Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Thursday, December 07, 2017

SUMU INAYOSABABISHA KANSA YAPATIKANA KWENYE MAHINDI

·       Ni kupitia Mahindi na Karanga


·       Sumu za kuhifadhia mazao zatajwa


·       TBS na TFDA walonga


NA GORDON KALULUNGA, MBEYAHATARI ya ongezeko la maradhi ya saratani (kansa) imezidi kuongezeka nchini kutokana na sumu inayodaiwa kuwemo katika nafaka hususani Mahindi na Karanga, KALULUNGA BLOG imebaini.Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa watanzania wengi wanatumia mahindi yaliyohifadhiwa kwa sumu aina ya Acteric ya maji badala ya Acteric  super Dust 100mg za unga ambapo sumu hiyo ya maji ni maalum kwa ajili ya kuua wadudu kwenye mimea na wala siyo kwa ajili ya kuhifadhia punje ili zisiharibiwe.Sumu hiyo ikiingia kwenye kiini cha punje ya mahindi huwa siyo rahisi kutolewa hivyo inatengeneza ukungu kwenye punje na kusababisha sumu aina ya SUMU KUVU maarufu kwa jina la kitaalam kama Aflatoxin ambayo binadamu akila inasababisha kansa ya ini ambayo haina dawa.
Mamlaka ya chakula na dawa nchini (TFDA) inathibitisha kupatikana sumu kuvu katika punje za Mahindi na Karanga ambazo zinahifadhiwa bila kukauka vizuri au kuwa na unyevu.Meneja wa TFDA kanda ya Nyanda za juu kusini, Rodney Alananga alipohojiwa alisema sumu kuvu inatokana na aina ya ukungu (fangasi) kwenye punje unaoota zaidi kwenye mazao kama mahindi na karanga.Alisema binadamu anaweza kupata madhara ya kiafya endapo atakula chakula kilichochafuliwa na sumu kuvu kwa kiwango kisichovumilika.“Dalili na madhara yatokanayo na sumukuvu ni pamoja na saratani ya ini, maumivu ya tumbo, kutapika, kuvimba tumbo, homa, kuharisha, kuwa manjano sehemu mbalimbali za mwili, degedege, kupungua kwa kinga mwili, udumavu kwa watoto na kupoteza maisha” alisema Alananga.Alizitaja njia za kuzuia sumu hiyo katika mazao kuwa ni pamoja na kutumia viatilifu vilivyothibitishwa katika dalili za awali za mazao kushambuliwa na wadudu, kuhakikisha mazao yanavunwa kwa wakati na kuondolewa shambani kisha kuanikwa pasipo kugusa udongo na sakafu.“Hakikisha usafi wa mahindi kabla ya kusaga na hifadhi unga kwenye chombo safi kisichoruhusu unyevunyevu, zuia wanyama waharibifu kama vile panya wakati wa kuhifadhi na chambua kuondoa taka mbegu hafifu, zenye ukungu, zilizopasuka, zilizooza, zilizobadilika rangi” alisema kiongozi huyo.Hata hivyo uchunguzi zaidi umebaini kuwa mbali na madhara hayo, baadhi ya wakulima hawachukui tahadhali kutokana na uhalisia kuwa asilimia 60 ya wakulima wazalishaji wa chakula nchini ni wale wa jembe la mkono ambao wanazalisha mazao ya chakula kwa asilimia 90.Asilimia 40 ya mazao ya wakulima hao yanapotea kwa njia mbalimbali kabla ya kumfikia mlaji wa mwisho ikiwemo uharibifu wa wadudu hivyo mkulima mdogo anashindwa kumudu kununua mifuko maalum ya kuhifadhia nafaka kwa Tsh. 4,000/=.Mkulima Sanke Lubhole wa Mbeya Vijijini anasema licha ya ubora wa mifuko ya kuhifadhia nafaka mbalimbali kwa ajili ya kuzuia wadudu waharibifu, punje za mahindi zinazohifadhiwa katika mifuko hiyo zikipandwa huwa hazioti.“Changamoto kubwa ya hiyo mifuko ni pale msimu wa kilimo unapofika ukienda kupanda zile punje hata kama hazijabunguliwa huwa hazioti na mimi ilinitokea mwaka jana hivyo tunalazimika kununua mbegu madukani kila unapofika msimu wa kilimo” alisema Mkulima huyo.


Hivi karibuni Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeyarudisha Mahindi yenye sumu yaliyoingizwa nchini kupitia mpaka wa Tunduma Mkoani Songwe yakitokea nchini Zambia.


Meneja wa TBS kanda ya Nyanda za juu kusini Abel Mwakasonda alisema katika kipindi cha Mwaka mmoja tangu Shirika hilo lifungue ofisi katika Kanda hiyo, limeweza kupima sampuli 2000 za bidhaa mbalimbali.“Tumeweza kupima sampuli 2000 ambapo chini ya sampuli 10 tulibaini kutokuwa na viwango na kurudisha zilikotoka hasa nje ya nchi yakiwemo Mahindi yenye wadudu” alisema Mwakasonda.Akifafanua athari ambazo zingeweza kujitokeza kwa watumiaji endapo Mahindi hayo yangefanikiwa kusambazwa nchini, alisema wangeweza kupata athari za magonjwa ya kansa za viungo kutokana na sumu iitwayo Sumu kuvu inayokuwemo kwenye nafaka ambayo ni jamii ya fangasi.Mbali na Mahindi hayo, alitaja sampuli zingine ambazo zilikataliwa kutokana na kubaini mapungufu kuwa ni pamoja na vifaa vya umeme zikiwemo nyaya, vifaa vya ujenzi na vipodozi.

No comments: