Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Thursday, May 18, 2017

TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA LEO TAREHE 18.05.2017.Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu.

KUPATIKANA NA POMBE HARAMU YA MOSHI [GONGO]

Mnamo tarehe 17.05.2017 majira ya saa 18:00 jioni, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko katika kivuko cha Magongo Street, Kata ya Ndandalo, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kuwakamata watu watatu wakiwa na Pombe Moshi [Gongo] ujazo wa lita 80.

Watuhumiwa waliokamatwa ni pamoja na:-
1.     AMOS MWAKASAPE [33]
2.     ROSE D/O ITULO [35]
3.     TUMAINI MAKULA [30] wote wakazi wa Tenende Wilaya ya Kyela.

Watuhumiwa walikamatwa wakiwa wamehifadhi pombe hiyo katika madumu 03 ya lita 20 na vidumu vya lita 5 na chupa zinazokadiriwa kubeba lita 10 kila mmoja. Watuhumiwa walikuwa wakisafirisha pombe hiyo kwenda kijiji cha Tenende kwa ajili ya kuiuza. Upelelelezi unaendelea na mara baada ya kukamilika watafikishwa mahakamani.

Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na matukio makubwa ya uhalifu pamoja na wahalifu. Jitihada zinaendelea kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha Mkoa wetu unakuwa mahala salama. Hata hivyo Kumekuwa na tukio 01 la mauaji kama ifuatavyo:-

Mnamo tarehe 17.05.2017 majira ya saa 16:00 jioni huko Kijiji cha Igodima, Kata ya Chokaa, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya. Mwanaume mmoja ambaye hajafahamika jina lake wala anuani yake, anaekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 40 - 45, aliuawa na wananchi walioamua kujichukulia sheria mkononi kwa kumpiga fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia majeraha yaliyopelekea kifo chake.

Inadaiwa kuwa, kabla ya tukio hilo marehemu alikuwa amevunja nyumba mchana na kuiba pesa taslim Tshs 1,500,000/= katika nyumba ya DANEL KILALA, na wakati anakimbizwa kwa lengo la kukamatwa alimjeruhi kwa kumchoma kisu cha tumbo DAUDI KILALA [27] Mkazi wa Igodima na ndipo nae alishambuliwa hadi kuuawa na kundi la wananchi.

Majeruhi amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya  kwa matibabu na mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitalini hapo. Upelelezi unaendelea.

Mnamo tarehe 16.05.2017 majira ya saa 11:00 Asubuhi huko katika eneo la Iwolelo, lililopo Kitongoji cha Kanoge, Kijiji cha Kambikatoto, Tarafa ya Kipembawe, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la NGIKA NG’WANI [55] Mkazi wa Ipenyelo alifariki dunia akiwa njiani kupelekwa Hospitali baada ya kukanyagwa na mnyama pori - Tembo.

Marehemu alikutana na athari hiyo wakati anatokea eneo la mkusanyiko akiwa anarejea nyumbani kwake na ndipo alikutana na Tembo ambaye alimkanyaga na kupelekea kifo chake. Inadaiwa kuwa, marehemu alipoteza maisha kutokana na kutokwa damu nyingi. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya Chunya.

WITO:

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishina wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa wananchi kuacha kutumia Pombe Haramu ya Moshi kwani ni kinyume cha sheria na ni hatari kwa afya ya mtumiaji. Pia anatoa wito kwa wananchi kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi wanapowakamata watuhumiwa kwa tuhuma mbalimbali na badala yake wajenge tabia ya kuwafikisha katika vyombo vya dola watuhumiwa wanaowakamata kwa makosa au tuhuma mbalimbali kwa hatua zaidi za kisheria.

Imesainiwa na:
 [DHAHIRI A. KIDAVASHARI - DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA

No comments: