Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Monday, January 22, 2018

Mbunge Sugu azidi kuishi Gerezani

Na Ezekiel Kamanga,  Mbeya

Kesi namba 12/2018 inayomhusu Mbunge wa Mbeya mjini Joseph Mbilinyi na Emmanuel Masonga Katibu CHADEMA Kanda ya Nyasa wanayotuhumumiwa kumfedhehesha Rais imeanza kusikilizwa leo Mahakama ya Mkoa mbele ya Hakimu Mfawidhi Michael Mteite.

Upande wa mashitaka ukiongozwa na Joseph Pande Wakili Mkuu wa Serikali akisaidiwa na Baraka Mgaya pamoja na Othman Mtenga wakati watuhumiwa wanatetewa na wakili Msomi Boniphace Mwabukusi akisaidiwa na Wakili Hekima Mwasiku pamoja na Sabina Yongo.

Mashahidi watatu wa upande wa mashitaka wameanza kutoa ushahidi wao akiwemo Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mbeya mjini Keneth James Chacha,Boniphace Mwaitolola(34)mkazi wa Soweto jijini Mbeya na Afisa Upelelezi William Nyamakomage kutoka ofisi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya.

 Shahidi wa kwanza ameiambia Mahakama kuwa alipata barua ya taarifa ya mkutano Disemba 27 mwaka jana na kuidhinisha Disemba 29 na mkutano kuruhusiwa kufanyika Disemba 30 mwaka jana ambapo pia taarifa zilitolewa kwa Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC),Afisa Upelelezi Mkoa (RCO),Afisa usalama wa Taifa Wilaya ya Mbeya na Mkuu wa Wilaya na kutoa maelezo kuwa mkutano wa Mbunge yasiwepo matusi wala kuitukana Serikali.

 Hata hivyo James Chacha amesema kuwa alipata taarifa kutoka kwa walinzi wa usalama juu ya watuhumiwa kumtukana Rais. Chacha aliwasilisha barua zote kama kielelezo ambazo zote zimepokelewa kama ushahidi. Shahidi wa pili Boniphace Mwaitolola ameiambia Mahakama kuwa alikuwepo eneo la mkutano na kwamba aliwasikia watuhumiwa wakitukana hali iliyomchukiza kwa kutukanwa Rais.

Kesi imeahirishwa baada ya saa moja ambapo upande wa mashitaka utaleta mashahidi wengine.

Hata hivyo baada ya ahirisho la muda Afisa Upelelezi kutoka ofisi ya Kamanda wa Polisi William Nyamakomage  ameiambia Mahakama kuwa Disemba 30 mwaka jana alipata taarifa kutoka kwa RCO ASP Modestus Chambo kwenda katika mkutano uliopangwa kufanyika siku hiyo viwanja vya shule ya msingi Mwenge ambapo alifika saa 10:30-10:45 jioni ambapo akiwa mita thelathini au zaidi ya hapo aliwasikia Mbunge Joseph Mbilinyi na Katibu Emmanuel Masonga wakitoa maneno ya kumfedhehesha Rais John Pombe Magufuli kama watu wengi wanauawa, wengine wanatupwa kwenye viroba na wengine kutekwa kama Roma, Benn Saanane pia mheshimiwa Sugu kuzuiwa kuongea.

Baada ya kusikilizwa kwa mashahidi hao Hakimu Michael Mteite aliahirisha kesi hadi Januari 23 mwaka huu upande wa mashitaka utakapoleta mashahidi wengine.Mbunge na Katibu walipelekwa mahabusu ya Gereza la Ruanda.

No comments: