Social Icons

ad3

ad3

ad2

ad2

ad1

ad1

Sunday, March 18, 2018

SAUTI YA NYIKANI......... Rais Magufuli watibu Watanzania kwa Tsh 70,000
NA GORDON KALULUNGA

MAENDELEO ya kiuchumi ya Taifa lolote hutegemea zaidi ubora wa afya za wananchi wake kwa hiyo mifumo ya afya inayoimarisha upatikanaji, ufanisi, urahisi wa kuzifikia na kuzimudu gharama za matibabu ni muhimu katika kuondoa sio tu janga la maambukizi  ya magonjwa bali pia kuondoa ufukara miongoni mwa wananchi.Utoaji wa huduma za afya kwa watu wote (Universal health Coverage) ni wazo liliasisiwa na katiba ya Shirika la afya duniani ya mwaka 1948 iliyoazimia ya kwamba huduma bora za afya ni haki ya msingi ya kila mtu na mpango wa afya kwa wote ni azimio la Alma Ata lililopitishwa mnamo mwaka 1978 na Tanzania ilisaini maazimio hayo.Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya duniani (WHO) ya mwaka 2005, mzigo wa kugharamia huduma za afya kwa malipo ya pesa taslimu kutoka mifukoni inapelekea watu milioni mia moja kuingia kwenye lindi la umaskini kila mwaka.Wengi wao wapo katika nchi za kusini mwa jangwa la sahara ikiwemo Tanzania na sababu kubwa ikiwa ni mifumo dhaifu iliyopo ya kugharamia huduma za afya na bima za afya na matokeo yake ni kuongezeka kwa maambukizi  ya magonjwa na kupungua kwa nguvu kazi ya Taifa.Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Benki ya Maendeleo ya Afrika mwaka 2010 nchini Rwanda, malipo ya pesa taslimu na gharama kubwa za huduma za afya ilisababisha wananchi kupunguza matumizi ya huduma za afya kwani idadi ya wagonjwa waliojitokeza katika vituo vya afya ilipungua sana kwa kuwa wengi wao hawakumudu kulipia huduma za afya.Utafiti uliofanywa na Onah na Govendor mwaka 2014 nchini Nigeria ilibainika kuwa baadhi ya mambo yanayosababisha kuwepo na utofauti katika kuzifikia huduma za afya kwa makundi hatarishi hasa akina mama wajane ni mifumo mibaya ya kugharamia huduma za afya na gharama kubwa za afya.Baadhi ya waliohojiwa  katika utafiti huo walieleza kuwa inapotokea wanapata maambukizi ya magonjwa na wakati huo hawana pesa ya kulipia vipimo pamoja na dawa, hulazimika kuchukua akiba ya pesa ya chakula, ada
ya shule au mtaji wa biashara anayoifanya ili kugharamia huduma hizo, hata hivyo atahudhuria hospitali endapo tu ugonjwa huo utakuwa mkubwa au homa hiyo itakuwa kali sana.Hali hii pia inawakumba wananchi wa Tanzania kwani huduma za afya ni ghali mno na wengi wao hawawezi kuzimudu. (Nazungumzia masikini) ila sina uhakika na baadhi ya waajiriwa wa vyama vya siasa ikiwemo CCM.Ripoti ya wizara ya afya na ustawi wa jamii ya mwaka 2004, inaeleza kwamba mara baada ya uhuru, Serikali ya Tanzania kupitia wizara ya afya ilianza kutoa huduma za afya bure kwa wananchi wote.

Lakini kufuatia mdororo wa kiuchumi katika miaka ya sabini, kuongezeka kwa idadi ya watu na kuongezeka kwa maambukizi ya magonjwa mapya ilipelekea serikali kushindwa kuendesha hospitali na vituo vya afya katika ngazi zote na hivyo kuleta matatizo makubwa katika mfumo wa afya.Ni katika miaka hiyo ndipo serikali ilianza kufikiria mfumo wa uchangiaji wa huduma za afya kwa kuanzisha ada ya kutumia huduma za afya yaani user fee, Bima za afya kwa wafanyakazi na wasio wafanyakazi hata hivyo baada ya miaka 50 ya uhuru tatizo bado ni kubwa na mifumo hiyo haijafanikiwa na sababu ikiwa ni gharama kubwa za dawa na vifaa tiba.Hata sasa kati ya wagonjwa kumi ambao wanafika hospitali na kutakiwa kulipia Tsh 10,000/= kununua dawa wanaomudu huwa hawazidi wagonjwa watano, na watano wengine aidha hawanunui kabisa au wanaomba wanunue nusu dozi kwanza na nusu dozi nyingine wakiahidi kununua pindi wapatapo pesa.Nimewahi kufanya utafiti, moja ya swali nililododosa ni hili, (unafikiri nini kinaweza tokea endapo mtu ambaye hana uwezo wa kulipia gharama za afya ataumwa?).Wengi wao walijibu ya kwamba mambo mawili yanaweza kujitokeza, moja kama ana akiba itabidi atumie akiba yake katika matibabu na hivyo kuendelea kuwa maskini zaidi au pili kukosa matibabu na hivyo kupoteza maisha.

Tafsiri yake ni kwamba gharama kubwa katika upatikanaji wa huduma za afya kwa watu wenye kipato cha chini unapelekea kuongezeka kwa umaskini miongoni mwa wananchi na kuongezeka kwa idadi ya vifo na hivyo kupoteza nguvu kazi ya Taifa.

Nakumbuka vema Rais wa Tanzania wa awamu ya tano, Dkt. John Pombe Magufuli, Agosti 23, mwaka 2015, wakati chama chake (CCM) kikiwa kinazindua kampeni katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam, alisema anakerwa na atashughulikia suala la ukosefu wa dawa katika hospitali zetu hapa nchini.

Ameanza vizuri sana chini ya Waziri shupavu Ummy Mwalimu licha ya changamoto zinazoendelea kufanyiwa kazi.

Mbali na dawa kuna suala la Bima za Afya ambapo zipo za mafukara ziitwazo Bima ya Afya ya jamii (CHF) ambayo inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kutotambuliwa pale mgonjwa anapotakiwa kulazwa, anapopatwa na ugonjwa nje ya wilaya aliyopatiwa kadi hiyo au kupata baadhi ya vipimo na dawa hata ndani ya wilaya husika.

Pia zipo bima za watanzania wenye hadhi ziitwazo Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) ambazo zinamwezesha mwenye kadi ya bima hiyo kutibiwa popote.

Kwa kuwa nchi yetu ni ya ujamaa na inajali utu na hadhi ya uswa wa binadamu, kama inaweza kumpendeza Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli na mamlaka zake ni vema kuliangalia jambo hili na ikiwezekana kupitia mfuko huo wa Bima ya Afya ya Taifa, watanzania waweze kukata bima zenye hadhi ya kutibiwa popote kwa shilingi hata 70,000 kwa kila mwaka.

Kwa sasa kuna bima ya watoto kupitia mfuko huo ambayo haizidi Tsh 55,000 kwa mwaka, hivyo nadhani ni vema sasa kama taifa tukawa na usawa au kupunguza “Gape” la masikini na walionacho kupitia huduma za Afya.

Na katika suala la Toto Afya kadi, inadhihilisha kabisa kuwa utoaji wa matibabu bure kwa watoto chini ya miaka Mitano kama ilivyo katika sera ya Afya ya mwaka 2007 tumeshindwa na ushahidi wa hili upo wazi.

Hivyo ni rai yangu kwa Mheshimiwa Rais Dr. John Pombe Joseph Magufuli kama itampendeza akaamuru watanzania wanaohitaji kadi za matibabu za NHIF wakalipa kwa bei niliyoipendekeza au chini ya hapo kwasababu siyo kila mmoja atakayekuwa na kadi hiyo ataumwa kwa mwaka huo.


Nimeona niandike makala hii kwasababu mifumo ya kugharami huduma za afya hapa nchini na soko holela la dawa na vifaa tiba inasababisha uwepo wa bei kubwa ya dawa na vifaa tiba katika sio tu hospitali zetu bali na maduka ya dawa binafsi.

Pia sababu nyingine iliyonisukuma ni baada ya kuona huduma za afya zinazidi kutolewa katika mtazamo wa kibiashara na sio mtazamo wa kihuduma (Business oriented and not service oriented.)

Wakati Maandiko yanasema kuwa hekima ya masikini huwa haisikilizwi, bahati nzuri tuliyoipata Watanzania, Rais wetu anasikiliza hekima za masikini.

Karibuni Nyikani.

Mwandishi wa makala hii ni mbobezi wa Habari za uchunguzi katika nyanja za Afya ya Uzazi, Dawa za kulevya na Viwanda.

Anapatikana kwa anuani yake
       Gordon Kalulunga(Development Journalist),
    Information and Media Consultant,
    P.O. Box 705, Mbeya-Tanzania.
    CELL: 255 (0)754 440749/ WHATSApp 255 (0)765 615858
    E-MAIL: kalulunga2006@gmail.com

No comments: