Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Thursday, June 29, 2017

SAUTI KUTOKA NYIKANI; KACHERO ASEMA VIJANA WASIOPENDA MAKUNDI WATAIUISHA CCM MBEYANA GORDON KALULUNGA

WIKI iliyopita niliahidi kuanza kufanya mahojiano na baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mbeya ambao wanatajwa kuwa wanaweza kufaa kuingia katika kinyang’anyilo cha nafasi ya Uenyekiti wa chama hicho mkoani humo.

Leo tunaanza na Kachero mstaafu wa idara ya usalama wa Taifa (TISS), Said Salimin Said maarufu kwa jina la mzee Salmin, mahojiano ambayo yalidumu kwa dakika 45 mjini Mbeya.

Anasema kwa sasa baada ya kustaafu makazi yake yapo Iwambi ndani ya Jiji la Mbeya ambalo linaongozwa na Mbunge wa jimbo hilo Joseph Mbilinyi (Sugu) na Halmashauri hiyo baraza la madiwani lipo chini ya chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Yafuatayo ni maswali sita kutoka kwa mwandishi na majibu ya kachero huyo anayetajwa kuwania nafasi hiyo ya Chama Cha Mapinduzi.

MWANDISHI: Wewe ulikuwa mtumishi wa umma katika idara nyeti ya serikali na sasa unatajwa kuwa ni mmoja wa wanachama wa CCM ambao wanatajwa kuwa wanatarajia kuwania nafasi ya Uenyekiti wa chama hicho mkoa wa Mbeya. Unapenda nini wakifahamu wana CCM na Watanzania kuhusu wewe hasa kile wasichokijua?

SALIMIN: Awali ya yote nishukuru kwa kupata nafasi ya kuhojiwa maana kuna wengine wananipigia simu kuwa nimetangaza kuwania nafasi hiyo jambo ambalo siyo sahihi maana chama bado hakijatoa utaratibu.

Pili niseme kuwa wana CCM wengi hawajui na kufikiri kuwa mimi ni mtumishi wa serikali wa hivi karibuni. Nimeanza kazi mwaka 1974 na nilikuwa mwanachama wa TANU toka nikiwa kama siyo JKT basi nilikuwa kidato cha Sita.

Pili nilikuwa mwana chama wa CCM mwanzilishi. Ilipokuja kuingia utaratibu wa watumishi wa serikali hasa wa vyombo vya dola, tulitakiwa tusijihusishe na siasa na tusiwe wanachama wa chama chochote.

Hivyo mimi nilitii ile amri nilijivua uanachama lakini siyo kwamba unarudisha kadi, kadi nilibaki nayo kama kumbukumbu. Lakini kumbuka nilizaliwa na nimesoma nikiwa mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi.

Nilipoanza kuwa mikoani tangu mwaka 1978 mkoa wa Dar es Salaam na Mkuu wa wilaya ya Ilala alikuwa Mheshimiwa Jenerali Ulimwengu ambaye pia ni kada wa chama.

Nilipofika mkoa wa Mbeya ndipo uwezo wangu zaidi ulipoonekana hasa Chadema na CCM nilikuwa nikivipa ushauri tangu mwaka 2007 na nimekuwa na mahusiano mema na viongozi na wanachama wa vyama vyote.

MWANDISHI: CCM Mkoa wa Mbeya ina nini cha kujivunia, inakosa nini na nini kikifanyika inaweza kurejesha uimara wake na kuaminika zaidi kwa wananchi?

SALMIN: CCM mkoa wa Mbeya bado inapendwa sana hivyo ni jambo la kujivuni. Lakini inakosa muunganiko wa viongozi na wanachama, chama kimekuwa kama mali ya viongozi hivyo wanachama wa kawaida wanahisi wanapuuzwa maoni yao.

Hali hiyo imepelekea kupoteza Jimbo la Mbeya Mjini kwenda upinzani baada ya wanachama wengi kuhisi kuwa wanapuuzwa maoni yao hasa kwa wagombea wanapojitokeza.

Kinachotakiwa kufanyika kwa sasa ni kuwaunganisha viongozi na wanachama ili kila mmoja aone kuwa chama ni chao kwa kukemea kwa vitendo mambo ya rushwa na makundi.

Makundi yanazaa rushwa na Lowassa alifanikiwa sana kuwatumia vijana na kibaya zaidi mshirika wake mzee Kingunge alikuwa kamanda wa UVCCM Taifa….

MWANDISHI: Kuna wanachama wa CCM wanasukwasukwa kwa hisia kuwa walikuwa na Lowassa hivyo ni wasaliti je wewe una unalizungumziaje jambo hilo

SALMIN: Kwanza mimi naichukia sana mitandao. Lakini ieleweke kuwa mitandao ni rushwa na kuna vijana walijiingiza huko ili kupata rushwa.

Kuhusu suala la Edward Lowassa ifahamike kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli, Benjamin Mkapa, Alhaji Ally Hassan Mwinyi na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pekee ndiyo hawakupata urais kupitia mitandao.

Ni Rais Jakaya Kikwete pekee ndiye alipata urais kupitia mtandao wa Lowassa ambao lengo kubwa lilikuwa ni matamanio ya Lowassa kupata nafasi ile baadae jambo ambalo limeshindikana.

Pia ieleweke wazi kuwa kwa sasa ndani ya CCM kundi la Lowassa ni dogo sana bali kuna makundi mawili hatari kuliko hata la Lowassa ndani ya chama na ngoja leo nisiyataje….

MWANDISHI: Endapo utagombea nafasi unayotajwa kuwa utajitokeza kuwania, kitu gani unatamani kukifanyia chama chako?

SALMIN: Kitu cha kwanza nikuwaambia wanachama ama wajumbe wachague viongozi waadilifu.

Pili nikipata nafasi ya kuchaguliwa ni kuanza kutoa elimu kwa wanachama kuhusu sera na ilani ya chama ili waweze kueneza vema kwa wananchi maana viongozi wengi ndani ya chama na jumuiya baadhi hawafahamu sera za chama na ilani hivyo inawapa shida kuelimisha umma kuhusu mafanikio ya chama chetu.

MWANDISHI: Unatajwa kuwa mmoja wa viongozi wenye mahusiano mema na vijana wa vyama vyote, nini utakifanya kwa vijana?

SALMIN: Nitajitahidi sana kuhakikisha chama kinaongeza wanachama hasa vijana ambao ni muhimu kuwapatia historia ya nchi tulikotoka na mpaka hapa tulipo ili waone ni jinsi gani maendeleo yanavyofanyika maana maendeleo ni hatua kama ya kuzaliwa kwa mtoto mpaka kuwa mtu mzima.

MWANDISHI: Kuna jambo lolote unalikumbuka ambalo unajivunia katika utumishi wako wa umma hasa ulipokaribia kustaafu?

SALMIN: Ndiyo, jambo kubwa ni mahusiano mema na jamii hasa nakumbuka jinsi nilivyoweza kushirikiana na viongozi wa Chadema na viongozi wenzangu wa serikali ya mkoa wa Mbeya kumaliza maandamano na machafuko yaliyowahi kudumu kwa simu mbili mjini Mwanjelwa yakihusisha wamachinga.

Niliwaita viongozi wa Chadema na kuzungumza nao kisha nikamwita Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo ndugu Sugu alipokuja akanisikiliza kisha tukaketi meza moja na kumtuma kwenda kunyamazisha zile fujo ambazo ndani yake kulikuwa na vimelea vya uhalifu.

Wahalifu walipanga kwenda kuvunja na kuiba katika mabenki hivyo ni jambo ambalo nalikumbuka sana maana halikuwa la kawaida.

Huyo ndiye Kachero Said Salmin Said maarufu zaidi kwa jina la mzee Salmin. Wiki ijayo tutazungumza na wanachama wengine wa CCM ambao wanatajwa kuwa na nia ya kuwania nafasi hiyo ya uenyekiti wa chama hicho mkoa wa Mbeya, nafasi ambayo kwa sasa inashikiliwa na Godfrey Zambi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu 0754 440 749 na Barua pepe kalulunga2006@gmail.com

No comments: