Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Saturday, May 06, 2017

SAUTI KUTOKA NYIKANI; Wakipata ajali kama zetu wataokoa maisha yetu

NA GORDON KALULUNGA

RIPOTI ya kwanza kutolewa na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) kuhusu hali ya dunia katika usalama wa barabarani, watu milioni 1.3 hufa kila mwaka na kati ya milioni 20 na 50 hupata majeraha makubwa katika ajali.

Na kwa mujibu wa takwimu hizi juu ya ajali hizo, Tanzania inakadiriwa kuwa na watu takriban milioni 40.4 na inapoteza watu (wanaoripotiwa) 34.3 katika kila watu 100,000 kutokana na ajali za barabarani.

Hii si idadi ndogo hata kidogo na hasa ikizingatiwa kuwa asilimia kubwa ya ajali hizi zingeweza kuepukika kama serikali ingeweka mkakati mzuri wa kukabiliana na tatizo hili.

Mafunzo ya imani yanatufundisha ama kutuelekeza kuwa binadamu wote ni sawa.

Ni kuwa licha ya tofauti zetu za mali, rangi, imani, pesa, kimo, kabila nk bado tu-sawa na tunao uhai ulio sawa.

Wakati tunatambua jambo hilo, lakini si kwa watawala wetu.

Tumejengewa tofauti kubwa sana kati ya uhai wa mtawala na uhai wa sisi watu wa nyikani. wajiitao viongozi, uhai wao umeonekana kuwa na thamani sawa na makumi, mamia na ama maelfu ya wananchi wanaowaongoza.

Kifo cha kiongozi ni kifo, lakini kifo cha mwananchi asiye kiongozi ni takwimu (hata kama wote wamekufa kwa sababu inayofanana).

Ndio maana awapo kiongozi hata shughuli za nchi zitasimama, japo ili zisimame kwa mwananchi, lazima liwe janga la kitaifa.

Na ndio maana thamani ya mwananchi wa kawaida inaonekana hasa wakati wa uchaguzi, ili waweze kuwavusha wanaotaka kuwa watawala.

Tumeshuhudia namna ambavyo watawala wa nchi mbalimbali wanavyotumia maelfu ya maisha ya wananchi wao kukinga nafasi na maisha yao.

Nalisema jambo hili kwasababu kuna siku nilidokezwa kazi za walinzi wa viongozi, sihitaji kumwaga mchele kwenye ukurasa huu.

Tatizo la ajali kwa nchi yangu ya Tanzania si tatizo la jana wala juzi. Si tatizo ambalo tunaona likipata unafuu wowote na hasa siku ama nyakati hizi ambapo wasafiri huongezeka, wenye magari kutamani pesa zaidi na wenye mamlaka ya kusimamia sheria za barabarani "Kuchuma" zaidi.

Wananchi kutamani zaidi kufika ilhali wakipuuza njia sahihi za kuwafikisha huko nk. Yote juu ya yote, nyakati hizi usalama kupuuzwa na akili kuwekwa kwenye pesa na muda.

Baada ya ajali ya kule mkoani Mara, iliyohusisha magari mawili ya abiria na watu zaidi ya 35 kupoteza maisha, Waziri wangu Dr. Harrison Mwakyembe, alitoa tamko la kuyafungia makampuni ya mabasi hayo na kutangaza kuwepo msako wa ukaguzi wa vyeti vya madereva na leseni zao..

Kwa baadhi ya sisi watu wa Nyikani haiingii akilini kama hiyo ni dawa, vyeti wanavyo, leseni wanazo, tena nzuri, lakini ukaguzi wa magari je upo vizuri? Au magari mengi yanapendeza kutokana na uzuri wa rangi kama makaburi ili hali ndani ya kaburi kuna maiti?

Imekuwa kawaida sasa kwa serikali yetu, kutoonyesha kuwa na mikakati madhubuti ya kupunguza na pengine kufuta ajali za kizembe, bali kitakachofuata ni salamu za rambirambi toka kwa viongozi.

Niseme wazi kuwa, tumechoshwa na salamu za rambirambi za ajali zitupatazo. Kinachokera zaidi ni kwamba salamu nyingi zinaambatana na onyo kali huku watendaji wakitakiwa kuhakikisha ajali zinapungua.

Lakini hakuna tofauti. Kwenye salaam zake za mwanzoni mwa mwaka 2009, Rais Jakaya Kikwete alisema "hatuwezi kuvumilia kutokea kwa ajali hizi wakati mamlaka zenye dhamana ya kusimamia sheria za usalama barabarani zipo.

Tufanye jitihada zote zilizo ndani ya uwezo wetu kupunguza kwa kiwango kikubwa na ikiwezekana kukomesha kabisa ajali hizi za barabarani ambazo zimeshapoteza maisha ya wenzetu wengi"

Kupitia Baraza la mawaziri la Rais wetu mpendwa Dkt. John Magufuli, namuomba mmoja wa mawaziri, ajitokeze na kuwa wa kwanza kukabiliana kikamilifu na suala la ajali, na aorodheshe atatenda nini? Vipi na kufikia lini.

"Ni nani atakayechukua jukumu la kushughulikia kuzuia ajali? Je! Ni Wizara ya Ujenzi (Barabara na Uwanja wa Ndege), Wizara ya Uchukuzi (Reli, Bandari, Usafiri Majini) ama Wizara ya Usalama wa Raia? Ama ni wizara gani?)"

Bila kuwa na mikakati inayofaa na endelevu na kutegemea tochi za trafiki wa Iringa ambao wamezigeuza tochi hizo kuwa duka la jumla na reje reja, tunasubiri mvua za ajali ambazo hata tukipona, hatutakuwa kama tulivyokuwa awali. Huko Arusha wanafunzi 29 tunaambiwa leo Mei 6, 2017 wamefariki pamoja na walimu wao wawili.

Hili linanifanya niamini kuwa serikali haioni tatizo la ajali kwa waTanzania mpaka pale litakapowahusisha viongozi, na ndio maana sasa nawatakia viongozi wapate ajali kama zetu ili watatue tatizo letu na kuokoa maisha yetu.

Credit to changamotoyetu blog

No comments: