Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Saturday, November 18, 2017

MSIMU WA KILIMO TANZANIA, PEMBEJEO FEKI ZADAIWA KUZAGAA*Baadhi wauziwa unga wa tofali za kuchomwa........NA GORDON KALULUNGA, MBEYAKUELEKEA msimu wa Kilimo nchini, imebainika kuwepo kwa mbegu na madawa feki wanayouziwa wakulima kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kwa lengo la kujitajirisha.Uchunguzi wa kina uliofanywa na Mwandishi wa habari hii umebaini kuwepo kwa dawa feki za kuhifadhia nafaka hasa mahindi na maharage.Wafanyabiashara hao, ambao baadhi yao kwa sasa hawakamatiki kutokana na utajiri walioupata kwa njia hiyo, wanadaiwa kusaga matofali yaliyochomwa  kisha unga wake kuhifadhiwa kweye mifuko kama dawa za kuulia wadudu wanaoharibu mimea na matunda ya Kahawa.Taarifa za ndani zinaeleza kuwa unga wa matofali hayo unauzwa kama dawa aina ya Red Copper huku Copper ya kuhifadhia mbegu za Pamba wanauza kama Copper ya kutibu magonjwa ya kahawa aina ya CBD jambo ambalo linawaumiza wakulima.Copper hiyo wakulima wakiikoroga kwenye maji inatuama chini ya chombo cha kuchanganyia kwasababu siyo Copper halisi ya kuchanganya na maji na wakulimwanaikimbilia kwasababu ni bei rahisi na hawana elimu ya kutosha kuhusu dawa hizo.Kwa upande wa mbolea imeelezwa kuwa baadhi yao wanachukua mbolea aina ya Minjingu ya punje inayouzwa chini ya Tsh. 10,000/= na kuweka katika mifuko ya DAP kisha kuiuza zaidi ya Tsh. 65,000/=.Wanafanya hivyo kwasababu mkulima anapotumia mbolea hiyo hawezi kugundua mpaka pale mazao yatakapokuwa yameanza kuharibika yakiwa shambani.Mbegu za mahindi, wamekuwa wakichukua mahindi ya kawaida na kuyachanganya na Copper ya kuhifadhia mbegu za pamba na Copper ya kawaida kisha kuhifadhi kwenye mifuko ya makampuni ya utafiti na kuwauzia wakulima.Mtaalam wa masuala ya pembejeo kutoka kampuni ya Bager, ambaye aliomba hifadhi ya jina lake kwa madai kuwa ni kwa usalama wake, anathibitisha kuwepo kwa mchezo huo mchafu kwa muda mrefu.Anasema mbali na mbolea na mbegu hizo kuchakachuliwa, wafanyabiashara hao wasio waaminifu pia wanachakachua sumu ambapo jina la sumu linalokuwepo kwenye kopo ni tofauti na dawa inayokuwemo ndani.“Kwa upande wa sumu, wanachukua dawa aina ya Sumision na kuweka katika makopo ya sumu aina ya Daksban’’alisema.Alisema hali hiyo imeendelea kushika kasi kutokana na mambo mawili, likiwemo suala la rushwa kwa wakaguzi au wakaguzi hao kutokagua kabisa maduka ya pembejeo hizo za kilimo ama kukaa muda mrefu bila kufanya ukaguzi hali ambayo inawapa mwanya wafanyabiashara hao kuendelea na mchezo huo.

May 25 mwaka huu wakulima wa zao la Kahawa wilaya ya Mbeya walilalamikia uzagaaji wa pembejeo feki katika maduka mbalimbali wilayani humo zinazoathiri mazao yao.Hayo waliyasema katika mkutano mkuu wa chama cha ushirika Usongwe AMCOS uliofanyika katika ofisi za chama hicho zilizopo Kijiji cha Iwindi wilayani humo.Akichangia hoja katika mkutano huo, mkulima Julius Mzumbwe, alisema kuwa inashangaza kuona uongozi wa chama hicho unawauzia pembejeo kwa ongezeko la Shilingi 500 tofauti na gharama wanayouza katika maduka ya watu binafsi.Akijibu hoja hiyo, Katibu msaidizi wa ushirika huo Godfrey Mwakalonge alisema kuwa hali hiyo inatokana na uendeshaji pia pembejeo wanazowapatia zinakuwa hazina shaka katika ubora wake.“Ndugu zangu wajumbe, mbali na gharama za usafiri, upakiaji, upakuaji na ugawaji, lakini tunazingatia ubora wa pembejeo tofauti na kuzinunua kwenye maduka kama mnavyokumbuka tumewahi kununua pembejeo kwa akina Kalinga Agro yaliyotukuta sote ni mashahidi kumbe Coper walituuzia matofali” alisema Mwakalonge.Akikazia jawabu hilo, Mwenyekiti wa bodi ya ushirika huo Jailos Mwashigala alisema mbali na pembejeo nyingi madukani kuwa feki, pia wafanyabiashara wanapunguza ujazo kwa kila pembejeo zikiwemo mbegu na dawa mbalimbali.“Mkitaka kujua zaidi waulizeni wakulima wa vijiji vya Shongo na Holongo Kata ya Igale hao wanajua zaidi athali za kununua pembejeo katika baadhi ya maduka ya pembejeo hasa yaliyopo Mbalizi” alisema Mwenyekiti huyo.Mbunge wa kwanza wa jimbo la Mbeya aliyetawala kwa miaka 15, ambaye pia ni mwasisi wa chama hicho cha ushirika mwaka 1968 Patrick Nswilla alipohojiwa na na JAMHURI alisema pembejeo feki zinazidi kushamiri wilayani humo kutokana na vitendo vya rushwa.“Tangu muda mrefu wakulima wanalalamika maana wafanyabiashara huwa wanasaga matofali ya kuchomwa na kuyaweka kwenye mifuko wakiuza kama Copper huku unga huo wa matofali wakipaka mahindi na kuziuza kama mbegu bora” alisema Nswilla.Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini Oran Manase  Njeza alipoulizwa kama anafahamu kadhia hiyo alisema kuwa kosa hilo ni la jinai na amewataka wakulima ambao wanapata matatizo hayo wayapeleke Polisi ili hatua ziweze kuchukuliwa.“Kuwepo  kwa pembejeo feki ni kosa la jinai. Hiki ni kilio Tanzania nzima na wabunge wote tumeendelea kupiga kelele” alisema Njeza.Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Mbeya Mareselin Mlelwa alipohojiwa alisema kwa sasa yeye amehamishiwa katika Halmashauri ya Busokelo.“Kwa sasa mimi nimepata barua ya uhamisho nipo Busokelo lakini idadi ya maofisa ugani kwa wilaya ya Mbeya jumla ni 119 na kuhusu pembejeo feki huwa tunawaambia wakulima wanaponunua wadai risiti na wakitumia waache hata punje 20 kwa ajili ya ushahidi lakini hawafanyi” alisema Ofisa huyo aliyekuwa Mbeya Vijijini.Alieleza kuwa hata hivyo serikali inajipanga kufanya ukaguzi kwenye maduka yote hasa kipindi hiki cha msimu wa kilimo na tunawashauri maofisa ugani kuwaelekeza wakulima kuhusu kuwa makini.Upande wake Ofisa Kilimo wa Mkoa wa Mbeya Enock Nyasebwa alipotafutwa kwa njia ya simu alisema kuwa hawezi kulizungumzia jambo hilo kwasababu yupo mapumziko.JAMHURI liliutafuta uongozi wa Kampuni ya Kalinga Agro ya mjini Mbalizi ili kutolea ufafanuzi wa tuhuma zilizotolewa katika mkutano wa AMCOS, ambapo Meneja wa oparesheni wa kampuni hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Albert alisema tuhuma hizo wamezipata mara kadhaa lakini wao hawahusiki na kama kuna mkulima mwenye malalamiko aweze kujitokeza akiwa na stakabadhi wanazotoa katika maduka yao.

No comments: