Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Sunday, July 02, 2017

MWAKASOLE: WANA CCM WENGI MBEYA WAMEVUNJWA MIOYOMwanasiasa Jacob Mwakasole.

NA GORDON KALULUNGA

WIKI iliyopita tulifanya mahojiano na Kachero mstaafu wa idara ya usalama wa Taifa (TISS), Said Salimin Said mmoja kati ya wana chama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaotajwa kuwa wanaweza kuwania nafasi ya uenyekiti wa chama hicho mkoa wa Mbeya mwaka huu.

Leo tunaye mwanasiasa Jackob Asanwisye Mwakosole (55) mkazi wa Mbalizi jimbo la Mbeya Vijijini ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya siasa ya chama hicho mkoa wa Mbeya na Ofisa Mahusiano ya kanisa la Uinjilisti Tanzania Makao makuu mjini Mbalizi.

Anasema alijiunga na chama hicho mwaka 1989 na kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika Serikali ya Kijiji cha Mbalizi na baadaye akachaguliwa kuwa diwani wa Kata ya Utengule Usongwe mwaka 1994 mpaka mwaka 2010 alipoamua kung’atuka.

MWANDISHI: Taarifa zinajipambanua kuwa wewe ni mmoja kati ya wanasiasa wakongwe mkoani Mbeya, tunaomba kufahamu nini unakumbuka ndani ya maisha yako ya siasa.

MWAKASOLE: Nianzie wakati wa Prof. Mark Mwandosya na kama Mbunge alikuwa ni kaka yangu wa karibu na nilikuwa karibu naye na kila nafasi aliyogombea nilikuwa nikishirikiana naye.

Nilishiriki naye wakati alipoomba nafasi ya chama kuteuliwa kuwania urais mwaka 2005 lakini baadae hakufanikiwa, basi tukaungana na mpendwa wetu Rais mstaafu Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete.

Kama kuna kura za kujivunia katika uchaguzi Mkuu basi ni kura za CCM kupitia Mheshimiwa Dkt. Kikwete ambaye alipata zaidi ya asilimia 80.

Baadae mwaka 2007 nilimuunga mkono Prof. Mwandosya katika nafasi ya NEC alipowania nafasi hiyo kwa mkoa wa Mbeya na mshindani wake mkubwa alikuwa kijana wetu Thom Apson Mwang’onda.

Hata kama alikuwa kijana mdogo kwa umri lakini alimtoa jasho mzee wetu Mwandosya. Basi tukaona kwasababu Mwango’onda alikuwa mdogo anaweza kupata nafasi zingine tukamchagua Prof. Mwandosya.

MWANDISHI: Unakumbuka kitu gani katika maisha ya kisiasa ya Prof. Mark Mwandosya ulipokuwa jirani naye?   

MWAKASOLE: Baadhi ya mambo machache ambayo naweza kutaja ni kwamba alikuwa mwaminifu sana kwenye chama na mtetezi mkubwa wa wanachi.

Pia alipokuwa mjumbe wa NEC aliiwakilisha vema Mbeya na alikuwa mstari wa Mbele sana kuhakikisha kuwa Mbeya tunapata uwanja wa wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe na alipokuwa Waziri aliusimamia kwa vitendo.

Aliinua Mbeya, aliipenda Mbeya, aliwapenda watu wa Mbeya na alifanya kazi yake akiwa na mapenzi mema na Mbeya na kwa hilo siwezi kumsahau.

MWANDISHI: Mbali na Prof. Mwandosya ni wanasiasa gani wengine mashuhuri unaowakumbuka katika Mkoa wa Mbeya?

MWAKASOLE: Wanasiasa wengi nawafahamu lakini siwezi kumsahau mzee Mkondya, Mwambulukutu, Julius Nswilla na Mulla ambao walikuwa wenyeviti wa CCM kwa nyakati tofauti.

Hawa niliowataja wanaweza kuwawakilisha wengine wakiwemo akina mzee Mwakangale na mzee Mwangoka ambao walikuwa viongozi wa CCM na walifanya kazi zao kwa uaminifu sana.

MWANDISHI: Upinzani unaendelea kukua na CCM inapata changamoto. Kukua kwa demokrasia hii nini maoni yako na anahitajika kiongozi wa namna gani ndani ya CCM Mkoa wa Mbeya kukabiliana na changamoto zilizopo?

MWAKASOLE: Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinakua sana lakini CCM bado ni chama imara zaidi na kinapendwa.

Kinachotakiwa kwa CCM ni kupata kiongozi mahili ambaye anaweza kuwa karibu na wanachama ili kuwajengea mazingira ya watu kuwa na imani zaidi ya chama.

Tungepata kiongozi wa namna hiyo anaweza kufaa zaidi maana naamini kiongozi akiwa karibu na wananchi na wanachama lazima chama kiwe na nguvu.

MWANDISHI: Je akipatikana kiongozi wa namna hiyo, Jimbo la Mbeya Mjini ambalo lipo chini ya Chadema linaweza kurejea CCM?

MWAKASOLE: Kwanza namsifu pia Mwenyekiti wa sasa ndugu Godfrey Zambi ambaye ameongoza chama chetu katika mazingira ya vyama vingi ambapo demokrasia yake ni tofauti na tulikotoka.

Na hata kama kuna wanaombeza kwa kusema viti vingi vimeenda upinzani wanakuwa wanamuonea maana ni nchi nzima hasa katika uchaguzi wa mwaka 2015 ambao ulikuwa ni mgumu.

Nina imani kuwa kwa sasa Mbeya tukipata kiongozi ambaye anaweza kuwaunganisha wana Mbeya vizuri kwa kuwa karibu nao na kuondoa masuala ya kutofautiana katika mambo ya ukabila anaweza kwenda vizuri na kuleta mabadiliko makubwa.

Mwaka aliochaguliwa Sugu (Joseph Mbilinyi) Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, watu walimchagua kwa hasira maana yeye hakuwa mwana siasa.

Chama hakikupokea vema ushauri wa wanachama ambao ndiyo wanafanya kampeni basi waliamua kuonyesha hasira zao kwa kuongeza nguvu upande mwingine. Tukapata maumivu makubwa.

MWANDISHI: Mwaka 2005 umesema ulikuwa unamuunga mkono Prof. Mwandosya katika kampeni za ndani ya chama chenu alipohitaji kuwania urais. Je Mwaka 2015 pia ulikuwa naye na je wanaoitwa wasaliti unawazungumziaje?

MWAKASOLE: Mwaka 2015 nilitambua kuwa makundi hayo hayakuwa mazuri na niliona dalili za kukigawa chama hivyo sikujihusisha na kundi lolote na alipoteuliwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli nikaungana naye kupiga kampeni.

Kwa wanaohisiwa kuwa wasaliti niombe chama kitumie hekima kuwachambua ili watu wasisingiziwe na hapo tutafanikiwa sana maana inaweza kutumika mwanya huo kwa wasiopendana kutajana bila uwepo wa ushahidi. Hekima inamaliza yote.

MWANDISHI: CCM imekataza watu kujitangaza kutaja nafasi wanazopenda kuziwania, lakini baadhi ya wana chama na wasio na vyama wanataja baadhi ya majina likiwemo jina lako kuwa waweza kuwania nafasi ya Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya. Tetesi hizi zikoje?

MWAKASOLE: Mimi sijatangaza nia ila nina mpango huo. Naheshimu sana taratibu za chama na wamezuia kutangaza nia ila mtu kuwa na mpango hawajazuia.

Ndoto yangu ni kukifikisha chama mahala pake na kuwafanya watu wengine hasa vijana kuwa wanasiasa kwa siasa za ustaarabu za kupinga rushwa. Naifahamu CCM. Naifahamu Mbeya na chama kikituruhusu kusema neno nitasema maana ninaweza na nimejipima.

Na yale ambayo yanawavunja moyo wana CCM wengine naamini nitayamudu maana nina hofu ya Mungu na ninafahamu siasa za pande zote za mkoa wa Mbeya maana nilipita kuwasaidia wabunge wangu mwaka 2015 na ni mlezi wa wilaya ya Mbozi.

MWANDISHI: Kitu gani chama kinatakiwa kufanya juu ya vijana ambao wengi wanakimbilia upinzani na wengine kuacha siasa

MWAKASOLE: Kwa kweli katika suala hili napenda kuwa wazee waliopo katika nafasi za chama waweze kuwapisha na vijana wetu kwasababu urithi wa chama ni vijana na chama kikikosa kuwaambukiza vijana hekima hakiwezi kuwa imara siku za usoni.

MWANDISHI: Kuna taarifa kuwa baadhi ya vijana wakiambiwa wawanie nafasi ndani ya chama hawataki, je unafikiri tatizo ni kutoandaliwa au nini kimetokea hapo katikati?

MWAKASOLE: Tunaendelea kuwaomba vijana kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali, labda wanaotoa ushawishi kwa vijana hao hawajaenda katika mpango unaoeleweka.

Maoni yangu ni kwamba chama changu kiendelee kujenga mahusiano na wanachama wake na kuwatia moyo wale ambao wanaonekana kuwa wamevunjika mioyo ili wajisikie kuwa nao wanathaminika maana chama siyo cha mtu bali ni cha wote.

Mbali na hayo yote, ni vema tukaungana na viongozi wetu wanaokemea rushwa kwa vitendo kwasababu rushwa imefanya chama kidumae kwa kuwapata baadhi ya viongozi wasio sahihi kwasababu ya pesa na kuwaacha viongozi wazuri kwasababu hawana pesa. Tuimarishe jumuiya zetu.

Namshukuru pia Mmisionari Mchungaji Marcus Lehner wa Kanisa la Uinjilist Tanzania kwa kuwa Mwalimu wangu mwema wa uongozi kwa kupenda watu na kuwaunganisha.

Mwandishi wa makala anapatikana kwa simu namba 0754 440 749 na barua pepe ni kalulunga2006@gmail.com

No comments: