Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Thursday, December 07, 2017

IFISI HOSPITALI YAPANDISHWA HADHI NA KALULUNGA, MBEYA

HOSPITALI teule ya Wilaya ya Mbeya Mbalizi Ifisi inayomilikiwa na Kanisa la Uinjilisti Tanzania, imepandishwa hadhi kutoka Nyota mbili na kufikia Nyota Nne.


Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dr. Martin Mbwile, alisema walistahili kuwa na hadhi ya Nyota Tano lakini asilimia 6 pekee ya vigezo vyote ndiyo imewakwamisha.

Alisema vigezo vilivyokuwa vikitazamwa ni pamoja na huduma ya Mama na mtoto, Rasilimali watu na vifaa tiba, upatikanaji wa dawa na uongozi wa Hospitali unavyofanya kazi.

“Katika maeneo hayo tulipata alama (A) kwa huduma salama na rafiki kwa wagonjwa, utawala na uwajibikaji katika kuwasikiliza wagonjwa, uedeshaji wa huduma kwa uwazi na uwajibikaji, jambo ambalo tunajivunia” alisema Dr. Mbwile ambaye ni kijana na anaongoza safu ya watumishi vijana zaidi ya asilimia 95 waliopo katika Hospitali hiyo.

Alilitaja eneo ambalo limewakwamisha kwa asilimia 6 kufikia hadhi ya Nyota Tano kuwa ni eneo la idadi ya watumishi na uchache wa majengo.

“Tunaishukuru Wizara ya Afya na shirika la wajerumani liitwalo GTZ kwa miongozo yao na tumejipanga kufanya kazi kutokana na hadhi ya Hospitali na ikumbukwe hii ni Hospitali ya Rufaa kutoka vituo vya Afya vilivyopo katika Wilaya yetu” alisema Daktari huyo.

Baadhi ya wagonjwa waliohojiwa akiwemo Suzana Frank, alisema kuna mabadiliko makubwa ikiwemo kauli za watoa huduma ambapo kwa sasa wanahojiana vizuri na hata uongozi wa Hospitali akiwemo Katibu wa Hospitali hiyo Emmanuel Martin anawatembelea wagonjwa wa nje (OPD) na hata wa ndani na kuwauliza kama wanapatiwa huduma au kama kuna malalamiko.

“Hali kwa sasa hapa ni nzuri tofauti na mwanzo ingawa changamoto ni suala la malipo kwa kadi za benki ya CRDB ambazo ukifika kwa mara ya kwanza hata kama unataka kupima Malaria tu unatakiwa ulipie Tsh 8,000 bila ufafanuzi” alisema mgonjwa huyo.

Akitolea ufafanuzi suala hilo, Dr. Martin Mbwile alisema kadi hiyo inasaidia kudhibiti mapato ya taasisi na mgawanyo wake ni kadi inauzwa Tsh 2,500, kufungua File ni 5,000 hivyo ndiyo maana wagonjwa wanaambiwa watoe hiyo Tsh 8,000 ambapo kadi hiyo ukiweka fedha kwa hapa Mbeya utatibiwa hapa kwetu, Mwambani, Ilembula na Hospitali ya Rufaa ya Mbeya bila kuinunua upya.


Katibu wa Hospitali hiyo Emmanuel Martin alisema wanajivunia kufikia kiwango hicho na matarajio yao ni kuwa ni hospitali ya kimataifa.Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali hiyo ambaye pia ndiye Mshauri Mkuu wa miradi ya Kanisa la Uinjilisti Tanzania Mchungaji Marcus Lehner, alisema wamefikia hapo baada ya kupitia changamoto kadha wa kadha.

“Haikuwa rahisi kufikia mafanikio hayo na niseme Hospitali yetu kwa sasa ina mashine za kisasa zikiwemo mashine za X-Ray ambazo hata kwa nchi za Ulaya ndiyo wanazitumia kutokana na ubora wake” alisema Mch. Lehner.

Alisema kwa Tanzania wao ni miongoni mwa Hospitali zenye mashine bora kabisa ya X-ray ambayo wameipata kwa msaada wa wafadhili kutoka hospitali ya Uswis. 

Hospitali hiyo ilifunguliwa rasmi mwaka 2008 na Rais wa awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

No comments: