Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Friday, October 20, 2017

MWENYEKITI WA KIJIJI MBEYA ADAI KUPIGWA RISASI


Mwenyekiti wa Kijiji cha Ilota wilaya ya Mbeya Mkoa wa Mbeya Patson Tembwele akiwa katika Hospitali ya Ifisi Mbalizi baada ya kujeruhiwa mkono wake wa kushoto na mguu wa kulia kwa kitu kinachodhaniwa kuwa ni risasi.


NA GORDON KALULUNGA, MBEYA

MWENYEKITI wa Kijiji cha Ilota Kata ya Mshewe wilaya ya Mbeya Jimbo la Mbeya Vijijini Patson Tusaline Tembwele, amelazwa katika Hospitali teule ya Wilaya hiyo Ifisi Mbalizi baada ya kupata majeraha yanayodhaniwa kuwa ni ya risasi.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi katika Hospitali hiyo, kiongozi huyo alisema tukio hilo lilitokea Octoba 18 mwaka huu, majra ya saa 2 usiku huko Ilota alipokuwa akitoka matembezini na kurejea nyumbani akiwa anaendesha pikipiki yake.

“Siku hiyo nilitoka kwa Mke wangu mdogo Mbalizi na kurudi Ilota ambapo baada ya kupitia kilabuni na kuanza kuelekea nyumbani ndipo nikasikia mlio wa bunduki na kuishiwa nguvu katika mkono wangu wa kushoto ambako nilipigwa risasi eneo la msuli wa mkono na mguuni juu kidogo ya kisigino cha kulia na kuanguka” alisema Patson.

Alisema baada ya kuanguka na wavamizi wake kumkimbilia ndipo akaamua kuinuka na kukimbia mpaka katika nyumba yake ambako alimwamsha mkewe na kumweleza kilichomtokea na kwamba kati ya watu watano waliomvamia wawili aliwatambua kuwa ni nduguze ambao awali walikuwa wana visa nae wakimtuhumu kwa ushirikina baada ya marehemu shangazi yake kuota ndoto kuwa alihisi ndiye mbaya wake na waliwahi kumtamkia maneno ya vitisho kabla ya tukio hilo.

“Walipoamka ndugu zangu na majirani nikapata msaada wa kupelekwa Polisi ambako nilijitambulisha kuwa ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Ilota, nikapewa msaada wa haraka kukimbizwa Hospitali na tayari nimepigwa picha nimeambiwa ndani ya mkono kuna risasi na mfupa umevunjika hivyo watanifanyia upasuaji” alisema Mwenyekiti huyo.

Katibu wa Hospitali hiyo Emmanuel Martin alisema kuwa mgonjwa huyo anaendelea kupatiwa matibabu wakati taratibu zingine za kisheria zikichukuliwa na mamlaka zinazohusika huku diwani wa Kata ya Mshewe Esther Mbega akimuombea kupona haraka kiongozi huyo.

No comments: