi ya tozo kutoka kwa wakulima wa zao hilo la Kahawa kutoka tozo 27 ikiwemo tozo ya mfuko wa maendeleo na tozo ya utafiti na kubakiwa na tozo 9.

Mwenyekiti aliyesimamia Mkutano huo Mwalimu Yangson Mwanjowe, aliwashukuru wana ushirika wenzake kwa kuweza kufikia muhafaka katika mambo mbalimbali na kufikia maazimio ya pamoja ya kila mkulima kuandaa Kahawa safi.
Hata hivyo, uchunguzi wa kina uliofanywa na Mwandishi wa habari hii umebaini kuwepo kwa dawa feki za kuhifadhia nafaka hasa mahindi na maharage.

Wafanyabiashara hao, ambao baadhi yao kwa sasa hawakamatiki kutokana na utajiri walioupata kwa njia hiyo, wamefikia hatua ya kusaga matofali yaliyochomwa  kisha unga wake kuhifadhiwa kweye mifuko kama dawa za kuulia wadudu wanaoharibu mimea na matunda ya Kahawa.

Dawa aina ya Red Copper baadhi ya wafanyabiashara wanauza kwa ujanja unga wa matofali ya kuchomwa kisha kuweka unga huo kwenye mifuko na kuuza kwenye maduka yao huku Copper ya kuhifadhia mbegu za pamba wanauza kama Copper ya kutibu magonjwa ya kahawa aina ya CBD.

Copper hiyo wakulima wakiikoroga kwenye maji inatuama chni ya chombo kwasababu siyo Copper halisi ya kuchanganya na maji lakini wengi wanaitumia kwasababu ni bei rahisi na hawana elimu ya kutosha kuhusu dawa hizo.

Kwa upande wa mbolea, wanachukua mbolea aina ya minjingu ya punje na kuweka katika mifuko ya DAP kwani DAP ina bei kubwa kuliko minjingu.

Wanafanya hivyo kwasababu mkulima anapotumia mbolea hiyo hawezi kugundua mpaka pale mazao yatakapokuwa yameanza kuharibika yakiwa shambani.

Mbegu za mahindi, wamekuwa wakichukua mahindi ya kawaida na kuyachanganya na Copper ya kuhifadhia mbegu za pamba na Copper ya kawaida kisha kuhifadhi kwenye mifuko ya makampuni ya utafiti na kuwauzia wakulima.

Mtaalam wa masuala ya pembejeo kutoka kampuni ya Bager, Alex Swilla anathibitisha kuwepo kwa mchezo huo mchafu kwa muda mrefu huku serikali ikiendelea kufumbia macho.

Anasema mbali na mbolea na mbegu hizo kuchakachuliwa, wafanyabiashara hao pia wanachakachua na sumu ambapo jina la sumu linalokuwepo kwenye kopo ni tofauti na dawa inayokuwemo ndani.

“Kwa upande wa sumu, wanachukua dawa aina ya Sumision na kuweka katika makopo ya sumu aina ya Daksban’’alisema Swilla.

Alisema hali hiyo imeendelea kushika kasi kutokana na mambo mawili, likiwemo suala la rushwa kwa wakaguzi au wakaguzi hao kutokagua kabisa maduka ya pembejeo hizo za kilimo ama kukaa muda mrefu bila kufanya ukaguzi hali ambayo inawapa mwanya wafanyabiashara hao kuendelea na mchezo huo.

Mwaka 2013, askari wa jeshi la polisi mkoani Mbeya walimkamata Jofrey Mbago mkazi wa Chimala wilayani Mbarali akiwa na mifuko 100 ya mbolea aina ya CAN ikidhaniwa kuchakachuliwa ikiwa katika mifuko yenye nembo ya kampuni ya Premium Agro Chem Ltd ya Jijini Dar es Salaam.

No comments: